The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kuwaondoa Wananchi Ngorongoro ni Shambulio Dhidi ya Ufugaji wa Asili

Jamii za kifugaji zimekuwa mpango bora wa matumizi ya ardhi yao na wamekuwa wakifanya hivyo kwa sehemu zote ikiwemo Ngorongoro.

subscribe to our newsletter!

Kwa ujumla, katika muktadha wa Tanzania, tuna jamii ambazo zinaishi kwa kutegemea mifugo kama nyenzo yao ya kuendesha maisha yao. Jamii hizi ni pamoja na jamii za Wamaasai, Wasukuma, Wambulu, Wabarbaigi na jamii nyingine nyingi tu.

Jamii hizi kwa sehemu kubwa zinafanya ufugaji wa asili kwa kutumia mifugo ya asili na mbinu za kawaida kabisa za kufuga. Sasa ukweli upo hivi, ni kama tu wavujajasho wengine nchini wanavyopata shida, mfano kama vile machinga, wafugaji wa asili nao wanachangamoto ya kutokuwa na sauti ya nguvu kuweza kufanya mambo yao kusikika.

Wafugaji hawa wa asili wana mchango mkubwa sana kwenye uchumi na hata upatikanaji wa chakula nchini. Mfano nyama ya ng’ombe, mbuzi au kondoo inayoliwa leo nchini asilimia kubwa inatoka kwa wafugaji wa asili kwa mfumo huu unaouna ambao wakati mwingine tunakutana nao mabarabarani.

Kwa hiyo, ukiangalia mnyororo wa thamani wa shughuli zao umeajiri watu wengi sana. Kwa mfano ng’ombe anayetoka Ngorongoro anauzwa kwa mfanyabiashara mnadani, yule mfanyabiashara ananufaisha watu wa usafirishaji, kuna watu wamejiajiri kwenye hayo masoko au minada.

Kuna mapato inapata Serikali kupitia ushuru pale. Akifika mjini kuna watu wameajiriwa kwenye machinjio. Kuna watu wameajiriwa kusafirisha nyama kwenda mabuchani kuuza. Kuna mtu ananunua kwa ajili ya kuuza chakula. Bado pia kuna mazao mengine kama ngozi na kwato vinauzwa. Hao ndiyo wafugaji wa asili tunaowazungumzia.

Kwa hiyo, ukija kwa watu wa Ngorongoro, hii ni jamii ambayo imekuwa ikitegemea ufugaji kama sehemu kubwa ya maisha yao. Na wamekuwa wakiendesha maisha yao kwa kutegemea ufugaji.

Jamii ya Ngorongoro ni Wamaasai kama wanavyotamkwa, na jamii hii imekuwa ikiishi ikitegemea mifugo hususan ng’ombe. Kupitia mfumo huu wa ufugaji umewasaidia kupiga hatua, na hata kusomesha watoto wao ngazi mbalimbali za elimu.

Shambulio dhidi ya wafugaji

Mtazamo wangu wa jumla kuhusiana na suala la Ngorongoro naona kwamba hili ni shambulio kwa ufugaji wa asili kwa sababu ni kwa muda mrefu wafugaji wamekuwa na maeneo ambayo wamekuwa wakiyatumia lakini sisi wengine tulio nje ya mfumo wa ufugaji tukitaka yale maeneo tunatoa sababu kulingana na vile mitazamo yetu itakavyotuongoza. Na mara nyingi tumekuwa tukiyaona maeneo ya wafugaji kama mapori au vichaka au maeneo yasiyo na kazi au thamani kwa jamii

Kwa mfano, yapo maeneo ya wafugaji yamegeuzwa mashamba na mengine yamegeuzwa hifadhi bila kujali mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa na jamii. Hivyo, kupelekea wafugaji kutafuta malisho maeneo mengine ambayo hupelekea na kuchochea  migogoro ya ardhi huko wanakokwenda.

Kwa hiyo, ukifuatilia historia utaona jamii za wafugaji, na hasa wafugaji wa asili, kwa nchi yetu ya Tanzania wamekuwa hawalindwi na sheria yeyote na Ardhi yao imekuwa hailindwi kisheria. Ndiyo maana mara nyingi wanakuwa kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Kuna propaganda nyingi sana kwamba wafugaji wa asili wanaharibu uhifadhi Ngorongoro. Jamii za kifugaji zina mpango bora wa matumizi ya ardhi yao na wamekuwa wakifanya hivyo kwa sehemu zote ikiwemo  Ngorongoro.

Kuna sehemu wanajua kipindi cha kiangazi tunachunga huku na kipindi cha masika tunachunga huku. Hao ng’ombe wamekuwa wakichunga kwenye baadhi ya maeneo na badaye kurudi kwenye maboma yao au mazizi yao.

Kama unavyojua hawa wafugaji pia wanahama na mifugo yao kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine hasa kunapokuwa na vipindi tofauti. Kwa hiyo, mipango ya ardhi kwa jamii ya wafugaji ipo na inafanya kazi vizuri.

Tatizo linakuja pale tunapoingilia kwa kupora ardhi yao na  kwenda kuvuruga ule mpango wa matumizi bora ya ardhi ya jamii wa asili. Ukienda maeneo nje ya Ngorongoro hilo limetokea sana, sababu walipoanza kusumbuliwa wafugaji na kuanzishwa mashamba makubwa ikapelekea hakuna tena ule mpango wa matumizi ya ardhi.

Kwa hiyo, hata ndani ya hifadhi ya Ngorongoro jamii ina hiyo mipango ya matumizi ya ardhi ila sasa zilipoanza hizi vurugu za uwekezaji, mfano eneo jirani na Kreta ya Ngorongoro yaani Loliondo,  walipoingia wawekezaji mfano wa OBC hii mifumo ya matumizi bora ya ardhi ya jamii ya wafugaji iliathiriwa sana na matokeo yake inapelekea wafugaji kusukumia mifugo sehemu moja kwenda nyingine.

Kama wafugaji wangeachwa wakijipanga wenyewe vizuri kwa kushirikiana na mamlaka mambo yangeenda vizuri tu.

Hoja ya mifugo kuzidi

Kuna hoja pia inaibuliwa kwamba mifugo imezidi eneo la Ngorongoro na hivyo kuhatarisha uhifadhi. Si kweli. Hata ukienda kushuhudia utaona hilo siyo kweli.

Siyo kweli kwa sababu hata ukifuatilia katika maboma, zamani boma moja lilikuwa na ng’ombe mia tano mpaka mia sita. Lakini leo watu wana ng’ombe thelathini, hamsini mpaka mia. Kwa hiyo, idadi ya ng’ombe siyo kubwa kama tunavyoaminishwa na baadhi ya watu ili kuhalalisha maamuzi yao.

Ni ukweli usiopingika kwamba ukiwaondoa wale watu wanaoishi ndani ya Ngorongoro ule uhifadhi wenyewe wa Ngorongoro utaondoka. Kwa sababu kuna mahusiano na utegmeano wa watu, makazi ya asili, mifugo na  wanyama pori.

Sasa Ngorongoro ndiyo sehemu pekee unaweza ukakutana na hiyo hali. Kwa hiyo, kukiondoa kitu kimoja kati ya hivyo vilivyopo ndani ya Ngorongoro hivi sasa basi utaondoa upekee wenyewe wa Ngorongoro na kuharibu uhifadhi.

Sasa, kwa ujumla, niseme, ni kweli kwamba uhifadhi ni muhimu lakini pia suala la ufugaji wa asili, kwa maoni yangu, ni ni muhimu pia. Lakini sasa lazima tuliangalie hili suala sawia tusiumize upande mmoja.

Kinachoonekana katika haya yanayoendelea ndiyo kile nilichokisema kuwa ni shambulio kwa wafugaji wa asili na wafugaji wadogo wadogo. Jambo hili hivi sasa linakwenda mbali zaidi kwani ukisikiliza michango ya baadhi ya watu wengine ni wabunge kabisa ndani yake wamefikia hatua hadi ya kutoa kauli zinazoweza kupelekea kutweza utu wa watu wengine, hususan wananchi wa Ngorongoro.

Njia ya majadiliano

Ni maoni yangu kwamba hawa watu wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro waendelee kuwepo pale na hiyo changamoto inayoelezwa ya watu kuongezeka na maendeleo mengine kuhitajika hicho ni kitu kingine kinawezekana kutatuliwa kwa njia ya kujadiliana kwa pamoja kati ya wananchi na mamlaka za hifadhi.

Ninachoona kinachokosekana ni ile baadhi ya watu, hasa wasio wafugaji kutokuwa na mtazamo chanya na ufugaji wa asili ambao mimi naona unawezekana kabisa kuwa endelevu na kutunza uasili wa eneo la Ngorongoro.

Kwa sababu hata ukienda kwenye nchi za wenzetu zilizoendelea, kwa mfano Hispania, italy, ufaransa n.k kuna wafugaji wa asili na wana siku yao maalum ya kufurahia ufugaji wa asili ijulikanayo kama transhumanes festival. Hayo ni mambo mazuri ambayo unaweza kuiga ambapo nchi inatambua ufugaji wa asili na kuwalinda hata kama ni wachache.

Ukisoma sera ya mifugo haitambui uendelezaji wa ufugaji wa asili bali inazungumzia kubidhaisha ufugaji ili hali ukisoma sera za nchi nyingine zinajivunia na kuipa serkali kazi ya kutunza ufugaji wa asili mfano ni sera ya mifugo ya nchi ya India ambayo inaitaka serkali kuweka miundombinu rafiki katika mapitio ya wafugaji wa asili.

Lakini huku kwetu tunachukulia ufugaji wa asili ni uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa uhifadhi. Tunafikiria ufugaji wa asili ni mfumo wa zamani ambao umepitwa na wakati na vitu kama hivyo.

Kwa hiyo, tulipaswa kuangalia kwa mtazamo wa kwamba hawa Watanzania wenzetu waliopo Ngorongoro, ambao wengine wanapenda kutumia lugha ya kusema Wamaasai wa Ngorongoro, wao wenyewe wanafahamu kwamba ni sehemu ya uhifadhi?

Na Serikali, pamoja na wadau wengine, hasa wanaoeneza maneno kwamba uhifadhi utapotea watu wakiendelea kuishi mule ndani, wanapaswa kuona kwamba hawa ni sehemu ya uhifadhi na upekee wenyewe wa Ngorongoro ambao unasifika sasa hivi kote duniani.

Eliud Letunga ni Mshauri wa masuala ya wakulima na wafugaji  anapatikana kupitia baruapepe ellyletungaa@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts