Songwe. Wananchi kutoka vijiji vya Rukwa na Udinde vinavyounda kata ya Udinde mkoani Songwe wameiomba Serikali iwajengee daraja litakaloviunganisha vijiji hivyo vinavyotenganishwa na Mto Kikamba ili kuepuka kushambuliwa na mamba pale wananchi hao wanapovuka mto huo kwa shughuli zao mbalimbali.
Hatua hiyo inakuja huku kukiwa na matukio kadhaa ya wanavijiji kuliwa na kujeruhiwa na mamba wanapojaribu kuvuka mto huo ambapo mara nyingi hufanya hivyo kwa kutumia ngarawa zilizothibitika kutokuwa salama kwa watumiaje wake.
Kilio hicho cha siku nyingi cha wanavijiji hao kiliibuliwa upya hivi karibuni kufuatia kifo cha mtoto wa miaka tisa, Ivan Vedastus Ntapanya, ambaye aliliwa na mamba mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili alipojaribu kuvuka mto huo kwa ajili ya kwenda kuchuma maembe upande wa pili, kwenye kijiji cha Rukwa.
Kifo cha mtoto huyo aliyekuwa akisoma Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Udinde kimeibua hisia kali miongoni mwa wanakijiji, kikiwakumbusha matukio kama hayo yaliyowahi kutokea huko nyuma na vilio vyao ambavyo wanadhani vimeendelea kupuuzwa na Serikali.
Vedastus Ntapanya, baba wa mtoto aliyeliwa na mamba, aliiambia The Chanzo kwamba aliipokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa sana, akibainisha kwamba ingekuwa ngumu kwa kijana wake kuliwa na mamba kama kungekuwa na daraja mtoni hapo.
“Hili ziwa lina mamba wengi sana, kwa sababu ukiangalia hata vivuko hapo utakuta watu wanavuka kwa kutumia ngarawa, kama maji yamepungua wanavuka maji ya kiunoni, lakini mamba lazima akufanyie tukio,” alisema.
“Kwa hiyo, sisi tunaomba Serikali ituwekee daraja hata la kuvuka kwa miguu lakini siyo utaratibu huu tunaotumia kwa sasa,” Ntapanya, 48, aliongeza. “Ni hatarishi sana, hususan sasa hivi tuna shule hapa watoto wa [kijiji cha] Rukwa wanakuja kusoma hapa.”
Wanakijiji wa Udinde wanaamini kuwa kujengwa kwa daraja katika Mto Kikamba kutarahisisha wanafunzi kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Philipo Mulugo, shule mpya ya kata.
Pia, daraja hilo litasaidia kusafirisha mazao ambapo kijiji cha Rukwa kinasifika kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.
Akiongea na The Chanzo, Diwani wa Kata ya Udinde Paschal Kapungu amefananisha kilio cha wananchi wa kata hiyo wapatao 16,000 na kilio cha samaki kwenye maji kutokana na machozi yake kutopatiwa majibu.
“Sasa hivi tunajifananisha na samaki, maana tunalia leo, tunanyamaza, kesho tenatunalia lakini bado hatusaidiwi, machozi yetu yanaishia kwenye maji,” alisema Kapungu.
Kapungu ameeleza kwamba pamoja na juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika katika kudhibiti eneo hilo kwa kuweka vivuko vya muda, bado vimekuwa siyo tiba ya kudumu kutokana na mto huo kuwa mpana ambao unahitaji matengenezo makubwa.
“Ndiyo jitihada zipo za Mbunge kutusemea bungeni na wilaya kuweka vivuko lakini bado havina msaada,” alilalamika Kapungu. “Sisi tunaonekana kama watoto yatima. Serikali kama ambavyo huwa inawasikiliza wengine wakilia, itusikilize na sisi. Ichukue hatua za haraka kwa wana-Udinde maana hatukuumbwa ili tuliwe na mamba.”
Tukio la mtoto Ivan kuliwa na mamba katika Mto Kikamba ni moja ya visa angalau vitano vilivyowahi kuripotiwa katika mto huo.
Thomas Bangu ni mkazi wa kijiji cha Udinde ambaye amehusisha kifo cha mtoto huyo na kutokuwepo kwa daraja, akisema kwamba watoto walienda kufua nguo ili wapate upenyo wa kwenda kuchuma maembe yaliyo ng’ambo ya Mto Kikamba.
“[Watoto] walikuja kufua ili wakachume maembe ng’ambo,” Bangu, 51, alisema. “Kwa hiyo, pangekuwa na daraja wangeenda kwenye maembe na wangerudi salama.”
Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Songwe Philipo Mulugo (Chama cha Mapinduzi – CCM), amesema jitihada zimekuwa zikichukuliwa lakini changamoto iliyopo ni kwamba Mto Kikamba umekuwa ukihama hama kila mwaka.
“Walikuja watu wa TARURA mwaka jana [2022] kupima, wanaendelea na usanifu na ujenzi wa daraja,” alisema Mulugo. “Bahati mbaya huu mto unahama. Kwa hiyo, ukipima hapa mwaka unaofuata unakuta umepasua mahala fulani. Kwa hiyo, unahama hama hivyo wanaendelea na usanifu.”
Asifiwe Mbembela ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini anayepatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.