The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

A-Z Sakata la Twiga Kuchukua Umiliki wa Tanga Cement na Ukinzani Unaombatana na Hatua Hiyo

Tume ya Ushindani yadaiwa kuendelea na zoezi hilo licha ya Mahakama ya Ushindani kuagiza zoezi hilo lisimame.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na fukuto likiendelea likizihusisha kampuni kubwa mbili za uzalishaji wa saruji hapa nchini, kampuni ya Twiga Cement na ile ya Tanga Cement lakini pia kuna mamlaka za kiserikali zimekuwa zikihusika humo ndani, ikiwemo Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) lakini pia Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara (FCT).

Sakata lenyewe linahusiana na mpango wa kampuni ya Twiga, au kampuni inayozalisha Twiga Cement, kutaka kuimiliki, au kwa Kiingereza wanasema ku-acquire, kampuni inayozalisha, au hisa asilimia 60 na kitu, za kampuni inayozalisha saruji ya Tanga Cement.

Mpango huu, hata hivyo, umeibua mashaka na wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya watu, zikiwemo kampuni nyingine zinazozalisha saruji, kama vile Chalinze Cement. Pia, Chama Cha Walaji Tanzania kiliingilia kati nacho kikawa kinapinga uamuzi huo kufanyika.

Lakini pia kuna watu binafsi ambao wao baada ya kufuatilia na kuona kinachoendelea wakaona kwamba hiki ni kitu ambacho hakipaswi kuendelea. Na moja kati ya watu hao ni Peter Hellar.

Hellar ni mwanasheria lakini pia ni mwananchi wa kawaida na mlaji na mtumiaji wa saruji. Kwa hiyo, na yeye akaamua kama kuongeza nguvu kwenye hili vuguvugu la huu mchakato wa kuzuia kampuni ya Twiga isiimiliki kampuni ya Tanga Cement.

The Chanzo ilifanya mahojiano maalum na Hellar kufahamu kwa nini aliamua kuchukua hatua hiyo na ni hatua gani aliichukua, mchakato kwa sasa unaendeleaje na kwa nini hili jambo linahusu maslahi mapana ya taifa na kwa nini kila mwananchi anapaswa alifuatilie. Hapa Hellar anaanza kwa kujitambulisha:

Peter Hellar: Kwa kifupi tu Peter Hellar ni raia, kama raia mwengine yeyote. Pia, kwa kitaaluma, mimi ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea, na ni mfanyabiashara pia.

Ukiongelea kuhusu suala lilipo mbele yetu, kikatiba, kama mwananchi, na pia kwa dhumuni la uanzishwaji wa Sheria ya Ushindani, inanipa haki pale ninapoona maslahi makubwa yanaweza yakawa kwenye shaka, napata haki ya kuweza kuingia kwenye suala kama hili ambalo liko mbele yetu.

Na ndiyo haswa nilichokifanya. Siyo mimi tu, naamini kuna watu wengine washaingilia kabla hata ya huo mchakato haujafanyika kwa sababu wanapata haki hiyo kikatiba na kisheria ya ushindani.

The Chanzo: Labda pengine kwa mtu ambaye hajui, labda kwa kifupi, unaweza kutupa background, au kwa Kiswahili wanaita usuli, yaani suala haswa ni nini, nini kinaendelea?

Peter Hellar: Kwa kifupi, Tanga Cement ni kampuni ambayo inazalisha saruji ya Tanga na Twiga Cement pia inazalisha saruji ya Twiga ambayo Twiga Cement inamilikiwa na kampuni inaitwa Scankem Internatinal DA, ni [kampuni] ya [Kijerumani], nadhani, hawa ni watu wakubwa kwenye soko la saruji.

Ni soko ambalo ni muhimu kwa sababu saruji ina matumizi makubwa mno kwa wananchi wa kawaida lakini na jamii. Ukianzia kujenga barabara, [na] majengo. Kwa hiyo, ni bidhaa ambayo ina umuhimu wa kitaifa.

Scankem Internatinal DA ambao ndiyo wamiliki wa Twiga Cement walitaka kununua hisa za Tanga Cement, hisa asilimia 30 – 69 za Tanga Cement.

 

Na kwa mujibu wa sheria, kutokana na matakwa ya Sheria ya Ushindani, walifanya hivyo kupitia Tume ya Ushindani ambayo ndiyo ina mamlaka haswa ya kusimamia, kwa Kiingereza tunaita mergers and acquisitions, yaani ni mfumo wa kampuni moja kuchukua umiliki wa kampuni nyingine.

Na kuna sheria ambayo imeweka wazi kwamba mergers and acquisitions ikiwa yenye thamani fulani ni lazima upitie huko. Kwa hiyo, walifuata taratibu zote za kisheria kupitia Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC). [FCC] walifanya tararibu zote za kuchunguza iwapo hii mergers and acquisitions ikifanyika haitakuwa na athari kwa watumiaji.

Na athari kwamba Twiga Cement akiimiliki Tanga Cement hatakuwa na monopoly, yaani ukiritimba, kwa mujibu wa sheria kwa sababu sheria inazuia mtu mmoja kuwa na nguvu kubwa kwenye soko ambalo anaweza tawala upangaji wa bei ya bidhaa.

Kwa hapa tunaongelea kama saruji na akiweza anaweza kuifanya ikawa juu [kwa bei] na ikamuathiri mwananchi au mtumiaji.

Na hili ndiyo ilikuwa sababu kubwa hata ya Chama cha Walaji nao kuingilia kati suala hili, Twiga Cement kwa mara ya kwanza alipotaka kuichukua Tanga Cement.

FCC ilifanya kazi yake na ikaona kwamba Twiga Cement akiimiliki Tanga Cement kwenye soko atakuwa na asilimia 68 ambayo inavuka kizingiti kilichowekwa.

FCC iligundua hilo kwa sababu ukipeleka maombi yako kwamba unataka kufanya mergers and acquisitions wao wanafanya uchunguzi kwamba itakuwaje hiki kikitokea, kwenye soko itakuwaje.

Kwa hiyo, ripoti yao ya kiuchunguzi ilionesha kwamba iwapo Twiga Cement ataimiliki Tanga Cement atakuwa na asilimia 68 kwenye soko. Kizingiti kilichopangwa na sheria, ukomo wa asilimia ambazo mtu mmoja anapaswa kuwa nazo, ni asilimia 34 [ya soko].

Kwa hiyo, angekwenda kuwa na asilimia 68 ambazo ni nyingi, angekuwa na nguvu ambayo ingeweza kumsababishia akapanga bei kwa atakavyo yeye.

Na hii ina athari kwa walaji, kwa watumiaji, ambao sasa akiamua iwe bei ya juu ingeweza kuwa bei ya juu, kwa sababu ni yeye ndiyo anahisa kubwa kwenye soko.

Kwa hiyo, kwa uchunguzi wao, [FCC] wakaona kwamba [Twiga] atafikia asilimia 68, walitaka kuendelea na hivyo lakini kukawa na muingiliano kati ya Chama cha Walaji kwa mujibu wa sheria na wazalishaji wengine wa saruji kama Chalinze Cement na watu wengine.

Wakaenda Mahakama ya Ushindani wakiomba zuio hiki kitu kisifanyike kwa sababu kitakuwa na athari kwa wazalishaji wa saruji na kwa walaji. Na Mahakama ya Ushindani ikasikiliza maombi hayo na kuyajumuisha kwa pamoja na kuyatolea maamuzi.

Maamuzi yao ni kwamba kutokana na matokeo na kutokana na walichokigundua Tume ya Ushindani, kwamba iwapo Twiga Cement ataimiliki Tanga Cement atakuwa na hisa kwenye ya asilimia 68 kwenye soko, ambayo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa cha asilimia 34, kwa hiyo, hiki kitu kisingeweza kufanyika, si kinavyotakiwa kufanyika.

Na [Mahakama] ikatoa hukumu, Mahakama ya Ushindani, kwamba lile suala la maombi ya Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement limezuiwa. Hiyo ni hukumu iliyotolewa mwaka jana [2022] na ilitolewa na Mahakama ya Ushindani kwamba haya maombi [ya] Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement yamezuiwa.

Na hukumu ilikuwa wazi kabisa kwamba maombi yamezuiliwa, kwamba [hili jambo] lisiendelee na ilikuwa ni kwa manufaa ya jamii kwa mujibu wa sheria kwamba likitokea hivyo Twiga Cement atakuwa na nguvu kubwa kwenye soko.

Kwa hiyo, Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara ikatoa zuio na iko wazi kwamba hii Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara imeanzishwa kwa sheria ya Bunge, ni Mahakama kama Mahakama nyingine, na imeanzishwa kwa mujibu wa sheria, inapaswa kuheshimiwa, maamuzi yake yanapaswa kuheshimiwa na ni maamuzi ambayo yanalinda maslahi ya umma.

Maslahi ya jamii kwa ujumla, wazalishaji wa saruji, watumiaji wa saruji kwa mtazamo huu tunaouogolea. Kwa hiyo, Mahakama ilitoa hukumu iliyozuia huu mpango wa Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement. Suala likawa limeisha pale na ilisema kabisa hili suala limezuiliwa, haliwezi kuendelea.

Lakini, cha kushangaza, mwezi Februari mwaka huu [2023] kupitia gazeti la Daily News likatokea tena tangazo lililotolewa na Tume ya Ushindani kwamba Twiga Cement anataka tena kuimiliki Tanga Cement.

Na akataka kuchukua hisa zilezile, asilimia zilezile 69, kila kitu ni kilekile kama kilivyokuwa mara ya kwanza. Na anajua kulikuwa na wadau walikwenda kupinga kwenye kamisheni kule, lakini ikatupiliwa mbali na wengine wakaenda tena kwenye Mahakama ya Ushindani wa biashara kuomba zuio kitu hiki kupinga kinachoendelea kufanyika.

Suala bado liko kwenye Mahakama ya Biashara, kuna watu tofauti ambao wamefungua shauri, nikiwemo mimi, mimi Peter Hellar, kama raia, kama mtumiaji wa saruji, ninayepata haki ya kikatiba na kisheria ninapoona maslahi yangu yanaweza yakaathirika, nina uhuru na haki ya kufanya hivyo.

Kwa hiyo, mimi ni mmoja wa watu waliofungua shauri Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara nikipinga tena suala la Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement.

Kinachonishanga hizi zote ni mamlaka zilizoanzishwa na sheria ya Bunge, Mahakama za kiserikali mahususi kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi na watumiaji na walaji.

Hakuna kitu ambacho hata kwenye tangazo la Februari 13, [2023] lililowekwa pale na Tume ya Ushindani (FCC) la Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement hawaelezei kama kuna mabadiliko yoyote ambayo yamefanyika kwenye soko ambayo, pengine, yangeweza kuwasababishia Twiga Cement sasa kuwa na uwezo wa kuimiliki Tanga Cement.

Ninavyoongelea mabadiliko namanisha kwamba, pengine, kuna wazalishaji zaidi wametokea kwenye soko [au], pengine, akiichukua sasa hizi asilimia hazitafika huko. Hakuna hayo mabadiliko, hakuna mabadiliko kama hayo.

Lakini wakaendelea kuweka tangazo na watu waliokwenda kupinga kule kamisheni maamuzi yalikuwa ni ya kutupilia mbali ndiyo maana watu wamekwenda tena kwenye Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara.

Kitu kikubwa zaidi ninachokiona ni kudharau maamuzi ya Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara ambayo yaliweka zuio, kwamba imezuiwa kwa hili suala kufanyika. Na naamini wanaofanya hili wanaupeo na uelewa mkubwa wa sheria.

Wangekuwa na uwezo kama wangekuwa wanafanya kitu wanachodhani ni sahihi wa kurudi kwenye Mahakama ya Ushindani wa Biashara na kuomba marejeo ya ile hukumu kwa kuridhia kuna mabadiliko kwenye soko na Mahakama ingeweza ikapitia na ingeweza ikabadilisha maamuzi yake.

Lakini nadhani kabisa mahususi kwa kujua kwamba hakuna mabadiliko yoyote wametaka kufanya kitu kwa kinyume kabisa na sheria, siyo kinyume tu na sheria, na kudharau maamuzi ya Mahakama, kitu ambacho ni kitu kibaya.

Hizi Mahakama zimewekwa kwa ajili ya kuheshimiwa, zinapotoa maamuzi ya haki ni maamuzi yanayolinda haki ya watu binafsi na maslahi ya umma pia.

Sasa sidhani hawa Scankem Internatinal DA wangeweza kufanya hiki kitu kama kingekuwa kinatokea kwenye nchi kama ya Kijerumani, kungekuwa kuna maamuzi ya Mahakama kama haya kama wangeweza kufanyia dharau na kebehi kama wanavyofanya hapa.

Kwa hiyo, ni kitu cha kustaajabisha lakini siwashangai wao. Naishangaa Tume ya Ushindani kwa sababu iko wazi kabisa wanaona haya maamuzi na wanajua.

Kwa kutaka kuendelea inanipa hofu ni wanafanya kwa maslahi gani kwa kitu ambacho kimeshatolewa maamuzi ya kimahakama, wao wanaendelea kutaka kupingana na maamuzi ya Mahakama ya Ushindani kwa maslahi yapi?

The Chanzo: Kwa hiyo, baada ya hatua hiyo ya Tume ya Ushindani ndiyo wewe ukafungua tena shauri?

Peter Hellar: Nimefungua shauri Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara, nikiomba wazuie kitu ambacho kinataka kufanywa, muunganiko kati ya Twiga Cement na Tanga Cement kama ilivyoombwa kupitia gazeti la Daily News la tarehe 13, Februari.

Ninapinga kwa kuzingatia maamuzi ambayo yalishatolewa na Mahakama ya mwaka jana [2022] na nikipinga nikiona utaratibu ambao unataka kutumika unakinzana na maamuzi ya kimahakama na unakinzana na utaratibu wa sheria.

The Chanzo: Na hukumu ambayo ndiyo imetoka, si ndiyo ya Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara?

Peter Hellar: Hukumu imetoka toka mwaka jana. Saa hizi kuna maombi mbalimbali. Kuna maombi ya kimsingi ambayo yanaomba hilo suala lisifanyike ambayo pia inataka kuwahoji.

Mimi nataka kuwahoji waliopeleka haya maombi kutaka muunganiko mwengine wa Twiga Cement na Tanga Cement. Kwa nini wasiletwe mbele ya Mahakama kwa kudharau hukumu ya Mahakama kwa ajili ya kufanya hivyo?

The Chanzo: Hii iliyotolewa Machi 24, [2023] ni nini?

Peter Haller: Hilo ni zuio la muda.

The Chanzo: Yaani ni kama vile Mahakama imerudia msimamo wao.

Peter Hellar: Imezuia kwa kuzingatia maombi ya msingi ambayo bado hayajasikilizwa. Kwa hiyo, hayo ni maombi madogo ya kwamba kinachotaka kufanyika kisifanyike kwanza.

Kuna maombi ya msingi, maombi ya msingi yanaomba huo muungano usifanyika lakini pia maombi ya msingi yanaomba Kamisheni ya Ushindani wa Kibiashara, ikiongozwa na Mkurugenzi wao Mkuu, Mkurugenzi wa Scankem Internatinal DA, ambaye ndiye mmiliki wa Twiga Cement na mawakili wengine ambao walikuwa kwenye maamuzi ya kwanza, kwa nini wasiitwe mbele ya Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara na wakachukuliwa hatua zaidi kwa kudharau maamuzi ya Mahakama?

Kwa hiyo, madogo yaliyotoka na kuzuia hiki kitu kuweza kufanyika, isifanyike kwanza mpaka hayo maombi ya msingi yatakapo sikilizwa.

The Chanzo: Kwenye hii ya Machi 24, huyu Jaji aliyetoa huu uuamuzi anasema kwamba wameshangazwa na huo uumuzi. Unadhani nini kiliwapa kujiamini hao FCC?

Peter Haller: Nisingependa sana kuongelea maamuzi madogo taliyotolewa hapo kwa sababu hili suala bado lipo mahakamani. Mimi ni mwanasheria kwa taaluma yangu naamini suala lililopo mahakamani sitaongelea sana masuala ya kimahakama.

Lakini nitaongea tu kwamba hilo ni zuio walilolitoa, kisiendelee kinachotaka kufanyika.

Na ni zuio walilolitoa na kama ulivyoongea kwamba wameshangazwa kwa sababu maamuzi yaliyotolewa ni yeye mwenyewe Mheshima Jaji Salma Maghimbi aliyeyatoa na anaelewa msingi wa kuyatoa.

Na anashangaa kwa sababu anaamini aliyatoa mbele yao wote, kwa hiyo, anashangaa ni vipi wamekwenda kurudia kilekile kitu ambacho kimezuiliwa na Mahakama. Ni kitu cha kushangaza!

The Chanzo: Wewe ni nini, binafsi, kilikusukuma?

Peter Hellar: Kwa kifupi tu mimi ni mwananchi, ni mlaji na mtumiaji wa saruji na sheria inanipa haki. Kwanza, nina haki ya kikatiba na haki ya kisheria iliyoanzisha hiki chombo cha FCC, kwamba nikiona maslahi yangu yanaweza kuathirika na mimi naweza kuomba kuingilia kwenye kitu ambacho kitanataka kufanyika.

Kwa hiyo, na mimi nimetumia haki yangu kikatiba na kisheria kwenye kuingilia kama mtumiaji [wa] saruji na kama mfanyabiashara pia ili kuzuia kile ambacho kinataka kufanyika kwa sababu nina haki kwa mujibu wa sheria.

The Chanzo: Unadhani hiki kinachoendelea ni muhimu kiasi gani, na unadhani kikipita mwananchi wa kawaida anaenda kuathirika kwa namna gani?

Peter Hellar: Kina umuhimu mkubwa sana, pengine nadhani jamii haijapata uelewa tu kwa kinachofanyika. Niliona tu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara wa ACT Wazalendo [Halima Nabalang’anya] akishangaa kinachofanyika kwamba kinaweza kutokea.

Lakini naamini ni kitu ambacho kilitakiwa kupigiwe kelele zaidi na mamlaka tofauti, ikiwemo Bunge kwa sababu sheria ilipitishwa kwa ajili ya kuwalinda walaji.

Kuwalinda walaji, tunapoongelea hii ni saruji, lakini tunapoongelea kila siku mfumuko wa bei ni vinaenda kuathiri moja kwa moja wananchi, vina athari sana kwenye uchumi.

Utakapokuwa na mtu moja anamiliki asilimia 34 kama sheria inavyosema anakwenda kuwa na asilimia 68 kwenye uzalishaji atakuwa na uwezo wa kupanga bei ya saruji anavyotaka kwa sababu yeye ndiyo mwenye nguvu sokoni.

Na sheria ilitaka kuzuia hivyo ili kusudi kuwalinda watumiaji na kuwalinda wazalishaji wengine pengine.

Kwa hiyo, tunapoongelea tafakari ya vitu kama hivyo ndiyo madhara yake hayo. Kwa hiyo, ni suala ambalo lilitakiwa kupigiwa kelele pengine uelewa wa umma, siwezi kusema kuwa ni mdogo, lakini ni suala ambalo watu wenye uelewa walitakiwa walipigie kelele. Kwa sababu linaenda kuwa na madhara makubwa kwenye soko.

The Chanzo: Na hii inakuambia nini wewe kama mlaji, hususan linapokuja suala la mamlaka za Serikali zilizowekwa kisheria kulinda maslahi ya mlaji, unadhani mlaji wa Kitanzania analindwa kwa kiasi gani, taasisi za Kitanzania zinamlinda mlaji wa kiasi gani?

Peter Haller: Sheria ziko wazi, zimewekwa na zinafanya kazi vizuri, ndiyo maana tumeona kuna suala la uendeshaji mzuri, kwa sababu ya sheria. Havitokei hivi vitu mara kwa mara na vinapotokea tunapaswa kupaza sauti.

Kwa hiyo, sheria kwa kweli iko sawasawa na ndiyo maana tunatumia sheria hiyohiyo kujaribu kulinda maslahi ya walaji.

Naamini na Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara inafanya kazi vizuri. Kinachonishangaza ni kwamba FCC, ambayo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza inapaswa kufanya uchunguzi na kuona hiki kitu kinapaswa kuendelea, yenyewe ndiyo imetaka kuendelea kukifanya hiki kitu ambacho kipo kinyume na sheria.

Hapo ndiyo napata hofu na sisi kama walaji, kwa sababu tuna haki ya kisheria, ndiyo maana tumeingia na kwenda kuomba zuio kinachotaka kufanyika kisifanyike kwa maslahi mapana ya walaji na nchi kwa ujumla.

The Chanzo: Kinachofata sasa ni nini?

Peter Haller: Kinachofuata kuna maombi ya msingi ambavyo yako mbele ya Mahakama, nayaongelea ya kwangu binafsi, najua kuna watu wengine pia wameomba, yatasikilizwa.

Maombi binafsi ni kwamba yanataka wale wanaoendelea na huu mchakato waitwe mbele ya Mahakama, wahojiwe kwa nini wasichukuliwe hatua zaidi kwa kufanya kitu kilichozuiwa na Mahakama.

Kwa sababu hukumu ya mwaka jana ya Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara iko wazi, ilisema imeizuia Twiga Cement kuimiliki Tanga Cement. Kwa hiyo, tumeomba wachukuliwe hatua zaidi za kisheria, isifanyike.

Kikubwa ambacho tumekiona ni kwamba Tume ya Ushindani kwa kufuata mchakato huo ikiendelea inaweza isiendele bila ya kujulisha umma kwa sababu sheria haitaki, haiwapi wajibu wakuwajulisha umma kwamba tumeshapitisha hii mergers and acquisitions kwa hiyo wanaweza kufanya kimya kimya.

Kwa hiyo, inaweza ikafanya kimya kimya. Athari zitakuja kuonekana baadaye, lakini kwa kuwa sisi tulioona hilo tangazo, tukaomba zuiyo na tukaona wanaendelea ndiyo maana, kama mimi, nimeona kuomba zuio la kinachofanyika kisiendelee kufanyika.

The Chanzo: Kaka Peter, mimi ninakushukuru sana. Ilikuwa ni muda mzuri wa kuzungumza na wewe kuhusiana na hili jambo ambalo limekuwa likiendelea lakini hatuoni mijadala mingi sana ikiendelea kulihusu. Labda neno lako la mwisho, labda pengine kama una wito.

Peter Hellar: Mimi wito wangu ni kwamba mamlaka husika, hususani Mahakama za Kiserikali kama FCC, ambao ndiyo wana wajibu wa kwanza wa kusimamia sheria, wajaribu kusimamia sheria kwa matakwa na maslahi mapana yaliyowekwa kwenye sheria ambayo ni maslahi ya umma na maslahi ya wananchi.

Pia, maslahi ya wananchi ni hata hao wanaoomba wenyewe wasimamie sheria ipasavyo kwa sababu wakisimamia sheria ipasavyo hiki kinachoendelea kisingeendelea. Ni aibu kwa mamlaka mbili za Serikali kukinzana moja kuidharau nyingine. Haipaswi.

The Chanzo: Unaamanisha Tume ya Ushindani (FCC) na Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara (FCT)?

Peter Hellar: Tume ya Ushindani (FCC) kudharau maamuzi ya Mahakama ya Ushindani wa Kibiashara (FCT) ambacho ni chombo cha haki. Ni suala ambalo ni aibu kwa nchi ambayo inajinasibu kufuata matakwa ya sheria, siyo kitu ambacho kinapaswa kuendelea!

Mahojiano haya yalibadilishwa kutoka sauti kuwa maneno na Najjat Omar na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamis amesimamia uzalishaji wa mahojiano haya. Kwa mrejesho kuhusu mahojiano haya, tuandikie: editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Hii sheria mbna kama ya kizee hivi,
    Waache soko huria mtu akitaka kununua viwanda vyote anunue, iwe kazi kwa Chalinze cement, Dangote et al kufanya kazi kuwashusha Twiga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *