Mtwara. Kitendo cha vyombo vya utatuzi wa migogoro kuchukua muda mwingi kutoa maamuzi, wananchi kukosa hofu ya Mungu na ukosefu wa elimu inayohusu masuala ya haki za binadamu ni baadhi ya sababu viongozi wa dini nchini wanazozihusisha na wimbi la mauaji holela ambalo limekuwa likiitesa Tanzania kwa siku za hivi karibuni.
Viongozi hao wa dini walioorodhesha sababu hizo wakati wa kikao cha mtandaoni kilichoitishwa na Umoja wa Wapigania Haki za Binadamu Wanawake Tanzania (CWHRDs) mnamo Februari 11, 2022, ikiwa ni kama juhudi za wadau kuendeleza mjadala kuhusiana na janga hilo linaloendelea kuumiza vichwa vya wadau mbalimbali.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa The Chanzo, kati ya Septemba 2021 na Januari 2022, jumla ya matukio 37 ya mauaji yaliripotiwa kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara. Matukio haya ni yale tu yaliyothibitishwa na Jeshi la Polisi na orodha hii haijumuishi matukio ambayo hayakuripotiwa.
Kwa mujibu wa tathmini hii, jumla ya watu 52 waliripotiwa kuuwawa kwenye matukio hayo, ambapo wanawake walikua 26 na wanaume walikua 26. Kati yao, watoto walikua kumi na moja. Uchambuzi wa The Chanzo pia umebaini kwamba mtu mwenye umri mdogo kabisa katika matukio haya alikua ni mtoto wa miaka mitatu, huku mtu mwenye umri mkubwa kabisa alikua na umri wa miaka 75.
“Kwenye mamlaka za maamuzi, kuna maamuzi yanayochelewa mpaka kumsababishia mtu kutoa maamuzi mabovu,” alieleza Sheikh Twaibu Swed kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu Tanzania. “Hili ndio naliona tatizo kubwa kuliko sababu zengine.”
Sheikh Swed aliongeza kwa kusema kwamba kumekuwa na tabia kwa vyombo vinavyohusika na utatuzi wa migogoro kwenye jamii kuchua muda mwingi kuliko inavyotegemewa bila kufikia tamati, hali isiyowaacha walalamikaji na uchaguzi wowote mbali na kujichukulia hatua mikononi mwao.
“Unamcheleweshea mtu mirathi yake, hana chakula na mirathi imezuiliwa,” aliongeza Sheikh Swed. “Unavyoendesha kesi kwa miaka mitano sita saba na anajua kuna mali yake pale angeweza kuendeleza maisha yake matokeo yake anakuja na maamzu ambayo yasiyostahiki na wala hayakubaliki kisheria.”
Sheikh Swed amezitaka mamlaka hizo kujitafakari na kuonya kwamba kama hakutakuwa na mabadiliko ya msingi katika eneo hilo basi juhudi za muda mrefu za kukomesha janga hili ni rahisi sana kufeli kuliko kufanikiwa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima pia alikuwepo katika kikao hicho ambapo alilamikia hali ya kutokuwepo kwa hofu ya Mungu miongoni mwa wananchi kama moja ya sababu zinazopelekea watu kuwa tayari kufanya mauaji ya kiholela.
Dk Kitima pia aligusia suala la ukosefu wa elimu inayohusiana na umuhimu wa masuala ya haki za binadamu kwenye mitaala ya elimu ya ngazi mbalimbali, hali ambayo amesema inahitaji kubadilika kama kweli Tanzania imekusudia kuepusha hali hii ya mauji holela kujirudia huko mbeleni.
“Ukosefu wa elimu ya haki za binadamu ndiyo chanzo kikubwa cha kuvunjwa kwa haki msingi za akina mama na kutokea kwa matokea mengi ya mauaji,” ni maoni ya Dk Kitima. “Kama Watanzania, elimu hii ya haki za binadamu tunaipandikizaje kwa watoto wetu? Mitaala yetu kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu ina kiwango gani cha haki za binadamu zikiwa bayana?”
Omari Mikoma ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.