Mtwara. Wakulima wa chumvi mkoani hapa na kutoka mikoa mingine ya jirani wako mbioni kupata suluhu ya tatizo la masilahi duni yatokanayo na kilimo cha bidhaa hiyo muhimu kufuatia hatua ya Jeshi la Magereza la Tanzania kujenga kiwanda cha kuchakata chumvi ambacho kimepangwa kuzinduliwa katikati ya mwezi ujao wa Februari, 2022.
Kiwanda hicho ambacho ujenzi wake unakisiwa kugharimu jumla ya Shilingi milioni 84.5 kinakadiriwa kuwa na uwezo wa kusaga jumla ya tani tatu za chumvi kwa siku na kutumia dakika 15 kwenye mchakato mzima wa kusaga na kufungasha kiasi cha kilo 30.
Kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hichi kunategemea kuwa na mchango wa mabadiliko ya msingi ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mikoa ya kusini, hususan miongoni mwa wakulima wa chumvi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilalamikia maslahi duni wanayoyapata kutoka kwenye kilimo hicho.
Kwa mujibu wa maelezo ya wakulima wa chumvi waliongea na The Chanzo kwa nyakati tofauti, masilahi hayo duni yamekuwa yakitokana na ukweli kwamba kuna uhaba wa wanunuzi wa kubwa wa bidhaa hiyo, hali inayofanya kutokuwepo kwa ushindani na wanunuzi waliopo kulazimika kununua kwa bei wanayoitaka wao.
“Kama tungekuwa na viwanda vya kuchakata chumvi, nafikiri hapo ingeturahisishia zaidi sisi kupata masoko vizuri,” mmoja kati ya wakulima wa chumvi wanaopatikana katika eneo la Ufukoni Stand mkoani hapa Salum Ally aliieleza The Chanzo ilipotembelea eneo hilo. “Lakini viwanda vya kuchakata hamna ndiyo tunategemea Neel peke yake kwa vile Neel anaweza akanunua vile anavyotaka yeye.”
Neel Salt ni moja kati ya kampuni za chumvi zinazofanya shughuli zake nchini Tanzania.
“Sehemu pakiwepo kiwanda maana kazi inakuwa nyingi sana,” anasema mkulima mwengine wa chumvi Babu Said. “Hata chumvi yenyewe inauzika kwa wakati na inakuwa na wateja sana. Kwa sababu mtu anajua nikishanunua basi kiwanda kipo naipeleka pale haraka.”
Kiwanda hicho cha Magereza baada ya kukamilika na kuanza kufanya kazi kitakuwa ni kiwanda cha kwanza cha kuchakata chumvi kujengwa katika ukanda wa mikoa ya kusini, yaani Lindi na Mtwara, na hivyo kutegemewa kumaliza vilio vingi na vya muda mrefu vya wakulima hawa.
Mkuu wa Magereza ya Kiwanda Chumvi Johnston Kabyemela ameiambia The Chanzo wakati wa mahojiano maalum kwamba ni mpango wa kiwanda hicho kununua chumvi kutoka kwa wakaulima wadogo wadogo, kitu ambacho anaamini kitatoa fursa kwa wakulima wengi wa chumvi kutoka Mtwara na mikoa ya jirani.
“Badala ya kuhangaika na wanunuzi ambao siyo wa uhakika, sasa wakulima watakuwa wanaleta chumvi yao hapa,” amesema Kabyemela. “Sisi tunanunua. Sisi tutalipa fedha taslimu. Sisi tunasaga halafu tunauza chumvi ambayo tayari imeshasagwa.”
Awali, Kabyemela amesema kwamba gereza hilo lilikuwa likilima na kuuza chumvi ghafi, lakini baada ya Suleiman Mzee kuteuliwa kama Kamishna Mpya wa Magareza alishauri kwamba Magereza, kupitia Shirika la Magereza (SHIMA), lijenge kiwanda hicho ili wauze chumvi iliyoongezewa thamani.
Akizungumza kuhusu upatikanaji wa soko, Kabyemela amesema: “Soko siyo kitu kinachotutia wasiwasi. Tukisema tusambaze kwenye magereza yetu tu nchi nzima hilo ni soko la kutosha.”
Zamra Dongwara ni afisa kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) mkoani Mtwara ambaye amebainisha kwamba tatizo kubwa ambalo limekuwa likiwakumba wazalishaji wadogo wa chumvi nchini ni ubora wa vifungashio, akiwaasa wazalishaji kulifanyia kazi jambo hilo.
“Ufungashaji mbovu unapelekea chumvi kuwa na ubora hafifu,” anasema Dongwara wakati akiongea na The Chanzo. “Kwa hiyo, tunategemea kwamba mara baada ya kiwanda [hiki cha magereza] kukamilika hawa [wazalishaji] wadogo wadogo wakitaka kutengeneza chumvi za kutumia majumbani waende wakakachakate pale kiwandani na kuwa na vifungashio vizuri.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.