Kumekuwa na maswali mengi yakiulizwa na wananchi wa Zanzibar kwa siku za hivi karibuni kiasi ya kuwa sehemu kubwa ya mjadala katika nchi yetu na ambayo tunaona Katiba ya Zanzibar imetubebesha wajibu kuyasemea na kutaka majibu kutoka kwa wenye mamlaka. Hoja zinazotolewa zinahusu kutofuatwa taratibu za kisheria katika manunuzi na matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kupelekea upotevu wa fedha za umma.
Tokea kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nane, wananchi wamesikia viongozi wakikemea ufisadi mkubwa katika miradi mbali mbali iliyosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Saba. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ule wa kuboresha miji unaojulikana kwa jina la Zanzibar Urban Services Project (ZUSP).
Kutokana na ubadhirifu mkubwa, viongozi wamekuwa wakieleza kuwa mradi huo haukuleta tija iliyokusudiwa. Mheshimiwa Rais Hussein Mwinyi ametoa ahadi mara kadhaa hadharani kuwa atapambana na ufisadi ili kuepusha matumizi mabaya ya fedha za umma ili makosa ya nyuma yasijirudie.
Baada ya wananchi kuona kuna dalili ya yale yaliyotokea nyuma kujirudia ndio maana wamehoji, wanahoji na wataendelea kuhoji iwapo hawatopata majibu ya kuridhisha na yanayotosheleza.
Chama chetu cha ACT Wazalendo kimejiridhisha kwamba zipo hoja za msingi ambazo Serikali inapaswa kuwapa wananchi majibu ya wazi na ya kutosheleza badala ya maelezo ya kisiasa ambayo wakati mwengine yameambatana na vitisho na kejeli.
Mradi wa ujenzi wa barabara za ndani
Thamani ya mradi huu tumeambiwa ni dola za kimarekani milioni 80. Hizi ni sawa na Shilingi bilioni mia moja na themanini na sita. Fedha hizi ni sawa na mshahara wa watumishi wote wa Serikali kwa zaidi ya miezi mitano. Ni zaidi ya asilimia 10 ya mapato yote ya ndani yaliyokadiriwa kukusanywa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha. Kwa kiwango chochote kile, ni fedha nyingi sana kwa Zanzibar.
Hoja zinazohitaji majibu kutoka kwa Serikali ni pamoja na ni kwa nini mradi huu amepewa mkandarasi bila ya kuitishwa zabuni ya wazi yenye ushindani? Rais Mwinyi anasema sababu ya kutoitishwa zabuni ni kuwa mradi huu unajengwa kwa utaratibu wa ujenzi wa mkopo (EPC PLUS FINANCE). Kwamba ni fedha za mjenzi na kwamba mjenzi ametoa bei rahisi sana ya ujenzi. Hapa kuna maswali kadhaa ambayo yanahitaji majibu.
Mwanzo kabisa, Sheria ya Manunuzi ya Umma Namba 11 ya 2016 inapaswa kutumika kwa matumizi ya fedha za aina zote za umma, zikiwemo fedha za mkopo. Ujenzi kwa mfumo wa mjenzi kutoa fedha kwa mkopo ni utaratibu wa kawaida duniani. Ni moja tu ya aina za mkopo na wajenzi wanaotoa huduma hiyo wapo wengi sana duniani. Katika mfumo huu wa ujenzi yapo maswali kadhaa.
Pili, ni taasisi gani iliyokuwa mnunuzi (procuring entity)? Je, ni Wizara ya Ujenzi, ni Ofisi ya Rais au ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo ndio kiongozi wa Timu ya Serikali ya Mapatano (Government Negotiating Team)? Suala hili ni muhimu kwa sababu wananchi hawajasikia Waziri wala watendaji wa Wizara kutoa majibu ya hoja za wananchi kuhusu mradi huu.
Tatu, ni vipi Serikali ilimpata mjenzi? Na je, Wizara husika ilifuata masharti ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kupata kibali maalum cha kutumia mfumo huo maalum wa manunuzi kama inavyotakiwa na Sheria?
Nne, bei na masharti aliyotoa yalilinganishwa na mzabuni gani mwengine? Tano, je, Serikali ilimfanyia tathmini wakati gani? Je, ni kweli kuwa Serikali iliingia mkataba na mzabuni kabla hata kumfanyia tathmini uwezo wake kwani mjenzi huyo hajawahi kufanya kazi hata moja Tanzania wala Zanzibar?
Sita, bei ya dola milioni 80 iliamuliwa wa kigezo gani wakati Serikali iliingia mkataba kabla ya usanifu wa barabara kufanyika? Saba, fedha za ujenzi ambazo tunaambiwa kuwa ni mkopo, zitalipwa kwa utaratibu gani na mkopo huu unatakiwa ukamilishwe ndani ya muda gani?
Majibu yanayotolewa na Serikali ni mepesi mno na yasiyoakisi uwajibikaji na kujali kwamba fedha hizo ni za umma wa watu maskini sana. Sheria ya Manunuzi ya Umma imesisitiza uwazi, usawa, ushindani, kutokuwepo upendeleo na kuzingatia thamani ya fedha kwa bidhaa au huduma zinazolipiwa (value for money) katika manunuzi yote ya Serikali.
Namna utoaji zabuni na upatikanaji wa mjenzi ulivyofanyika katika mradi huu hautimizi hata kigezo kimoja cha sheria, uadilifu na uwazi. Maswali tuliyoyaorodhesha hapo juu yanahitaji majibu ya kina, ya kutosheleza na yanayozingatia misingi ya sharia.
Wananchi walitaraji viongozi wa Serikali, hasa Mheshimiwa Rais, kuwahoji watendaji waliohusika na mchakato wa manunuzi katika mradi huu, ama kuvitaka vyombo husika kuchunguza, badala ya kuonekana kukasirika na wanaohoji ukiukwaji wa wazi wa sheria na taratibu za manunuzi.
Kwa vile sheria ya manunuzi inalazimisha kuwekwa kwa kumbukumbu zote za manunuzi hadi mradi utapokamilika, tunategemea wananchi watawekewa wazi badala ya kupewa kauli za kejeli.
Uendeshaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa
Mradi huu unajumuisha fursa ya kibiashara kwa kampuni ya Dnata yenye Makao Makuu yake Dubai, UAE na washirika wake kuendesha shughuli za uendeshaji wa uwanja wa ndege sehemu ya ndani (land side) ikiwemo maduka, kumbi za kupumzikia (lounges), migahawa, maegesho nakadhalika.
Mbali ya kampuni hizo kupata faida kwa kukodisha na kuendesha sehemu hizo, Serikali bado inawajibika kuwalipa ada ya utaalamu katika uendeshaji ya takriban dola za kimarekani zisizopunguna elfu sabini ($70,000) kwa mwezi.
Mbali ya biashara hiyo, kampuni ya Dnata imepewa haki (concession) ya kuendesha biashara ya kuhudumia ndege (ground handling services) ambayo kwa sasa inaendeshwa na kampuni mbili za ZAT na Transworld. Kampuni ya Dnata imepewa haki ya kipekee (exclusivity) ya kuendesha shughuli zake katika jengo jipya la abiria (Terminal 3) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Kwa maana hiyo watakapoanza kazi, kampuni mbili zinazotoa huduma sasa hivi hazitokuwa na haki hiyo kwenye Terminal 3. Mchakato wa utoaji zabuni katika mradi huu katika hatua zake zote una dalili zote za kupindisha sheria, kanuni na taratibu katika hali ambayo inazua maswali mengi ya nani hasa anatoa msukumo huo na nani anakusudiwa kufaidika?
Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Namba 8 ya 2011, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (Zanzibar Airports Authority) kupitia Bodi yake ya Wakurugenzi ndiyo yenye uwezo wa kuendesha viwanja vya ndege ama moja kwa moja au kwa kupitia watoa huduma watakaoingia nao mkataba.
Kwa hivyo, ZAA ndio yenye uwezo wa kuamua kama wanahitaji watoa huduma. Ni ZAA ndiyo yenye uwezo wa kuanzisha mchakato wa manunuzi kwa kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma. Kama Serikali kupitia Waziri mwenye mamlaka juu ya ZAA inahitaji ZAA kutafuta mtoa huduma, Serikali inatakiwa itoe maelekezo kwa Bodi ya ZAA na kuwaachia waendelee na mchakato huo.
Hoja muhimu hapa ni je, utaratibu huo ulifuatwa au haukufuatwa? Maelezo yanayotoka serikalini yamekuwa yakiitaja Timu ya Serikali ya Mapatano (Government Negotiating Team). Swali linakuja, ni nani walikwapua mamlaka hayo ya Bodi ya ZAA na kuipa Timu ya Mapatano ya Serikali inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu?
Je, Bodi ya ZAA iliarifiwa juu ya kutafuta mzabuni na kuachiwa kusimamia mchakato huo ambayo ni majukumu yake? Kwa kukwapuliwa majukumu hayo kutoka kwenye Bodi na kupewa Timu ya Serikali ya Mapatano (kama maelezo yaliyotolewa yalivyotaja), ni wazi kuwa waliohusika kufanya hivyo walikiuka maelekezo ya wazi ya kisheria ambayo hayawezi kutenguliwa na mtu yeyote.
Suala muhimu tunalouliza, ni kwa nini Rais haoni kwamba kukiuka sheria kwa kiwango hicho ni tatizo? Na kwamba wahusika wanapaswa kuwajibishwa? Kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, mchakato wa kupata mtoa huduma ulipaswa uwe wa wazi, wenye ushindani, wa haki na unaofuata utaratibu uliowekwa.
Kama kulikuwa na mazingira maalum ambayo yalilazimisha kutumia njia mbadala isiyokuwa ya wazi na yenye ushindani, wahusika walipaswa kuomba idhini kutoka kwa Mamlaka ya Manunuzi Zanzibar kama Sheria inavyoelekeza. Je, maelekezo hayo yalifuatwa? Na kama hayakufuatwa, ni kwa nini hayakufuatwa? Na kama hayakufuatwa, ni nani anayesimamia yasifuatwe?
Maswali mengine muhimu ni vipi Dnata ilipatikana, nani alifanyia tathmini, kiwango cha ada ya dola 70,000 anacholipwa kwa mwezi kimeamuliwa kushindanishwa na kiwango gani cha ada? Maswali haya yaahitaji majibu na yasipopatiwa majibu, wananchi watakuwa na sababu za kuhoji iwapo hakuna ufisadi katika mradi huu.
Kwa mujibu wa uamuzi Namba 1 wa 2016 wa Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA), Kiwanja cha Ndege cha Zanzibar kinapaswa kihudumiwe na watoa huduma wasiozidi wawili. Wakati Serikali inaingia mkataba wa kutoa huduma kwa ndege na kampuni ya Dnata tayari zilikuwepo kampuni mbili za kutoa huduma kwa ndege.
Hivyo, kuingia mkataba na kampuni ya tatu na kuipa kampuni hiyo haki ya kipekee (exclusivity) ilikuwa na maana kwamba Serikali ilikusudia kuziondoa kampuni mbili zilizokuwepo kwa nguvu au kwa njama. Hiyo ni kwenda kinyume na Sheria na miongozo ya Sheria ya Mamlaka ya Anga (TCAA).
Mbali ya kwenda kinyume na Sheria ya Mamlaka ya Anga (TCAA), Serikali iliwapa Dnata ambayo haikuwa na haistahiki kupata leseni ya kutoa huduma kwa ndege Zanzibar, haki ya kipekee ya kibiashara ya kutoa huduma katika jengo jipya. Utaratibu huo ni kuvunja Sheria ya Ushindani wa Kibiashara ya Zanzibar Namba 5 ya 2018.
Chini ya kifungu cha 44 cha Sheria hiyo ni kosa la jinai kuingia mkataba wa kupunguza ushindani au kutoa upendeleo usiokuwa na ushindani. Suala muhimu ni kuwa je, waliohusika na maamuzi haya hawakujua kwamba kwa kuingia mkataba wenye upendeleo na Dnata wanatenda kosa la jinai?
Kwa mujibu wa Kanuni za Utoaji Huduma kwa Ndege (Ground Handling Service Regulations) zilizochapishwa chini ya Tangazo la Serikali Namba 251 la 2013, Kanuni ya 6 ya Kanuni hizo inalazimisha mwekezaji wa kutoa huduma kwa ndege lazima awe na asilimia 35 ya hisa za mtu ambaye ni Mtanzania.
Dnata inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali na hivyo haikustahiki kupewa mkataba wala leseni ya kutoa huduma kwa ndege na ndio maana Mamlaka ya Anga Tanzania imewakatalia kuwapa leseni na hivyo kulazimika kusajili Kampuni tanzu yenye hisa za mwenyeji.
TCAA wenyewe kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Ndugu Hamza Johari, imeeleza kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kwamba Dnata haikuwa na leseni na haina sifa ya kupewa leseni na kwa hivyo Serikali ya Zanzibar haikupaswa kuingia mkataba nao.
Ni mwezi uliopita tu ndiyo Dnata Zanzibar ikiwa ni kampuni tanzu ya kampuni ya Dnata ya Kimataifa imepewa leseni na TCAA. Suala hapa ni kuwa kwa nini Serikali iliingia mkataba na kampuni ya Dnata ya Kimataifa ambayo haikuwa na leseni na hata sasa haina leseni?
Ifahamike kwamba mbele ya macho ya sheria, kampuni ya kimataifa ya Dnata yenye makao makuu Dubai na kampuni ya Dnata Zanzibar iliyopewa leseni na TCAA mwezi uliopita ni wahusika wawili tofauti kisheria (two different legal entities).
Suala la muhimu hapa ni je, waliohusika na maamuzi haya wakati wanaingia mkataba na Dnata hawakuzijua Sheria na Kanuni hizi ambazo wao ndio wasimamizi?
Pametolewa hoja kwamba kampuni mbili zilizopo zimeshindwa kutoa huduma kwa viwango vinavyostahiki na kwa hivyo, palikuwa na ulazima wa kutafuta kampuni ya kimataifa yenye hadhi. Hapo hapo pametolewa hoja kwamba Dnata imekubali kutoa malipo (concession) zaidi kwa Serikali ambayo ni asilimia 12 badala ya asilimia nane wanayotoa kampuni zinazotoa huduma hivi sasa.
Maswali yanayohitaji majibu ni hayo malalamiko ya kutoridhika na huduma yalitolewa na nani kati ya wahusika ambao ni aidha mashirika ya ndege yanayohudumiwa, TCAA, Shirika la International Civil Aviation Organisation (ICAO) au IATA?
Na kama palihitajika kuinua huduma hizo, kwa nini kufanyike njama za kuwatoa waliopo sasa kwa kuvunja sheria, kanuni na taratibu zote badala ya Serikali kupitia ZAA kukaa na kampuni hizo na kuzitaka zitafute wabia wa kimataifa wenye hadhi inayotakiwa?
Na kuhusiana na malipo ya “concession” kufikia asilimia 12, je, Serikali ilikaa na kampuni za Kizanzibari zinazotoa huduma hivi sasa na kuwataka waongeze wakakataa?
Maswali haya ni mbali na hoja nyingine kwamba unapoipa kampuni ya nje haki ya kipekee (exclusivity) ya kuhudumia Terminal 3 bila ya shaka unaipa upendeleo (advantage) utakaoongeza faida kwao na kwa hivyo kuongeza “concession” haiwezi kuwa tatizo kwao. Hii ni tofauti na hali ya sasa ambapo kuna kampuni mbili zinazoshindana.
Mbali na kampuni zinazohudumia ndege (ground handlers), Dnata pia imepewa haki ya kipekee (exclusivity) katika kazi ya utoaji huduma na uendeshaji wa maduka ndani ya Terminal 3.
Hoja wanayouliza wananchi ni kwamba wale Wazanzibari ambao wamekuwa wakitoa huduma na kuendesha maduka ndani ya Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kwa zaidi ya miaka 15, tena katika hali ngumu, hawana haki ya kufikiriwa kutoa huduma na kuendesha maduka katika Terminal 3 ambako sasa ndiko wasafiri wa ndege za kimataifa watakapokuwa wanahudumiwa?
Ni kwa nini Serikali haikuona haja ya kuweka masharti kwa Dnata kuwazingatia wazalendo hawa waliofanya kazi hii kwa miaka yote hii? Je, huku kweli ndiko kuwajali Wazanzibari? Wananchi wana haki ya kupata majibu ya wazi na ya kutosheleza katika sakata hili lote.
Ukodishwaji visiwa vidogo
Katika ukodishwaji wa visiwa, pamoja na kuwepo timu ya wasimamizi wa ukodishaji na pia kutolewa utetezi, tena ukiambatana na hasira, lakini bado kuna maswali na hoja za msingi ambazo haziashirii dalili njema.
Miongoni mwa maswali na hoja hizo ni pamoja na ukweli kwamba tuliambiwa kupitia taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Ndugu Sharif Ali Sharif aliyoitoa Disemba 23, 2021 kwamba katika kuamua washindi wa zabuni za ukodishwaji wa visiwa, vigezo vitano vilizingatiwa.
Vigezo hivyo alivitaja kuwa ni: (1) uwezo wa mwekezaji; (2) uwekezaji wenye tija kwa taifa; (3) kiwango cha mtaji wa uwekezaji; (4) uwekezaji wenye kuzingatia hifadhi ya mazingira na ushirikishwaji wa wananchi; na (5) kiwango cha malipo ya awali (lease acquisition costs) ambazo mwenyewe alisema wanaziita “mahari.”
Swali la kwanza na ndilo la msingi kabisa ni kwamba iwapo walizingatia hoja ya ushirikishwaji wa wananchi ambayo ni kigezo namba 4, je, ni vipi tena tulishuhudia wananchi wa maeneo husika wakitoka hadharani kupinga ukodishwaji wa visiwa hivyo?
Pili, Ndugu Sharif alitaja malipo yote yaliyofanywa hadi wakati anatoa tangazo hilo kwa ukodishwaji wa visiwa tisa alivyotangaza siku hiyo ni dola milioni nane na akasema malipo yakikamilika zitakuwa ni dola milioni 12. Fedha hizo hata zikikamilika zitakuwa sawa na shilingi bilioni 27.6 za Tanzania.
Suala linalokuja ni kwamba hivi Serikali imeona thamani ya kiasi hicho cha fedha (tena kwa kukodishwa kwa muda ambao haukutajwa) zinalingana na gharama watakayolipa wananchi wa Zanzibar kwa kutokuwa na haki na visiwa hivyo kwa kipindi chote ambacho vitakuwa viko chini ya waliokodishwa? Suala jengine, ni je, visiwa hivyo vimekodishwa kwa miaka mingapi? Ni miaka 33, 66 au 99?
Tatu, wakati anataja majina ya kampuni zilizokodishwa visiwa hivyo, Ndugu Sharif alikuwa akiainisha zile zinazomilikiwa na aliowaita wazawa au wazalendo.
Suala ni kwamba kwa hizi kampuni nyingine alizozitaja, kwa mfano, Changuu Lodge Limited iliyopewa kisiwa cha Changuu, Bawe Retreat Limited iliyopewa kisiwa cha Bawe, East Africa Investment (Mauritius) Limited iliyopewa kisiwa cha Misali na Tulia Zanzibar Beach Resort iliopewa visiwa viwili vya Pamunda A na Pamunda B ni nani hao wamiliki wake wa kigeni?
Nne, kutokuwepo mchakato wa wazi wa tathmini za zabuni na uchaguzi wa walioshinda zabuni.
Tano, mpango huo kusimamiwa na ZIPA ambayo haina uwezo kisheria kusimamia ukodishwaji wa ardhi na ni jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Ardhi na Sheria ya ZIPA yenyewe. Mamlaka aliyovishwa Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA katika ukodishwaji wa visiwa yanaibua maswali na hoja nyingi na Serikali ina wajibu wa kuwapa wananchi wanaohoji majibu ya wazi na yenye kujitosheleza.
Sita, katika utetezi ambao umekuwa ukitolewa, kumekuwa na majibu kwamba Serikali ya sasa siyo ya kwanza kuanza kukodisha visiwa na kufikia kutajwa baadhi ya visiwa vilivyokodishwa huko nyuma. Hapa suala ni kwamba hata kama ilifanyika hivyo na tuseme na huko nyuma taratibu hazikufuatwa, je, makosa mawili yanafanya jambo kuwa halali? Huu ni utetezi wa aina gani?
Masoko ya Chuini, Mwanakwerekwe na Jumbi
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Serikali, miradi ya ujenzi wa masoko hayo hautumii fedha za Serikali bali fedha za wawekezaji binafsi. Miradi yote hii mitatu ina harufu kali ya ufisadi na kwa sababu hiyo wananchi wana haki ya kupewa majibu ya wazi na yenye kujitosheleza.
Miongoni mwa mambo yanayoacha maswali hayo ni, kwanza, katika kuandaa miradi hiyo Serikali ilipaswa kujua mahitaji yake, ubora unaohitajika na gharama za ujenzi kabla ya kuwaalika wawekezaji binafsi. Kwa kukosekana uwazi katika thamani, gharama za ujenzi wa masoko hayo umekuwa mkubwa kupindukia.
Kwa mfano, Soko la Chuini shilingi bilioni 36, Mwanakwerekwe bilioni 46 na Jumbi zaidi ya bilioni 30 zinaonesha wazi kuwa ni kubwa kupitiliza. Mfano wa karibu wa miradi kama hiyo ambayo imejengwa kwa gharama ndogo zaidi ni ujenzi wa Soko la Kisutu miaka miwili iliyopita uligharimu si zaidi ya bilioni 14 ukiwa na ghorofa nne pamoja sehemu ya chini ya kuegeshea magari.
Soko Kuu la Mwanza lilojengwa miaka mitatu iliyopita lilijengwa kwa gharama isiyozidi bilioni 24 na Soko la Job Ndugai Dodoma lilojengwa kwa gharama ya chini kuliko masoko ya Zanzibar.
Pili, Serikali ilipaswa kutoa mwaliko wa wazi kwa wawekezaji wote wenye uwezo. Sheria ya Manunuzi ya Umma na hata ile ya Public Private Partnership (PPP) zinataka uwazi na ushindani na ipatikane thamani kwa fedha zitakazotumika. Kukosekana kwa uwazi na uadilifu kumepelekea masoko yote hayo kupata wawekezaji wasio na uwezo kifedha. Kwa bahati, hili limeshuhudiwa na umma wote kupitia ziara zilizofanywa na Makamu wa Pili wa Rais kwenye maeneo ya masoko hayo ambako ilisemwa kwamba ujenzi unaendelea.
Ni aibu kubwa kwa Serikali kuingia katika mikataba na wawekezaji wasio na uwezo kwa miradi mikubwa kama hiyo na inayogusa maisha ya watu moja kwa moja. Je, ni nani waliokuwa nyuma ya miradi hii ya masoko na ambao kwa hali ilivyo sasa bila shaka kuna ufisadi mkubwa nyuma yake? Nani aliwaidhinisha? Na ni kwa nini bado Wakuu wa Serikali wanashindwa kuwawajibisha?
Tatu, kuchelewa na kusuasua ujenzi wa miradi yote mitatu ni fedheha kubwa lakini ni mateso makubwa kwa wananchi waliokuwa wakitumia masoko yaliyovunjwa ya Mwanakwerekwe na Jumbi. Hivyo, mbali ya Serikali kuwajibika kuwapa majibu wananchi, inawajibika pia kuwafidia kwa hasara kubwa na usumbufu waliyopata.
Uuzaji wa nyumba za Mji Mkongwe
Uuzaji wa nyumba za Mji Mkongwe, hasa nyumba za Serikali, umegubikwa na kukosekana uwazi, maamuzi ya ubabaishaji na kukosekana uadilifu. Ingawa awali yalitolewa matangazo ya kukaribisha ununuzi lakini baada ya hapo kila kitu kimekuwa siri na kupelekea maswali mengi yasiyo na majibu.
Kwanza, wangapi waliomba kununua nyumba hizo na bei iliyotolewa na kila mmoja? Pili, vigezo vilivyotumika katika kuwabariki waliouziwa nyumba hizo? Tatu, kiasi cha fedha kilichopatikana? Nne, maslahi ya umma yamezingatiwa?
Ni muhimu kupata majibu ya maswali hayo kwa vile zipo hoja kwamba baadhi ya nyumba wameuziwa watu ambao hawakuomba kuuziwa. Nyumba kama inayotumiwa na Shirika la Nyumba waliouziwa mwanzo walipewa kwa bei ya chini sana haijulikani kwa vigezo gani na baadae wakapokonywa na Serikali kwa kisingizio kuwa wamepewa kwa bahati mbaya na kuuziwa mtu ambaye hakuomba na haijulikani kwa kiasi gani.
Ofisi za Serikali zilizohamishwa katika nyumba zilizouzwa zimehamishwa bila ya maandalizi ya uhakika na hivyo kuathiri utendaji wa kazi zao. Kwa sababu hiyo, Serikali lazima itoe majibu ya kutosha juu ya kadhia hizo na mazingira yake.
Katika hili la nyumba za Mji Mkongwe, jambo ambalo limezua maswali makubwa na kuwashangaza wananchi wengi ni linalohusu Skuli ya Tumekuja. Skuli hii yenye historia kubwa Zanzibar imetangaziwa kupewa mwekezaji eti kwa hoja kwamba ni mbovu na ni hatari kwa wanafunzi.
Wanafunzi wameonekana wakihamishwa na madeski yao. Badala yake, tunaambiwa mwekezaji aliyepewa skuli hiyo atajenga madarasa 40 katika eneo la Mwembeladu. Hivi kweli ndiyo wenye mamlaka wamechoka kufikiri kiasi hichi?
Kwamba hatujui kutofautisha thamani ya eneo kama la Shangani linalokabiliana na bahari (prime location) na eneo kama la Mwembeladu? Hivi Serikali imeshindwa kuwa na fedha za kulitengeneza na kulitunza jengo hilo la Skuli ya Tumekuja?
Na iwapo mwekezaji huyo ana mapenzi makubwa na Zanzibar, kwa nini asiitengeneze Skuli ya Tumekuja na kuwakabidhi Serikali iendelee kutumika kama skuli? Hivi maeneo ya uwekezaji yamemalizika hadi tutoe Skuli kugeuzwa hoteli? Ni taifa gani hili lisilothamini urithi wake wa historia?
Maswali haya yanaulizwa huku skuli nyingine mbili za Darajani na Vikokotoni nazo zikiwa hazijulikani hatima yake. Serikali inapaswa iseme je, aliyepewa Skuli ya Tumekuja na aliyepewa nyumba iliyokuwa Shirika la Nyumba siye mtu huyo huyo?
Je, hakuna mpango wa kuunganisha majengo hayo na kuyafanya hoteli moja? Haya ni maswali ambayo wananchi wanahitaji majibu yake, tena ya kutosheleza.
Dhima ya kupiga vita ubadhirifu
Serikali ya Zanzibar inapaswa kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, usawa, amani na uadilifu. Tumesisitizwa kwamba mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.
Tumesisitizwa kwamba tuna wajibu wa kuhakikisha tunasimamia uhuru, mamlaka, ardhi, umoja, maliasili, mali ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa Zanzibar kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadae ya taifa letu.
Na kwa namna ya pekee, tumesisitizwa kwamba vyeo vyote vya madaraka ni dhamana na vipo kwa faida na manufaa ya umma na kwamba wale wote walio na madaraka watawajibika ama moja kwa moja kwa umma au kupitia vyombo vya uwakilishi.
Sisi ACT-Wazalendo leo hapa tumetekeleza wajibu wetu wa kikatiba kama wananchi wa Zanzibar lakini pia kama chama ambacho Wazanzibari wanakitegemea kisimamie hoja zao. Tumeibua maswali ambayo yanahitaji majibu na siyo kejeli au vitisho.
Watu kusema kwamba watatia pamba masikioni kwenye masuala yanayohusu umma na yanayohusu Katiba na Sheria si hekima wala si busara za uongozi.
Katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ndiyo miongozo ya kuongoza na kuendesha nchi. Wajibu wetu wananchi ni kuhoji na kusimamia uwajibikaji kutoka kwa walio kwenye mamlaka.
Ni wajibu wa walio kwenye mamlaka kutoa majibu na kuwajibika kwa wananchi. Iwapo tuna nia na utashi, muda wa kusawazisha haya bado upo.
Ismail Jussa ni mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania ambaye anahudumu kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo. Kwa sasa, Jussa pia anahudumu kama Kaimu Kiongozi wa chama hicho. Anapatikana Twitter kama @IsmailJussa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.