Hivi ulimwengu ndiyo umebadilika au walimwengu ndiyo waliobadilika? Ninachokiona mimi katika karne hii kinasikitisha na kusononesha sana. Imani yangu ni kwamba kwenye kundi hili siko peke yangu bali wapo watu wengi wataungana na mimi kwenye hitimisho langu hilo.
Ulimwengu wa sasa hivi ni kama kila mmoja anapenda kusikia tu kile anachopenda kusikia na ukienda tofauti na matakwa yake basi unakuwa adui ghafla; unaonekana huna adabu, huna nidhamu na kuna uwezekano mkubwa sana maoni yako ikawa ni chanzo cha kupoteza hata kazi yako.
Hiyo iko hivyo haijalishi kama unachokisema ni cha ukweli au cha uongo. Hakuna mtu anatumia muda wake kutafakari na kufanya utafiti kugundua kama ulichosema ni ukweli au ni uzushi. Nitatumia mfano wa sakata linaloendelea la Cristiano Ronaldo kufafanua hoja yangu ya msingi.
Sakata la CR7
Ilipofika kipindi cha usajili, Cristiano Ronaldo alikuwa katika nafasi ya kuhitajika na vilabu vingi ulimwenguni kwa ajili ya kuwatumikia. Moja ya vilabu hivyo ni Manchester City, timu ambayo hakuna shabiki yoyote wa Manchester United angefurahi kumuona CR7 akienda kuwatumikia City.
Yalipigwa maneno mengi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari mbalimbali na mwisho wa siku raia huyo wa Ureno akaamua kurudi Manchester United kutokana na historia aliyokuwa nayo na klabu hiyo.
Msimu wake wa kwanza siwezi kusema ulikuwa mbaya kutokana na umri wake na aina ya wachezaji waliokuwa wamemzunguka. Alifanikiwa kutia kambani magoli 18 kwa msimu mzima.
Alionekana ana ari na nia ya kuipambania Manchester United kuhakikisha inabaki katika nne bora ili iweze kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya.
Mnamo Februari 2022, zilisambaa taarifa kuwa Cristiano Ronaldo alimfuata aliyekuwa kocha wa Manchester United kwa muda ule, Ralf Rangnick, na kumwambia kuwa wachezaji hawakuwa wanaridhishwa na utendaji kazi wa nahodha wa timu Harry Maguire na kushauri apumzishwe.
Ronaldo anasemekana kumwambia Rangnick kwamba hatu hii ni muhimu kama kweli kocha huyo alihitaji matokeo mazuri msimu huo.
Cristiano Ronaldo alikuwa anapendekeza wachezeshwe Erick Bailly na Victor Lindelöf ambao, kimsingi, kwa wakati huo walikuwa wanafanya vizuri kuliko Harry Maguire.
Raf hakutilia maanani ushauri wa mchezaji mwenye uzoefu na anayeifahamu vizuri Manchester United na kuamua kuendelea kumtumia Harry Maguire.
Cristiano Ronaldo hakuonesha kukasirishwa na chochote; aliendelea kutumikia klabu na kupachika magoli 10 kati ya Februari hadi mwisho wa Msimu.
Hii inaonesha alikuwa tayari kuipambania timu kuhakikisha inabaki katika Michuano ya Klabu Bingwa. Msimu mpya ulipoanza kukawa na maneno mengi mitandaoni.
Kushambuliwa
Cristiano Ronaldo akawa ni mwenye kushambuliwa na baadhi ya wachezaji wa zamani wa Manchester United pamoja na mashabiki kadhaa mitandaoni.
Hii ni licha ya kuthibitika kuwa kiungo huyo alikuwa na matatizo ya kifamilia ambayo kimsingi yalimlazimu kukaa na familia zaidi kuliko kazi yake, kama binadamu mwengine yoyote tu angefanya.
Hata hivyo, Ronaldo aliamua kutulia na klabu licha ya kutoshiriki katika Michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya, moja ya michuano ambayo anaongoza kwa kuweka rekodi kadhaa katika michuano hiyo. Kwa kifupi unaweza kusema ni michuano yake.
Ralf Rangnick aliondoka klabuni na Erik ten Hag akatambulishwa rasmi kama kocha wa Manchester United.
Kutokana na historia ya wawili hawa ilikuwa matarajio ya mashabiki wengi ulimwenguni kwamba wanaweza kufanya kazi vizuri na Cristiano Ronaldo akabaki kwenye ubora wake na kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri.
Katika mikutano yake na wanahabari, Erik ten Hag alinukuliwa akikiri kuhitaji huduma ya Cristiano Ronaldo na alisema wazi ana mipango naye kwenye timu hivyo na hafikirii kuruhusu klabu kumuuza mchezaji huyo mkongwe.
Msimu ulianza ukiwa na kupanda na kushuka huku klabu ikijitahidi kupanda nafasi za juu lakini bado kuna safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya kuweza kurudi katika ubora ule wa Klabu ambao wengi tuliuzoea.
Ikafika kipindi mambo yakaanza kumwendea kombo Cristiano Ronaldo na kocha akaamua kuwa anamuweka benchi katika mechi muhimu zingine ambazo ilikuwa wazi huduma yake inahitajika.
Kocha akawa mwingi wa sababu, akisema mara hajamchezesha Ronaldo kwa sababu anamheshimu sana, hivyo asingependa kumuweka timu ikiwa imeshafungwa vile, akizungumzia ile mechi dhidi ya Totenham Spurs.
Ukiangalia katika jicho la kiutaalamu na kiuchambuzi, kocha yoyote hatakiwi kufanya vitu kama hivyo, yaani kutoa sababu za ajabu vile eti ni heshima kwa mchezaji.
Umemsajili mchezaji ili akae tu benchi au umemsajili aweze kuisaidia timu kupata matokeo mazuri hata kama mmeshafungwa 10 kipindi cha kwanza?
Ila ndiyo hivyo, Cristiano Ronaldo aliendelea kushambuliwa na wengi wakiwemo wachezaji wa zamani wa Manchester United na wengine wa vilabu vingine ambao wamevitumikia vilabu vyao na hawakuwahi kushinda hata taji moja ila wanapata nguvu ya kumsema Cristiano Ronaldo.
Mahojiano na Morgan
Mnamo Novemba 13, 2022, Cristiano Ronaldo amefanya mahojiano na mwanahabari Piers Morgan na kufunguka mambo mengi kuhusu mategemeo yake wakati anarudi Manchester United na mapungufu yaliyopo kwenye klabu ambayo amekuwa akitamani kuona mabadiliko lakini anaona hakuna mabadiliko yoyote hadi sasa.
Sikubaliani na baadhi ya mienendo yake iliyochangia kuwa anawekwa benchi lakini pia tuangalie upande mwingine wa shilingi.
Anayoyasema Cristiano Ronaldo kuwepo ndani ya klabu ni ya ukweli? Na kama ni ya ukweli, klabu inachukua hatua gani kuweza kubadilika na kuendana na mifumo ya kisasa?
Mpaka sasa hakuna mchambuzi, au mchezaji, wa zamani wa Manchester United miongoni mwa waliokuwa wanaongoza kumsema CR7 wametoa suluhu ya nini kifanyike ili klabu iweze kusonga mbele, wao mdomo na lawama tu.
Hadi sasa ninapoandika hivi kuna uzushi mwingi ambao umeanza kusambaa mitandaoni na nukuu za uongo ambazo hata hajazisema lakini watu wameanza kuzisambaza na lawama kibao juu ya mchezaji huyo mwenye historia kubwa na aliyeweka alama katika tasnia ya mpira wa miguu.
Maneno yanazungumzwa mengi kuwa amekosa “weledi” ndiyo maana amesema hivyo na hakutakiwa. Hivi nikuulizeni swali moja, asiposema mmoja wapo nani atakuja kusema?
Kuna muda mtu mmoja kujitoa kusemea kitu fulani inaweza kuwa chanzo cha kuokoa majanga mengi zaidi.
Ni bora zaidi kujadili hoja na kutafuta utatuzi kuliko kuanza kumshambulia mtu aliyetoa hoja na kutoa ya moyoni.
Hiyo ndiyo namna pekee tutaweza kusonga mbele kama tunahitaji kupata mabadiliko kwenye kila kitu.
Jalilu Zaid amejitambulisha kama mfuatiliaji na mchambuzi wa mchezo wa mpira wa miguu. Unaweza kumpata kupitia jaliluzaid@gmail.com au kupitia Twitter kama @jaliluzaid. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Hoja nzuri.
Hivi Ferguson hajalitilea neno lolote hizi hoja za ronaldo