Hivi karibuni, Watanzania 15, akiwemo Mbunge wa Geita Vijiji (Chama cha Mapinduzi – CCM), Joseph Kasheku Musukuma wametunukiwa shahada ya udaktari wa heshima na kinachojulikana kama Academy of Universal Global Peace. Tuzo hii imezua mjadala mpana kwa sababu kadha wa kadha ambazo nitaeleza.
Kwanza, nimnukuu Musukuma mwenyewe: “Mimi nimepata PhD yangu ya Siasa na Uongozi. Na mimi ni Mbunge ambaye kwenye Bunge letu nimekuwa nikiwa-challenge sana Madaktari na Maprofesa. Sasa kwa vile nimekuwa na mimi Dokta ninaamini na mimi siku moja watakubali nitoe mhadhara ili waweze kusikiliza ninayoyasema kwa sababu ni Daktari mwenzao.
“Lakini hili pia ni fundisho kwa vyuo vyetu vya Tanzania. Tanzania tunavyo vyuo vingi sana. Leo tunasheherekea miaka 60 ya uhuru, tujiulize Maprofessa na Madaktari wa vyuo vikuu ni Watanzania wangapi wenye uwezo kama Musukuma – wa kujenga hoja, wa kusaidia watu, ambao mmeweza kuwatunuku tuzo kama hii? Jibu linakuja mna wivu na watu wanaofanya kazi vizuri. Naona hata waandishi wengine wananionea wivu.”
Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo, ambaye pia ni Mbunge wa Vwawa (CCM) Japhet Hasunga naye alitunukiwa shahada ya Udaktari wa Heshima lakini yake haijavuma kama ya Musukuma. Inawezakana kuna sababu nyingi kwa nini Musukuma amekuwa kwenye kitovu cha mjadala.
Kushambuliwa kwa wasomi
Kwa miaka ya hivi karibuni, Musukuma amekuwa akiwashambulia wasomi ndani na nje Bunge, kama alivyokiri mwenyewe kwenye nukuu hapo juu. Amekuwa akisisitiza kwamba elimu sio kigezo pekee au hata cha muhimu kwa mtu kufanikiwa. Na mafanikio kwake yeye, na kwa wenye mtazamo kama wake, ni mapesa na vyeo. Yaani kujipatia maarifa kumedunishwa kwa kiasi hiki!
Nikiri kwamba hii ni sehemu tu ya simulizi za kimazoea (popular discourse) ambazo badala ya kujikita kuelewa matatizo ya kielimu na kiuchumi tuliyonayo kama nchi, huwaambia na kuwaaminisha watu kwamba haijalishi mtu upo katika hali gani kimaisha, utatoboa tu kama akina Musukuma au fulani na fulani wa fulani.
Simulizi hizi pendwa ambazo huleta matumaini hewa huhubiriwa na wanasiasa wetu, wahubiri, wahamasishaji, matajiri na watu mbalimbali mashuhuri katika jamii. Hawa wote ni mitume wa mfumo wa uliberali-mamboleo ambao hubidhaisha na hivyo kudunisha elimu na maarifa. Chakushangaza, makundi haya haya ndiyo walengwa wa shahada zinazofanania shahada za kitaaluma.
Shahada ya heshima
Tofauti na shahada za kitaaluma, shahada ya heshima sio ya kusomea darasani wala huifanyii utafiti. Shahada hii hutolewa kwa mtu yoyote ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika jamii (kitaifa au kimataifa) au amekiheshimisha chuo husika kwa namna fulani. Kwa mfano, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alitunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya kwa kutambua mchango wake katika uimarishaji wa elimu na utatuzi wa migogoro. Chuo hicho hicho kilimtunuku shahada hiyo mwanariadha mashuhuri wa nchini Kenya Eliud Kipchoge kwa kutambua mchango wake kwenye michezo.
Vyuo vikuu vikongwe duniani kama vile Oxford na Cambridge vya nchini Uingereza vilianza kutoa shahada hii kuanzia karne ya 15. Hata hivyo, kila chuo kina utaratibu wake na vigezo vya kutoa shahada za heshima. Baadhi ya vyuo vina utaratibu wa wazi wa jinsi ya kufanya maombi au kupendekeza majina ya watu na hata kuweka majina hayo kwenye gazeti ili kuweza kupata maoni ya umma na hatimaye hufanya uchaguzi.
Kwa vyuo vingine, zoezi hili hufanywa kwa usiri na umma utashtukizwa tu siku ya tukio. Vile vile, vyuo hujiwekea idadi maalum ya shahada za heshima zitakazoitoa kwa muda fulani, kama vile mara mbili au moja kwa mwaka, au hata mara moja tu kila baada ya miaka mitatu kama ilivyo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati chuo hiki hutoa shahada za heshima tatu tu kila baada ya miaka mitatu, Chuo cha Oxford hutoa kati ya nane na kumi kila mwaka.
Kwa kawaida, panakuwa na kamati maalum ya shahada za heshima ambayo kwa kushirikiana na vyombo vikuu vya maamuzi kama Baraza la Chuo au Seneti hupitia mapendekezo ya nani apewe tuzo ipi kwa sababu zipi. Kwa mfano, baadhi ya vyuo havitoi shahada hizi kwa wanasiasa waliopo madarakani wakati vingine kama vile Massachusetts Institute of Technology (MIT), Stanford na Virginia havijawahi kabisa kutunuku shahada ya udaktari wa heshima kwa mtu yoyote yule. Mwanzilishi wa MIT William Barton Rodgers aliona utoaji wa shahada hii kama ni hisani ambayo huchochea mbwembwe tu na ni kutowatendea haki wale wanaosotea shahada za kitaaluma.
Pia, ni dhahiri kwamba mchakato wa utoaji wa shahada hizi unaweza kufanywa kisiasa, hivyo, wakati mwingine ni vigumu kutambua kama utoaji wa shahada kwa watu fulani ni uamuzi wa chuo au msukumo wa wenye mamlaka. Tumeona pia vyuo vya hapa nyumbani vikigawa shahada hizo kwa viongozi wakubwa kama vile Mkuu wa Nchi. Kikwete na Hayati Rais John Magufuli walitunukiwa wakiwa madarakani na pengine tutarajia ya Mama Samia Suluhu Hassan muda sio mrefu ujao.
Umuhimu wa kujiweka mbali na wanasiasa
Nakubali kuwa ipo haja ya kuwatambua na kuwatunuku viongozi wanaofanya vizuri tena wakiwa bado wapo hai. Lakini pia naona ni uamuzi wa busara chuo kujiweka mbali na wanasiasa waliopo madarakani ili kulinda uhuru na weledi wake.
Tunaweza kuhoji baadhi ya shahada za heshima zilizotolewa na vyuo vyetu lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Nikisikia wanasiasa kama Musukuma wanalalamika kuwa hawajatambuliwa na vyuo vyetu, kwa namna fulani ni ishara nzuri kwamba vyuo vyetu vina utaratibu na vigezo vinavyowaongoza, hivyo, hawagawi tu hizi shahada kama karanga au tisheti za kampeni.
Wanasiasa wana tamaa kubwa sana ya kupata umaarufu na hakuna asiyejiona kwamba kafanya makubwa kwa wananchi wake. Kila mwanasiasa anajiona kuwa anastahili heshima kubwa. Jacob Zuma, Rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye yupo gerezani hivi sasa, alitunukiwa udaktari wa heshima pamoja na kwamba alikuwa mshirika mkubwa wa familia ya Gupta iliyogeuza Afrika Kusini shamba la bibi.
Wanasiasa wenye kiu na njaa ya umaarufu na ambao wengi wao hawajabahatika au walishindwa kuendelea na elimu kwa mkondo rasmi wamekuwa wateja wakubwa wa soko la shahada za udaktari wa heshima. Wanasiasa hawa (na wengine wenye vyeo vya kidini) wanaona hii kama fursa adhimu au mlango wa kuingilia kwenye klabu ya wasomi: “Hatimaye sasa watanisikiliza, nami ni dokta ujue?”
PhD ya mchango au mchongo?
Minong’ono na manung’uniko kuhusu shahada, ziwe za kitaaluma au za heshima (kama vile za kitaaluma sio za heshima! Ila kuna kaukweli ama?), ni mingi miongoni mwa wanajamii. Na hili sio suala la hapa kwetu tu. Mfumuko wa shahada za heshima umeendelea kuzua gumzo kwa majirani zetu Kenya, na mataifa mengine ya Afrika ikiwemo Zambia, na Nigeria.
Kwa miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mfumuko wa shahada za uzamivu (PhD), ziwe za kitaaluma au zile zinazoitwa za heshima. Serikali pia ilikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la vyeti feki nchini, hali ambayo iliambatana na utiriri wa vyuo vingi na taasisi za elimu ya juu ambazo vinakuwa na uhaba mkubwa wa rasilimali, iwe majengo au wakufunzi.
Kabla ya Serikali awamu ya tano kuendesha zoezi la kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki katika utumishi wa umma, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilishabaini uwepo wa PhD feki katika baadhi ya vyuo vyetu. Ilisemekana kwamba baadhi ya wahadhiri walipata shahada zao kutoka katika vyuo ambavyo ubora, uhalali na uadilifu wake ni wa kutiliwa mashaka.
Lakini vipi kuhusu shahada za heshima? Hizi si ni za kutunukiwa tu? Je, ni sawa kuzifuatilia au kuzihoji? Bila shaka. Sio kwa sababu tunawaonea wahusika wivu kama anavyodai Musukuma. Bali kama vile ambavyo jamii inapaswa kujali uhalali wa taaluma za madaktari, wanasheria, wahasibu na wataalam mbalimbali, vivyo hivyo inapaswa kujali uhalali na uheshima wa shahada za heshima wanazotunukiwa viongozi wetu wa kisiasa na kijamii.
Tume za vyuo vikuu Afrika Mashariki vilishtushwa pia na ongezeko kubwa la shahada za udaktari wa heshima zinazotolewa kwa wanasiasa, hasa na vyuo vya nje ambavyo uhalali wao ni wa kutiliwa mashaka. Kwa mfano, mwaka 2012, TCU ilitoa tahadhari kwa umma baada ya kupata taarifa kupitia matangazo yanayotolewa na chuo kinachojiita ‘Japan Bible Institute Graduate School of Theology’ kikijitangaza kwamba kinatoa shahada mbalimbali za uzamivu (PhD) kwenye nyanja za dini na jamii.
Chuo hiki kilidai kwamba kinawakilisha tawi la taasisi iliyopo nchini Marekani na kwamba makao yake makuu kwa bara la Afrika yapo Dar es Salaam, pamoja na ukweli kwamba eneo halisi ofisi zao zilipo haikujulikana.
Sifa za zinazoshabihiana
Vyuo hivi vina sifa za zinazoshabihiana. Hudai kwamba wapo nchi mbalimbali duniani au angalau mabara matatu tofauti lakini haijulikani ofisi zao hasa ziko wapi. Vyuo hivi vinajitanabaisha kuwa vyenyewe vimegundua kwamba kuna Waafrika wengi sana wamefanya mambo makubwa lakini hawajatambuliwa na wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata heshima hiyo! Hata hivyo, tofauti na utaratibu wa kawaida wa utoaji wa shahada za heshima, vyuo hivi hudai malipo toka kwa watunukiwa. Hii inashangaza na ni hatari.
Ili kulinda heshima na uadilifu wa Vyuo Vikuu nchini na hadhi ya shahada zinazotolewa kwa Watanzania ilionekana pana haja ya kuweka sheria na taratibu zitakazodhibiti viwango vya wa ubora wa shahada mbalimbali zinazotolewa na Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Ndipo ikapitishwa Sheria ya Vyuo Vikuu (Cap. 346) ya Mwaka 2013. Ibara ya 47(1) (c) ya sheria hiyo inatamka kuwa, “Si ruhusa kwa mtu au taasisi yoyote, iwe ndani au nje ya nchi, kutangaza kutoa tuzo yoyote ya ngazi ya Chuo Kikuu, ikijumuisha shahada za heshima, kwa mtu yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila idhini ya Tume [ya Vyuo Vikuu, Tanzania].” Tafsiri ni yangu.
Kufahamu kama shahada ya Musukuma ni halali au ni mchongo, TCU watatuambia. Nasema hivi kwa sababu ndivyo sheria inavyoelekeza. Kuna mijadala mtandaoni kuhusu uhalali wa chuo hicho cha Academy of Universal Global Peace. Wapo Watanzania wanaodai kwamba wamefuatwa na chuo hicho kikitaka kuwatunuku udaktari wa heshima lakini kwa sharti kwamba walipe kiasi fulani cha fedha.
Vyuo vya kitapeli
Hili si jambo la kushangaza kwani huko nyuma TCU ilitahadharisha kuwepo kwa vyuo vya kitapeli vinavyouza shahada kwa bei kama Dola za Kimarekani 2,000, kama Shilingi milioni nne na zaidi. Baadhi ya vyuo hivi hutoa shahada za chap chap. Kwa mfano, unaweza kupata shaha ya uzamivu (PhD) ndani ya mwaka mmoja. Aliyekuwa Mwenyekiti wa TCU wakati huo alikiri kupokea baruapepe kutoka kwa baadhi vyuo hivyo vikimtaka anunue bidhaa hiyo.
Binafsi nimejaribu kukifuatilia chuo hiki cha Academy of Universal Global Peace na baadhi ya mambo yananipa wasiwasi. Mosi, haijulikani makao yake makuu yapo wapi. Je, ni Marekani au India?
Sehemu fulani wanaonyesha kuwa makao yao makuu yapo New Jersey nchini Marekani lakini kwingine wanasema kiongozi wao mkuu huwa anahamahama na kwa sasa yupo India. Kwa hiyo, makao makuu ya chuo yapo Chennai. Vile vile, chuo kinaonekana kuwa na tovuti zaidi ya moja, hivyo kufanya upatikanaji wa taarifa za uhakika kuwa mgumu.
Kitu kingine kinachovutia kufuatilia chuo hiki ni madai yake ya kujihusisha au kujitanabaisha na vyuo vingine na taasisi za Umoja wa Mataifa ambayo yenyewe yanakanusha mahusiano hayo. Kingine ni tuzo alizopewa mwanzilishi wa chuo hiki: kwenye tovuti ya chuo inaonekana Madhu Krishan ametunukiwa medali zaidi ya saba ndani ya miaka miwili tu ambapo kati ya hizo tatu ni za kitaifa nne ni za kimataifa.
Pengine hili sio tatizo lakini hawaonyeshi hizi tuzo zimetolewa na nani jambo ambalo linaongeza wasiwasi zaidi kwa wadadisi wa mambo. La mwisho, lakini sio kwa umuhimu, ni kwamba chuo kinatangaza kuwa kinatoa shahada za heshima mtandaoni na kwamba mtu anayetaka atume tu kitambulisho chake na maelezo kuhusu mafanikio yake katika eneo husika. Wale waliosema kwamba walikuwa wanafuatiliwa kwa miaka mitatu wanaweza kutuambia labda kuna utaratibu mwingine wa tofauti.
Utambuzi wa shahada za heshima
Kanuni na Miongozo ya Kutathimini Tuzo Zinazotolewa na Taasisi za Kigeni, Toleo la mwaka 2019 zimejikita kwenye shahada za kitaaluma tu! Hata hivyo, TCU inasisitiza kuwa shahada za heshima zitatambuliwa tu iwapo zimetolewa na vyuo vilivyosajiliwa kisheria na kutambuliwa na taasisi za udhibiti ubora katika nchi husika.
Kwa kuwa TCU ina ushirikiano na Tume ya Vyuo Vikuu ya India (University Grants Commission) inaweza kutusaidia kujua zaidi kuhusu taasisi hii. Lakini je, hii peke yake inatosha? Nadhani kwa mazingira ya sasa na tunakoelekea tunahitaji kwenda zaidi ya hapo. Wahenga walisema kinga ni bora kuliko tiba. TCU isaidie umma kutambua hivi vyuo feki na sio kusubiri tu kuhakiki vyeti.
Nilipotembelea tovuti ya TCU katika jitihada zangu za kutaka kuhakiki uadilifu wa chuo cha Academy of Universal Glopal Peace, nilishangaa kuona some of the recognized foreign universities (baadhi ya vyuo vya kigeni vinavyotambuliwa na TCU) ambapo ni vyuo 14 tu vilivyopo katika mataifa 12 tofauti.
Kwangu mimi hii haikuwa na msaada wowote. Kwa nini hivyo vyuo 14 tu? Nadhani ingekuwa jambo la maana sana kuweka orodha ya vyuo visivyoaminika na orodha hii iwe inasasishwa (updated) mara kwa mara kwa kufuatilia yanayojiri ndani na nje ya nchi.
Kwa kuwa vyuo halali ni vingi, TCU ingewekwa tu kiungo cha baadhi ya vyuo ambavyo wanafunzi wengi wa Kitanzania huenda mara kwa mara. Muhimu pia kuweka kiungo cha taasisi za udhibiti wa ubora wa elimu katika nchi mbalimbali.
Nimalizie kwa kumhakikishia Musukuma kuwa sisi hatuna wivu na tuzo yake lakini tuna wivu mkubwa sana na elimu yetu na tusingependa watu wakose imani nayo. Na kamwe tusisahau kwamba binadamu wote wanastahili heshima sawa. Tukijua na kuliishi hili kutafuta haya majina makubwa na vyeo haitakuwa vita ya kufa na kupona!
Leiyo Singo ni Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Bayreuth, kilichopo nchini Ujerumani. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni Leiyo.Singo@uni-bayreuth.de. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na silazima yaakizi mtazamo wa The Chanzo Intiative.
2 responses
Leiyo ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu hizi PhD zinazoleta mtafaruku ktk jamii. Ukweli ni kwamba tunajipoteza wenyewe kama tukifanya vyuo vyetu kuwa majukwaa ya wanasiasa kujipigia promo. Tumekuwa na tabia chafu ya kuwasifia wanasiasa hadi inakuwa kero. Na kutokana na jinsi tunavyowamwagia sifa, nao wanafika mahala wanajisahau wanakuwa kama miungu watu.
Maoni yangu ni kwamba degree za namna hii zinahitajika sana huitaji kupasua sana kichwa ilhali kuna uwezo wa kupata degree za namna hii za heshima na mtu akitunukiwa kusiwe na discrimination ktk kumkubali aliyetunukiwa kwa kuhoji uhalali wake maana hata phd za shule nazo ukizifatilia ni majanga tu,tunahitaji PhD nyingi zaidi kuchagiza maendeleo sio kungangania kuumiza vichwa tu mbn wazungu wamerob African economy na hawajaripishwa fidia hadi leo??