The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara

Kutokana na wakulima wengi kushindwa kumudu manunuzi ya pembejeo za kuweza kukidhi mahitaji yao, wengi wao walilazimika kupuliza mashamba yao kwa awamu chache kinyume na wanavyoshauriwa na wataalam wa kilimo.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Wakati wakulima wa korosho mkoani hapa wakijiandaa na msimu wa zao hilo la biashara kwa mwaka 2022/2023, vilio juu ya upatikanaji wa kusuasua wa pembejeo, uwepo wa tozo kubwa na korosho kuuzwa bei ya chini vimetawala miongoni mwa wakulima ambao wameiangukia Serikali kuingilia kati kurekebisha hali hiyo.

The Chanzo ilizungumza na baadhi ya wakulima wa korosho kutoka chama cha msingi cha Mayanga Amcos kilichopo katika kijiji cha Msijute, manispaa ya Mtwara Mikindani ambao walibainisha kwamba msimu wa mwaka 2021/2022 walishindwa kupata manufaa makubwa kutoka kwenye kilimo hicho, wakihusisha changamoto hizo kama sababu za msingi.

Kutokana na wakulima wengi kushindwa kumudu manunuzi ya pembejeo za kuweza kukidhi mahitaji yao, wengi wao walilazimika kupuliza mashamba yao kwa awamu chache kinyume na wanavyoshauriwa na wataalam wa kilimo.

“Serikali ilituambia kwamba dawa  [pembejeo] tungepata bure lakini baadae ikawa pembejeo hazipatikani kwa wakati,” anasema Mohamedi Hamisi Namoto, mmoja kati ya wakulima waliongea na The Chanzo.

Mnamo Mei 15, 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza mpango wa Serikali wa kugawa pembejeo za korosho bure kuanzia msimu wa kilimo wa 2017/2018, ambapo wakulima wangepata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.

Wakati wakulima wengi wameipongeza hatua hii, kitendo cha pembejeo hizo muhimu kuwafikia wakulima kwa kuchelewa kimelalamikiwa na wakulima wengi. Namoto anadhihirisha hili kwa kusema: “Wewe umeshategemea kwamba mwaka huu dawa zitapatikana bure, lakini kuchelewa kwake kunakulazimu kununua, unaingia gharama ambayo hukuipangilia. Kwa kweli pale tayari unakuwa umeshaathirika.”

The Chanzo ilimuuliza Namoto ambaye anamiliki shamba lenye ukubwa wa hekari kumi za mikorosho kama angeweza kubainisha ni kwa kiwango gani haswa bei za pembejeo hizo zimeongezeka ambapo alibainisha kwamba bei ya pembejeo nyingi zilipanda mara mbili kulinganisha na msimu uliopita wa 2020/2021.

“Kwa mfano, Mupavil bei ya chini ilikuwa inauzwa Sh8,000 lakini baadae ilipanda mpaka kufikia Sh17,000,” anasema Namoto. Mupavil ni dawa inayotumika kutunza mikorosho inayozalishwa na kampuni ya Mukpar Tanzania Ltd.

Mbali na changamoto inayohusiana na bei ya pembejeo, wakulima wa korosho mkoani Mtwara pia wanalalamikia tozo kubwa wanazotozwa ambapo katika kila kilo moja wanayouza sokoni hukatwa Sh260, inayodaiwa kuwa ni kwa lengo la kuchangia mfuko wa elimu, chama cha msingi, hamashauri, na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Naliendele.

“Leo hii ukitoa bei tunayouzia korosho ambayo hairidhishi, tozo imefikia Sh260, lakini hawa watu wanaochukua pesa hatuoni juhudi wanazofanya kwenye kuendeleza zao la korosho,” Ally Hassan Kumbo, mkulima wa korosho na mwanachama wa Mayanga Amcos anaiambia The Chanzo. “Mimi narudia kwenye tozo tozo, wapunguze tozo.”

Kuna suala la bei ya korosho kushuka pia ambapo wakulima wameiambia The Chanzo kwamba kwa msimu wa mwaka 2021/2022 waliweza kuuza korosho kwa bei ya chini ya Sh1,200 kwa kilo kulinganisha na miaka miwili iliyopita ambapo walikuwa wanauza Sh1,900 kwa kilo.

The Chanzo ilimtafuta Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kumuuliza kama anafahamu changamoto hizi za wakulima na kama Serikali ina mpango wowote wa kuzitatua, hususan kwenye eneo la ucheleweshaji wa pembejeo. Hata hivyo, juhudi za kupata kauli yake hazikuweza kuzaa matunda.

Lakini Hamis Halid Hausi, ambaye ni meneja msaidizi wa chama cha msingi cha Mayanga Amcos, anakiri kuwepo kwa changamoto hizi.

Hausi anabainisha kwamba tayari maandalizi ya msimu ujao kwa ajili ya kuwapatia pembejeo wakulima yameanza ambapo wakulima wameanza kuandikisha majina kwa ajili ya kupata dawa ambazo Serikali itagharamia nusu ya bei ya kununua dawa hizo na nusu nyingine atatakiwa kuchangia mkulima mwenyewe.

Hausi anatoa wito kwa Serikali na mamlaka zingine za nchi zilizopewa dhamana ya kusimamia zao la korosho nchini kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinatatuliwa kwani vinginevyo uzalishaji wa korosho nchini utashuka kama hali itaendelea kama ilivyo.

“Msimu wa 2021/2022, huu tuliokuwanao, tumekusanya takribani tani 1,110 na kilo 989,” Hausi anaieleza The Chanzo. “Hii ni pungufu ukilinganisha na msimu uliopita ambao tulikusanya zaidi ya tani 1,800. Nilikuwa naomba Serikali waweke uwekezaji mkubwa sana kwenye zao la korosho.”

Omari Mikoma ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts