Kauli ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally kwamba ipo haja kwa wakulima wadogo nchini kuungana dhidi ya wanaowadhulumu imeendelea kuzua gumzo na hivyo kuifanya iendelee kuishi.
Tutakumbuka kwamba akiwa huko Morogoro, wakati wa kongamano lililoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) kujadili mustakabali wa wakulima wadogo, Dk Ally alitoa kauli iliyogusa hisia za watu wengi kwa namna tofauti.
Pengine kilichowauma zaidi watu, hususan makada wenzake ndani ya CCM, ni onyo la Bashiru, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo, kwa wakulima wadogo nchini dhidi ya kuungana na wimbo wa “Mama anaupiga mwingi.”
Kauli ya “Mama anaupiga mwingi,” nadhani utakuwa unafahamu, hutumiwa na watu wanaoamini kwamba Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi nzuri kama kiongozi wa nchi na hivyo anastahili kumwagiwa sifa.
“MVIWATA, mkifika hatua za kusema lugha za mnaupiga mwingi, uhai wenu upo mashakani,” Bashiru alisema kwenye kongamano hilo lililofanyika Novemba 18, 2022. “Kwa sababu, [MVIWATA] siyo chombo cha kusifu, siyo chombo cha kushukuru.”
Kauli hiyo iliwatoa vigogo kadhaa wa CCM mafichoni na kumtaka Bashiru aombe radhi, wakibainisha kwamba hakuna ubaya kwa wakulima kusema “Mama anaupiga mwingi,” kama wanashawika huo ndiyo ukweli wa mambo ulivyo.
Kigogo wa hivi karibuni kabisa kumkosoa Bashiru hadharani ni Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Yusuf Makamba ambaye, akiongea kwenye mkutano wa hivi karibuni wa chama hicho huko Dodoma, alimshangaa Bashiru kuwataka wakulima wasiseme “Mama anaupiga mwingi.”
“Kuupiga mwingi maana yake ni mtu aliyefanya kazi nyingi na kubwa,” Makamba alizungumza kwenye mkutano huo wa CCM, mbele ya Rais Samia. “[Bashiru,] wenzako wakiamua kusema ‘Mama anaupiga mwingi’ tatizo inakuwa ni nini?”
Bashiru amekosea?
Lakini hebu tujiulize, ni kweli kwamba Bashiru, aliyetaka wakulima wadogo nchini kuunganisha nguvu kupambana na watu wanaowadhulumu, ambao mara nyingi huungwa mkono na watu walioko kwenye nyadhifa za uongozi, amekosea kuwatahadharisha wakulima wadogo nchini dhidi ya kauli ya “Mama anaupiga mwingi”?
Ukweli ni kwamba wakulima wadogo kwenye nchi hii wanapitia changamoto lukuki kiasi ya kwamba haiyumkiniki kwao kuongeza sauti za kusifu badala ya kuitaka Serikali ifanye zaidi katika kuboresha ustawi wao.
SOMA ZAIDI: Migogoro Isiyokwisha Kilosa Yawasukuma Wakulima Kutafuta Kikao na Majaliwa
Moja kati ya changamoto hizi, na ambayo ndiyo ilikuwa msingi wa hoja ya Dk Bashiru Ally, ni wimbi la uporwaji holela wa ardhi za wakulima wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, unaofanywa kwa kisingizio cha “uwekezaji” na ukiwa na baraka tele za viongozi wa Serikali wa maeneo husika.
Kimsingi, malalamiko haya yalitawala mkutano huo wa siku mbili wa MVIWATA ambapo wakulima wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi walilamikia kuporwa ardhi zao, huku viongozi wa Serikali kwenye maeneo yao wakishindwa kuwapa msaada stahiki.
“Matarajio yangu ni kwamba mshikamano wenu [wakulima wadogo] uweze kufikisha ujumbe kwa hao wanaotuongoza,” Bashiru aliwaambia wakulima wadogo baada ya kusikia vilio vyao. “Kauli zenu na misimamo yenu iwatishe ili wawe upande wenu.”
Hili la viongozi wa Serikali kushindwa kusimama na wakulima wadogo ni suala ambalo hata Rais Samia mwenyewe analitambua na kwenda mbali zaidi hata kwa kuwashutumu wasaidizi wake katika ngazi za wilaya kuchochea migogoro ya ardhi.
SOMA ZAIDI: Ushirika na Ustawi wa Wakulima Wadogo Tanzania: Hadithi ya Kufurahisha, Kuhuzunisha
Mnamo Aprili 6, 2021, kwa mfano, Rais Samia alitoa maagizo kwa watendaji wa Serikali, akisema:
“Watu wengi wameporwa ardhi zao [kwenye nchi hii], na waliofanikisha uporwaji wa ardhi ni maofisa wa ardhi. Nendeni mkalisimamie hili. Mkawasimamie watu wa wilayani, huko ndiyo kuna dhuluma kubwa.”
Kama hii ndiyo kauli ya Kiongozi Mkuu wa Nchi, kosa la Bashiru kuwataka wakulima wadogo waunganishe nguvu kupambana na wanyonyaji na waporaji wa ardhi zao, wenye baraka za viongozi wa Serikali, liko wapi?
Ardhi kuwa bidhaa
Na kusema ukweli, malalamiko ya uporwaji wa ardhi yana msingi wake kwenye uamuzi tuliouchukua kama nchi wa kuifanya ardhi kuwa bidhaa kama zilivyo bidhaa nyengine badala ya kuwa sehemu muhimu ya uhai wa binadamu, kama Azimio la Arusha, lililouliwa na CCM wenyewe, lilivyokuwa limekusudia.
Ukiniuliza mimi, malalamiko mengi yanayohusiana na wakulima wadogo nchini Tanzania yana msingi wake kwenye uamuzi huo wa hatari tuliouchukua kama nchi, iwe ni kwa wakulima wa Kilosa kulalamikia kuporwa ardhi zao au wakulima wa Mtwara kulalamikia bei mbovu ya korosho zao.
Na huu ndiyo muktadha ambao kauli ya Bashiru imetolewa, kwamba hali itaendelea kubaki hivi hivi kwa wakulima wadogo endapo kama hawataungana na kuhitaji Serikali yao ifanye zaidi ya kile inachokifanya sasa katika kulinda na kutetea haki zao.
Ushauri wangu ni kwamba watu waache kuvamia hoja wakiwa na hisia na badala yake watulize bongo zao inapokuja mijadala nyeti inayogusa maslahi mapana ya kitaifa kama ile inayohusu ardhi na hatma ya wakulima wadogo nchini Tanzania.
Kwa maneno mengine, tuache kujadili watu na badala yake tujadili hoja wanazoweka mezani.
SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Ajenda Kuu ya Wakulima Wadogo Wanawake Barani Afrika
Pengine tungetumia muda kujadili hoja ya Bashiru, badala ya kumjadili yeye kama mtu, tungeona ni kwa namna gani jitihada za makusudi zinahitajika kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.
Labda tungejadili tunafanya nini kukifanya kilimo, kinachoajiri watu wengi zaidi Tanzania, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kiwe na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa ambao kwa sasa unakisiwa kuwa siyo zaidi ya asilimia 30.
Rai yangu, nikiwa namalizia safu hii, ni kwamba tujadili hoja ya Bashiru kwa kuipa uzito wake unaostahiki na iwe sehemu ya tafakuri zetu juu ya hali ya kilimo chetu na hatma ya wakulima wadogo hapa nchini.
Tupo wapi? Tunafanya nini? Na tunaelekea wapi? Ni maswali muhimu ambayo nadhani yanahitaji tafakuri jadidifu kutoka kwetu sote.
Nassoro Kitunda ni mhadhiri msaidizi wa sosholojia, Mwenge Catholic University. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.
One Response
Dak Bashiru hakukosea kutoa maoni yake. CCM kama chama cha kidemokrasia ni lazima kiruhusu maoni ya wanachama yanayokinzana na ya wakuu
Wanaomlaani Bashiru ni walamba asali na waganga tumbo