Mbeya/Songwe. Wananchi wa Mbeya na Songwe wameiomba Serikali kuhakikisha inaviwezesha vituo vya afya vilivyojengwa hivi karibuni mikoani humo ili viweze kuwa na uwezo wa kutoa huduma stahiki kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Wananchi hao walikuwa wanazungumzia vituo vya afya vilivyojengwa kupitia tozo za miamala ya simu. Mkoani Mbeya, jumla ya vituo sita vya afya vilipaswa kujengwa ambavyo ni Kifunda, Itungi, Njisi, Kambikatoto, Ntokela-Ndato, Itagano, Swaya, na Mahongole.
Kwa upande wake, Songwe ilipaswa kujengewa vituo hivi sita, ambavyo ni Ngwala, Ndola, Mwakakati, Msangano, Hezya, na Nambizo.
Hata hivyo, The Chanzo imebaini kwamba kwenye vile vituo vya afya vilivyokamilika kwa takriban miezi mitano sasa katika mikoa yote miwili ya Songwe na Mbeya, hakuna kilichoanza kazi kwa kukosa vifaa muhimu na wataalamu.
Miongoni mwao ni Kituo cha Afya cha Ndola na Kituo cha Afya cha Lubanda, vinavyopatikana Ileje, mkoani Songwe. Kituo cha Afya Ngwala (Songwe); Kituo cha Afya Kambikatoto; Kituo cha Afya Sangambi; na Kituo cha Afya cha Ilemi, vyote vikipatikana Chunya, mkoani Mbeya.
Kusafiri umbali mrefu
Kwenye mahojiano yake na wakazi wa Ndola, wanaokadiriwa kufikia 7,340, The Chanzo ilielezwa ni kwa namna gani hali ya vituo hivyo kushindwa kufanya kazi inawaathiri wananchi wa kata hiyo, wakilalamikia kulazimika kutembelea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Mmoja kati ya wakazi hao ni Tabia Simbeye, mama wa watoto wanne aliyelalamikia wajawazito kulazimika kutembea umbali mrefu kwa njia ya usafiri wa pikipiki kufuata huduma za matibabu kwenye kituo cha afya cha jirani.
Wananchi wa Ndola kwa sasa wanalazimika kusafiri zaidi ya kilomita 60 kwenda na kurudi kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Itumba ambayo kwa miundombinu ya barabara imekuwa na changamoto hasa nyakati za mvua ambapo baadhi ya sehemu zimekuwa hazipitiki.
SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu
“Tunaomba tu kwamba tuwe tunatibiwa hapa [Ndola],” Tabia, 38, alisema. “Maana mjamzito kwenda na pikipiki Itumba ni mbali.”
Mwananchi mwengine wa Ndola, Sophia Mwamahonje, alisema kutokuwepo kwa kituo cha afya kwenye eneo hilo imekuwa mwiba kwa wazee, watoto na wajamzito ambao wanakwenda kijiji cha Ishenta kupata matibabu.
“Yani tunahangaika [na] watoto na sisi watu wazima kwenda Ishenta, kwenda Itumba, Shilingi 14,000 au Shilingi 15,000 kwa pikipiki kwenda na kurudi,” Mwamahonje alisema. “Sasa Itumba ni mbali. Tunaomba hapa hapa jamani watufungulie.”
Naye Solomon Pamu, mkazi wa kata ya Ngwala, ambayo watu wake hulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Songwe ama hospitali binafsi ya Mwambani, alisema Kituo cha Afya Ngwala kitaweza kuwasaidia wananchi kuacha kupata shida katika kusafiri kwenda umbali mrefu.
“Sasa tunapata shida kusafiri, tunasafiri kwa shida maana hata gari zenyewe hazina ubora, sasa chukulia mtu ni mgonjwa itakuwaje?” Pamu, 56, alisema. “Tunapigwa viwango vikubwa vya hela kwa sababu ni mbali. Lakini pia barabara yenyewe siyo nzuri.”
Diwani wa Ndola, Bahati Kyomo, ameiambia The Chanzo kuwa kila mara wamekuwa wakitoa ahadi kwa wananchi wao kwamba Kituo cha Afya kitafunguliwa lakini mwisho wa siku hatua hiyo haifikiwi.
SOMA ZAIDI: Wahama CCM Kisa Mradi wa Kituo cha Afya
“Kila muda ukiwauliza wataalamu wao wanakwambia tunafungua lakini hawatekelezi,” alilalamika mwakilishi huyo wa wananchi. “Kwa hiyo, naweza kusema hii inatokana na kutokuwepo kwa uwajibikaji.”
Serikali yakiri
Kufuatia malalamiko haya, The Chanzo ilimuuliza Mkurugenzi wa Afya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI Dk Ntuli Kapologwe endapo kama Serikali ina mpango wowote wa hivi karibuni kuviwezesha vituo hivyo kufanya kazi.
Kwenye mahojiano haya, Dk Kapologwe alikiri uwepo wa changamoto hiyo, akisema tatizo halipo kwenye vituo vya afya tu bali hata katika hospitali za wilaya kwenye wilaya ambazo zimeanzishwa karibuni.
Dk Kapologwe alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba vituo vyote vya afya takribani 250 vinavyotokana na tozo za miamala ya simu na vituo vya afya vingine 100 vinapatiwa vifaa na wahudumu ili viweze kuanza kazi.
“Mwaka huu wa fedha tumetenga Shilingi bilioni 34.1 kwa ajili ya kununua vifaa na vifaa tiba ikijumuisha na kuajiri watumishi wapya, hususan wataalamu kwenye maeneo ya mionzi, chumba cha kuhifadhia maiti, mabingwa wa huduma za upasuaji, na wataalamu wa kutoa dawa za usingizi ambao wanahitaji sana,” alisema.
Hata hivyo, Dk Kapologwe amewahimiza wasimamizi wa Serikali za Mitaa na mikoa kuhakikisha vifaa ambavyo vinafika katika vituo vya afya na hospitali vinaanza kufanya kazi kwa huduma za awali ili kuwapunguzia changamoto wananchi hata kwa huduma za awali.
“Tunafahamu hatuwezi kupata vifaa na wataalamu kwa wakati mmoja,” alisema. “Sasa viongozi wa wilaya na mikoa wanatakiwa kusimamia utaratibu wa kuanzisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa nje kulingana na namna ambavyo wamekuwa wakipokea vifaa tiba na wataalamu ambao wamekuwa wakiajiriwa.”
Asifiwe Mbembela ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka mkoa wa Mbeya na Songwe anapatikana kwa mbembelaasifiwe@gmail.com.