The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hivi Wachezaji Wazawa Hawazidai Klabu Zinazowaacha?

Sitaki kuamini kuwa mikataba ya wachezaji wazawa ni mizuri kiasi kwamba maslahi yote ya mchezaji hushughulikiwa bila ya matatizo anapomaliza mkataba wake au kuachwa.

subscribe to our newsletter!

Karibu wiki nne zilizopita nilikwenda kushiriki bonanza la wachezaji wastaafu wa soka kwenye Uwanja wa Gwambina, Chang’ombe, wilayani Temeke ambako nilionyeshwa mchezaji mmoja aliyekuja uwanjani hapo, lakini kwa malengo tofauti.

Wakati sisi tulienda kuburudika na mpira wa wazee, yeye, ambaye namuhifadhi jina, alifika hapo kuvizia viongozi wa timu moja ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuwadai haki zake.

Niliumia! Kweli niliumia kwa kuwa nilijua isingekuwa rahisi viongozi hao kutekeleza matamanio yake pale Gwambina (zamani TCC), tena kwenye shughuli ya kujifurahisha kwa kucheza mpira wa wazee na baadaye kuburudika kwa vinywaji na muziki.

Huyu ni kijana anayedai haki zake na si kutafuta huruma au upendeleo kwa viongozi na hivyo hastahili kuvizia watu wanaoongoza klabu iliyosajiliwa na inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Anaidai timu ambayo imesajiliwa na Serikali na inashiriki ligi inayoendeshwa na shirikisho lililosajiliwa na lenye kila kanuni inayoweza kulinda haki zake zote kama mchezaji. Inaendeshwa na shirikisho lenye ofisi na wafanyakazi waliopo kazini muda mwingi wa siku na wanaojua ofisi za klabu ambayo haijamlipa haki zake mchezaji huyu.

SOMA ZAIDI: Tujipe Muda Kabla ya Kuanza Kuitumia V.A.R

Sijui ni kwa nini mchezaji huyu aliamua kuvizia viongozi badala ya ama kwenda ofisini kwa klabu yake kuwasilisha rasmi madai yake au kukumbushia madai yake na kama imeshindikana kwenda ngazi ya juu zaidi ya shirikisho kudai haki zake. Sijui ni kwamba hana ufahamu wa sheria na kanuni zinazolinda haki zake ama anadai kirafiki.

Huyu haoni wachezaji wa kigeni wanavyoziweka klabu za Ligi Kuu na Championship kwenye hali ngumu hadi zinazuiwa kufanya usajili kutokana na kutolipa madai ya wachezaji ziliowaacha? Au anadhani madai ni lazima yapelekwe Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA)?

Wanaotelekezwa

Nahisi huyu ni mmoja kati ya wachezaji wengi wazawa wanaotelekezwa na klabu zao bila ya kulipwa haki zao kulingana na mikataba yao. Huenda ni kwa sababu ya kutojua, ama kudai kirafiki, ama mikataba yao haikuwa na vipengele vingi vinavyoweza kumlinda iwapo anatelekezwa na klabu bila ya sababu za kimpira.

Wakati fulani ufahamu wa sheria na kanuni zinazolinda haki na hadhi ya wachezaji ulianza kukua na barua za wachezaji kuzishtaki klabu zao kwa kutowalipa stahiki zao zilianza kujaa kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na wale waliosimama imara, walishinda kesi zao.

Kuna walioshinda kesi zao, lakini klabu zikapuuza kuwalipa hadi kama sekretarieti ilipochukua hatua za kuzitaarifu klabu zilizokuwa zinadaiwa kuwa iwapo hazitatekeleza uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kwa kipindi fulani, tutaanza kuzikata kwenye mapato yao.

SOMA ZAIDI: Simba Inahitaji Kutathmini Safari Yake ya Mabadiliko

Na tulifanya hivyo, si tu kwa maslahi ya wachezaji hao, bali mpira wa miguu nchini ili kuweka heshima kwenye klabu wakati wa kushughulikia haki na malipo ya wachezaji. 

Tulizikata klabu nne zaidi ya Shilingi milioni 60 na kuziwasilisha kwa wachezaji, hali iliyorejesha furaha yao. Lakini ile hali ya kuheshimu klabu walizozitumikia kwa muda mrefu ikapungua kutokana na vituko vya viongozi wa wakati huo.

Shirikisho kuaminiwa

Na hilo lilirejesha hali ya shirikisho kuaminiwa na wachezaji wa kigeni ambao pia baadaye waliwasilisha madai yao dhidi ya klabu walizochezea hapa Tanzania.

Ni nadra kwa wachezaji wa kigeni kuwasilisha madai ya haki zao kwenye vyombo vya haki katika nchi wanazochezea kwa kuwa huwa wanahisi kunaweza kufanyika upendeleo na wasipate haki zao ama kupunjwa. Na hata kanuni za Fifa ni kama zinawasukuma waende huko kudai haki zao.

Taarifa ya hivi karibuni kwamba klabu ya Yanga imetakiwa kuwalipa wachezaji wawili wa kigeni iliowaacha, Lazarous Kamboole na Mamadou Doumbia, zaidi ya Shilingi milioni 840 na wasipotimiza wanafungiwa kusajili, zilifaa kuwastua wachezaji wazawa kuhusu mikataba na namna ya kudai haki zao kwenye vyombo vya haki vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

SOMA ZAIDI: Olimpiki ya Paris Imeshatupita, Tujiandae ya 2028

Na si wawili hao tu. Wachezaji wengine walioenda FIFA wamesababisha klabu nyingine za Singida Fountain Gate, Tabora United, Biashara United na FGA Talents zipewe amri hivyo na zisipotekeleza, zitazuiwa kusajili.

Hawa wachezaji wetu wazawa ni lazima wajue kuwa kuna Kamati ya Sheria inayoshughulikia hadhi na haki zao ili mradi tu wajue wanasaini mikataba ambayo inawalinda dhidi ya vitendo vya hovyo vya kutelekeza wachezaji bila ya sababu za msingi.

Ni muhimu wachezaji wakawa makini wakati wa mazungumzo yanayolenga kuwataarifu kuwa wataachwa ili wajue stahiki zao wakati watakapoachwa. Hii ni kwa sababu mchezaji anaposaini kuichezea klabu fulani kwa miaka miwili au mitatu anakuwa anajua amepanga kufanya nini katika kipindi hicho.

Hivyo, ikitokea kwamba anaachwa, maana yake anazuiwa kutekeleza malengo aliyojiwekea kwa kipindi hicho na hivyo anastahili fidia. Zaidi ya hayo, kuna posho, bonasi na haki nyingine ambazo anastahili kulipwa kabla ya kupewa mkono wa kwa heri.

Sitaki kuamini kuwa mikataba ya wachezaji wazawa ni mizuri kiasi kwamba maslahi yote ya mchezaji hushughulikiwa bila ya matatizo anapomaliza mkataba wake au kuachwa. 

SOMA ZAIDI: Kwa Hili, Serikali Imeheshimu AFCON 2027

Nataka kuamini kuwa huenda lugha nzuri za viongozi, kutojua haki zao, kutozingatia hadhi zao wakati wa kusaini mikataba na mambo mengine ndiyo husababisha wachezaji wengi kudhani kuwa malipo ni fadhila ama utashi wa viongozi.

Na ndiyo maana yule kijana anawavizia viongozi wa klabu aliyochezea kwenye sehemu ya burudani ili eti adai haki zake. Hii haistahili kuendelea. Ni lazima wachezaji wetu wazawa wajenge ujasiri kama wenzao wa kigeni katika kusimamia haki zao ili wanaporudi mtaani maisha yasonge kulingana na matarajio yao na kuachana na tabia ya kuvizia viongozi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *