The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sakata la Wanyamapori Hai na Ugeugeu wa Sera za Kibiashara Tanzania

Serikali ni lazima ijue kuwa Tanzania haitaweza kupaa kiuchumi kama sera na taratibu za kibiashara zitakuwa zinabadilika kila siku.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Juni 4, 2022, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilitoa taarifa kwa umma ikitangaza kuruhusu usafirishaji wa wanyamapori hai waliosalia wakati zoezi la kusafirisha wanyama hao nje ya nchi lilipositishwa ghafla mnamo mwaka 2016.

Hata hivyo, siku moja tu baadae, mnamo Juni 5, 2022, Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye suala husika lipo chini yake, Pindi Chana alitangaza kusitisha zoezi hilo hadi pale “Serikali itakapopata taarifa rasmi kutoka katika taasisi husika,” alisema Dk Chana.

Hii haijalishi kuwa TAWA ni taasisi ya Serikali ambayo nayo katika taarifa yake ya Jumamosi ilianza na neno Serikali, ikisema: “Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii […] imeruhusu usafirishaji wa wanyama pori.”

Hakuna cha kushangaza hapa kama wengi wanavyoonekana kulichukulia suala hili. Inawezekana TAWA, taasisi hii ya Serikali iliyoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, haikuwasiliana na waziri kabla ya kutoa tangazo husika.

Kukosekana kwa uratibu ndani ya Serikali siyo jambo geni. Wakati akimuapisha Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Athman Kattanga mnamo Aprili 1, 2021, kwa mfano, Rais Samia Suluhu aliongea kwa uchungu kuhusu wizara, idara na taasisi za Serikali kushindwa kuwasiliana, akimuagiza Kattanga alishughulikie tatizo hilo. Inaonenaka changamoto hizo bado zipo.

Lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa kelele zilizopigwa kupinga uamuzi wa TAWA kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari zilitosha ‘kuitikisa’ Serikali na kupelekea kusitisha zoezi hilo kwa muda.

Kama ni kelele ndizo zilizopelekea usitishwaji basi angalau sasa tumejua kuwa kelele zikipigwa vya kutosha Serikali inasikia na mambo yanaweza yakabadilika. Kwa upande mwingine, hata hivyo, kama usitishaji ulifanyika kwa sababu tu ya kelele za watu, basi kuna tatizo.

Kwa sababu tangazo la TAWA linaonekana kuwa ni la kisheria na usafirishaji huo wa wanyamapori hai ni wa makubaliano ya kibiashara na ya kisheria kati ya wafanyabiashara na Serikali.

Pia, ni lazima ieleweke wazi kuwa haiwezekani kuwa tangazo la TAWA lilikuja kwa ghafla au kwa bahati mbaya. Lazima kuna maandalizi ya ndani ya Serikali yaliyokuwa yamefanywa kwa muda mrefu kabla tangazo halijatolewa.

Mnamo Novemba 9, 2021, kwa mfano, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja alitangaza bungeni kuwa Serikali ingetoa muda wa miezi mitatu kuruhusu wafanyabiashara kusafirisha wanyamapori hai waliosalia kwenye mazizi na mashamba kabla ya zuio la Machi 17, 2016.

Biashara halali

Tanzania ni moja kati ya nchi zilizokuwa zikiruhusu usafirishaji wa wanyamapori hai kabla ya usitishaji wa mwaka 2016. Usafirishaji huu wa wanyama ni sehemu ya uvunaji wa wanyama unaofanywa ili kuongeza kipato cha uhifadhi. Shughuli nyingine za uvunaji ni uwindaji wa kitalii na uvuvi wa kitalii.

Mwaka 2015, kwa mfano, Serikali ilitenga idadi (quota) ya wanyama 64,921 waliotakiwa kuuzwa. Asilimia 78 ya wanyama hao walikuwa ni aina ya reptilia. Uuzwaji huu unaratibiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori na CITES, ambalo ni shirika la kimataifa linalodhibiti biashara ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka.

Katika mazingira hayo ya kisheria, ni wazi kuwa usitishwaji wa zoezi husika kama ulivyofanywa na Dk Chana unaturudisha kwenye machungu ya ugeugeu wa sera za biashara za Serikali ambao ndiyo ulipekelea katazo la mwaka 2016.

Mbunge wa Mtama (Chama cha Mapinduzi – CCM) Nape Nnauye alikuwa sahihi alipotishia kuzuia bajeti ya Wizara ya Maliasilia na Utalii isipitishwe mwaka 2017, akitaka Serikali iruhusu usafirishwaji wanyamapori hai waliokuwa tayari wameshalipiwa na tayari kuondoka wakati wa zuio la ghafla la 2016.

Hoja ya Nape ilijengeka kwenye msingi kwamba ni Serikali yenyewe ndiyo iliruhusu biashara ya kusafirisha wanyamapori hai na kuwa wafanyabiashara walichokifanya ilikuwa ni kuitikia wito wa Serikali kuifanya biashara hiyo.

Wafanyabiashara wakawekeza katika biashara hiyo, wengi wao kwa kuchukua mikopo benki; wakawa wanalipa kodi kwa kufanya biashara hiyo. Wakati Serikali inazuia biashara hiyo, tayari wafanyabiashara hao halali walikuwa wameshalipia wanyamapori hai, wakawaweka mazizini wakifanya michakato ya kuwasafirisha.

Na ndiyo hao ambao TAWA ilisema ingeruhusu wasafirishwe ili kutimiza makubaliano ya mkataba wa kisheria na wafanyabiashara hao.

Nape, ambaye sasa ni waziri kwenye Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, alisema mwaka 2017: “Serikali iruhusu [wafanyabiashara] wasafirishe hao viumbe ambao walikwishawakamata, wakawaweka kwenye mazizi yao kwa kufuata utaratibu, walikata leseni, walilipa kodi na wengine walichukua mikopo benki.”

Nape aliongeza kuwa kama kuna wafanyabiashara waliokiuka masharti ya leseni zao, hatua mahsusi zilitakiwa kuchukuliwa kwa wafanyabiashara hao tu na siyo kuadhibu wafanyabiashara wote.

Ugeugeu

Rais Samia alipoingia madarakani aliahidi kushughulikia na kuondoa mazingira yote yaliyofanya uwekezaji na ufanyaji biashara Tanzania uwe mgumu. Katika hotuba aliyoitoa bungeni mnamo Aprili 22, 2021, Samia alisema moja kati ya matatizo ambayo angeyashughulikia ilikuwa ni suala la sera zisizotabirika.

Katika suala la kusafirisha wanyamapori hai wafanyabiashara wana makosa gani? Kubadilikabadilika kwa kauli za Serikali, hasa kwa kuzuia mambo ambayo Serikali yenyewe iliyaruhusu na hivyo kuleta hasara kubwa kwa wafanyabiashara, kunatoa ujumbe gani kwa wawekezaji?

Hivi kuna muwekezaji mwenye akili timamu atakuja kuwekeza Tanzania wakati akijua mambo yanaweza kubadilika muda wowote?

Ilikuwaje Naibu Waziri Mary Masanja akatoa tamko bungeni kuhusu mpango wa Serikali kuruhusu wanyamapori hai waliosalia mwaka 2016 wasafirishwe? Je, Masanja alijitungia hatua hiyo au huo ulikuwa ni msimamo wa Serikali?

Hasara kwa wanavijiji

Kwa hakika uuzwaji wa wanyama pori umekuwa mjadala mkubwa sana kwa miaka mingi, hususan kutokana na kesi ya utoroshaji wanyama kupitia uwanja wa ndege wa kimataiafa wa Kilimanjaro (KIA) hapo mwaka 2010.

Watu kadhaa, wakiwemo raia wa Kenya na Pakistan, walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mwaka 2011 kwa tuhuma za kutorosha wanyamapori hai 136 na ndege hai kwenda Uarabuni Novemba 26, 2010, kwa kutumia ndege ya Jeshi la Qatar.

Kesi hiyo iliisha Disemba 5, 2014, kwa hukumu ya kifungo cha miaka 60 jela kwa raia wa Pakistani, Kamrani Ahmed, aliyetambulika mahakami kuwa wakala mkuu katika utoroshaji huo.

Watuhumiwa wengine hawakupatikana na kesi ya kujibu. Kamrani pia hakuwepo mahakamani kwa kuwa alikwishatoroka baada ya kuwekewa dhamana. Lakini hata baada ya kesi hiyo bado wafanyabiashara waliendelea kuruhusiwa kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi.

Utaratibu wa Serikali kuruhusu biashara ya wanyamapori hai na kuwasafirisha nje uliwasukuma wanavijiji mkoani Tanga kutoka katika milima ya Usambara Mashariki na wilaya ya Korogwe kufuga na kuuza nje vipepeo hai.

Wanavijiji mkoani Tanga wamekuwa wakiuza wanyamapori hai tangu miaka ya 1990. Lakini ufugaji wa vipepeo ulishika kasi sana kuanzia mwaka 2003. Wakati wa zuio la mwaka 2016, zaidi ya wafugaji 150 kutoka mkoani Tanga walikuwa wanajihusisha na ufugaji na usafirishaji wa vipepeo hai.

Wanavijiji hawa waliokuwa wanaliingizia taifa fedha za kigeni walipoteza uwekezaji wao na kuachwa katika wimbi la umasikini kwa sera zisizotabirika za Serikali.

Suala la msingi

Kitu ambacho Serikali inapaswa kuangalia katika muktadha mzima wa usafirishwaji wanyamapori hai ni umuhimu wa kuwa na sera zisizobadilikabadilika.

Kama Watanzania hawakubaliani na suala la kusafirisha wanyamapori hai hilo siyo suala la wafanyabiashara, wakiwemo wanavijiji wa mkoani Tanga, waliowekeza mabilioni ya shilingi katika biashara iliyokuwa imeruhusiwa na Serikali.

Ni wajibu wa Serikali kutafuta namna ya kuelemisha umma kuhusu biashara hiyo ili angalau wafanyabiashara waliokuwa wameshawekeza katika biashara hiyo waruhusiwe kumalizia mizigo yao iliyokuwa imesalia.

Serikali ni lazima ijue kuwa Tanzania haitaweza kupaa kiuchumi kama sera na taratibu za kibiashara zitakuwa zinabadilika kila siku. Mabadiliko haya ya mara kwa mara yanayotia hasara wafanyabiashara ni ya ajabu ukizingatia kuwa nchi hii imekuwa chini ya chama kimoja cha siasa tangu uhuru.

Je, kama kungekuwa na mabadiliko ya vyama tawala kila baada ya miaka kumi nchini Tanzania hali ingekuwaje? Kwa nini Serikali ya chama kile kile inakuwa na sera kigeugeu za biashara zinazodidimiza nafasi ya Tanzania kushindana kibiashara na nchi nyingine?

Tujitafakari!

Damas Kanyabwoya ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi. Anuwani yake ya barua pepe ni dkanyabwoya@gmail.com. Anapatikana pia Twitter kama @DKanyabwoya. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts