Mtwara. Wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa nchini Tanzania wamekuwa na mawazo tofauti kuhusiana na kile kinachoonekana kama ni kuongezeka kwa hamasa miongoni mwa vijana wa Kitanzania kuonesha nia ya kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa umma nchini.
Maoni ya wachambuzi hao yanakuja huku kukiwa na kundi kubwa la vijana waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) ili washiriki kinyang’anyiro cha kumrithi Job Ndugai kama Spika wa Bunge aliyejiuzulu mnamo Januari 6, 2022, baada ya kutofautiana na Rais Samia Suluhu Hassan juu ya mikopo.
Mpaka kufikia Januari 15, 2022, jumla ya makada 70 wa CCM waliripotiwa kurejesha fomu za kugombea kiti cha uspika, miongoni mwao wakiwa ni watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wachekeshaji na hata wanafunzi wa vyuo vikuu.
Wengi wa waliojitokeza kumrithi Ndugai ni kutoka CCM, – ukiacha mtia nia mmoja kutoka chama cha ADC – huku upinzani kwa kiasi kikubwa ukionekana kuwa na hamasa ndogo ya kuchangamkia kinyang’anyiro hicho.
Hali hii inaweza kuwa imetokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya upinzani nchini Tanzania wanaliona Bunge hilo la 12 kukosa uhalali, na hivyo kutojishirikisha na kitu chochote kinachohusiana nalo.
Hii si mara ya kwanza kwa Watanzania wengi kuonekana kuwa na hamasa kubwa ya kushiriki kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa kitaifa.
Hali kama hii ilionekana pia mwaka 2020 wakati wa uchaguzi mkuu ambapo Watanzania wa kila rika walijitokeza kuomba ridhaa ya vyama vyao – vya CCM na upinzani – ili kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ile ya udiwani, ubunge na hata urais.
Harakati za kusaka uteuzi
The Chanzo ilimuuliza Hebron Mwakagenda, mchambuzi wa masuala ya kiutawala na mfuatiliaji mzuri wa siasa za Tanzania, anadhani ni nini kinaweza kuwa kinahusika na ongezeko hili la hamasa miongoni mwa Watanzania kutaka kushika nafasi za uongozi wa kitaifa.
“[Rais John] Magufuli alitumia sana wale waliogombea kwenye mchakato wa CCM kuwapa nafasi mbali mbali kama vile ukurugenzi [wa halmashauri] na ukuu wa wilaya,” alijibu Mwakagenda.
Magufuli alikuwa Rais wa awamu ya tano aliyefarikai Machi 17, 2021, kutokana na changamoto za moyo. “Kwa hiyo, watu wamegundua kwamba kujulikana kijimbo au kimkoa hukusaidia sana ujulikane kitaifa sasa,” aliongeza Mwakagenda.
Ni maoni ya mchambuzi huyu kwamba wengi kati ya wale wanaojitokeza kuwania nafasi za uongozi wa umma hawana lengo la kushinda kwenye michakato hiyo, isipokuwa hutumia michakato hiyo kujitangaza kwa mamlaka ya uteuzi kwamba na wao wapo na wapo tayari kwa kazi yoyote watakayopangiwa.
Mtazamo wa Mwakagenda unaweza kuwa ni mtazamo wa watu wengi wanaofuatilia kinyang’anyiro hicho cha uspika, hususan wale wanaotoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii, lakini hata hivyo siyo mtazamo wa watu wote.
Mabadiliko ya mitazamo ya kijamii
Wakili na mwanasiasa kijana wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo Bonifasia Mapunda anadhani kwamba kujitokeza kwa vijana wengi kwenye kugombea nafasi za uongozi kunadhihirisha kumomonyoka kwa mila na desturi kandamizi ambazo zilikuwa zikiwazuia vijana hao kushiriki kwenye michakato hiyo huko nyuma.
“Jamii zetu kwa miaka mingi zilikuwa hazimuamini kijana anaposema kama angependa kugombea nafasi fulani ya uongozi wa umma,” anasema Mapunda wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo kwa njia ya simu. “Tunachokishuhudia kwa sasa ni kupanuka kwa uelewa ndani ya jamii zetu, imani kwa vijana imeongezeka na hiyo imewafanya vijana wajiamini zaidi katika kugombea nafasi hizi.”
Lakini licha ya mabadiliko haya chanya kwenye mitazamo ya kijamii kuhusu vijana na uongozi, Mapunda anaamini kwamba uwezekano wa vijana kuibuka washindi kwenye michakato hii ni mdogo sana, akigusia suala la rasilimali na uzoefu kama baadhi ya sababu zinazopelekea hali hiyo.
“Hata hivi kuchukua fomu inatakiwa ulipe,” anasema Mapunda. “Si vijana wengi wanaweza kumudu hizo gharama. Lakini changamoto nyengine ni hiyo ya ukosefu wa uzoefu. Kwa mfano, watu wanaogombea kwenye nafasi ya uspika watawatazama pia kwa nafasi ile kwa kiti kile kwa kijana bado. Kwa hiyo, bado pana hizo changamoto ambazo bado zinahitaji utatuzi.”
Ushauri wa watia nia wa baadaye
Tumemuuliza mtaalamu wa masuala ya vijana na utawala wa umma Selemani Makwita anadhani ni tatizo gani la msingi linawakabili vijana wa Kitanzania ambalo linaweza kuathiri nia yao ya kuwa viongozi wa umma na kama kuna ushauri wowote anaweza kutoa na haya ndiyo yalikuwa majibu yake.
“Vijana wengi wanasubiri wapewe nafasi na sio wachukue,” anaeleza Makwita. “[Wanasema] tumuunge mkono mama fulani au baba fulani aingie halafu atufikirie na sisi. Wakati wao ndio wanaofanya hizo kazi za kuwaingiza watu kwenye hizo nafasi. Kwa hiyo, ni muhimu vijana wabadilishe mitazamo yao na kujiona kwamba wanastahili kukaa kwenye zile nafasi. Siyo wawe wapambe wa wanaotakiwa kukaa kwenye zile nafasi halafu baadaye ndio wakumbukwe.”
Kwa upande wa Mapunda, yeye anadhani kwamba ni muhimu vijana kutambua kwamba uongozi wa umma unahijati maandalizi na ni mchakato ambao kila anayetaka kuwatumikia Watanzania inabidi aupitie.
“Ili uweze kufikia malengo ya kupata nafasi unayotaka ni lazima ujifunze na uanze kujiandaa mapema,” anashauri. “Huwezi tu kutoka unakotoka uje uwe kiongozi wa umma. Siasa siyo kitu ambacho unaweza kukurupuka tu.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.
One Response
Story nzuri imeandikwa kwa weledi mkubwa niwapongeze kwa hilo The Chanzo.
Kuhusu kuongezeka kwa hamasa kwa vijana wa kitanzania maoni yangu nafikiri ni kupanuka kwa demokrasia na elimu pia inachangia vijana wengi kuona kuwa hata upande wa siasa nako wanaweza kufanya kazi kama kawaida. Huo ni mfano tosha ukiangalia bungeni kuna idadi kubwa ya vijana, hata kwenye ngazi nyingine za kiutawala.