Mtwara. Tulitembea kwa boti umbali wa takribani kilomita nne kutoka upwa wa bahari uliopo kwenye Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma inayopatikana kwenye kijiji cha Ruvura, kata ya Msimbati, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, kwenda kuwaona wanyama aina ya nyangumi wanaopatikana hifadhini hapo.
Tulipofika tulianza kuona mawimbi makubwa ya maji mbele ya boti tuliyopanda. Haikuchukua muda tuliona nyangumi mkubwa akijirusha kutoka kwenye maji na kujipidua, kisha kuzama tena kwenye maji.
Inaelezwa kwamba kila mwaka kuanzia mwishoni mwa Julai, wanyama aina ya nyangumi hufika hifadhini hapa makundi kwa makundi wakitokea Bahari ya Kusini, yaani kwenye nchi za Afrika Kusini na Msumbiji, na kukaa kwenye hifadhi hii mpaka mwezi Novemba.
Wanyama hawa huwa na tabia ya kukaa kwenye maeneo tofauti tofauti kutegemeana na misimu inavyobadilika. Hata hivyo, kwenye kila ukanda wa Bahari huwa na eneo maalumu ambalo hufanya makazi yao.
Inadawaiwa kuwa kwa ukanda wa Bahari ya Hindi wa nchi za Afrika, mashariki Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma ndiyo sehemu pekee inayowavutia wanyama hao kuishi.
Mazingira salama, yenye joto
Paul Maige ni Mhifadhi wa Bahari na Muongozaji wa Watalii wa ghuba hiyo, aliiambia The Chanzo kuwa sababu kubwa zinazowafanya wanyama hao wavutiwe kukaa kwenye hifadhi hiyo ni kutokana na kuwa na mazingira salama na yenye joto, tofauti na maeneo wanayotoka ambayo yana baridi kwa kipinidi hiki. Wanapofika kwenye eneo hilo hutumia muda huo kwa ajili ya kujamiana ili waweze kuzaa, Maige anasema.
“Kitu kikubwa kinachowavutia katika hifadhi yetu ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma ni kwamba, nyangumi anakuwa katika kizio cha kusini kule, sasa hivi kuna baridi kubwa anakuja katika hifadhi yetu, ambayo maji yake ni ya joto kwa ajili ya lengo moja tu, kwa ajili ya lengo la kujamiana,” alieleza Maige.
SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo UVIKO-19 Inavyoliza Wafanyakazi Sekta ya Utalii Zanzibar
“Vilevile, kwenye mazingira yetu kuna chakula cha kutosha ndani ya hifadhi, hifadhi ya bahari ya Ghuba ya ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma,” aliongeza Maige. “Kwa sababu nyangumi anakula viumbe wadogo wadogo wanaoitwa plankton. Kwa hiyo, tuna plankton ya kutosha ambayo ndiyo chakula kikubwa sana cha hawa nyangumi.”
Sababu nyingine ni mazingira ya usalama wao, Maige alisema, na kuongeza: “Wana uhakika mkubwa ndani ya hifadhi hii [ya usalama]. Hatuna shughuli za kibinadamu nyingi ambazo zinaweza zikaathiri ustawi wao.”
Ujio wa nyangumi kwenye hifadhi hii umeendelea kuwa kivutio kwa baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi ambapo hutembelea hifadhini hapa na kujionea wanyama hao.
Kampeni yazinduliwa
Kutokana na hali hiyo, mwaka huu wa 2023, hifadhi hiyo, kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa wa Mtwara, imezindua kampeni maalumu ya msimu wa utalii wa nyangumi. Kupitia kampeni hiyo, kila mwezi huandaliwa siku maalumu za watu kwenda kufanya utalii wa wanyama hao kwa kipindi chote cha msimu.
Dk Redfred Ngowo ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma aliiambia The Chanzo kwamba kwa kipindi cha miaka miwili idadi ya watalii imeendelea kuongezeka ambapo mwaka 2022 waliweza kutembelea watu 560, huku mwaka huu wa 2023 mpaka sasa wameweza kutembelea watu 630.
“Tunagemea watu zaidi watakuja, hususan baada ya kuanza hizi kampeni na kuanzia sasa kila mwezi tutaandaa safari ambayo watu watakuja kwa magari mpaka hapa kisha tupanda boti kwenda kuwaona hawa nyangumi,” Dk Ngowo alisema.
SOMA ZAIDI: Baada ya Vilio vya UVIKO-19, Wafanyakazi Sekta ya Utalii Z’bar Wana Fursa Nyingine ya Kutabasamu
Nyangumi wamekuwa kivutio kwa watu ndani na nje ya nchi kwa kuwa wanyama hao wamekuwa na sifa za kipekee ambazo ni pamoja na kuwa ni viumbe wakubwa wanaoishi majini wakiwa na uzito mkubwa unakadiriwa kufika tani 40,000.
Nyangumi hubeba mimba kwa kipindi cha miezi 12 na mtoto wake huzaliwa akiwa na uzito wa kilogramu 900 hadi 1000, akiwa na uwezo wa kuzaa kila baada ya miaka mitatu.
Inatajwa kuwa nyangumi ni moja kati ya viumbe vilivyoko kwenye hatari ya kutoweka kutokana na kuvuliwa na kukutana na misusuko wakiwa baharini.
Maige aliiambia The Chanzo kwamba nyangumi waliwindwa sana hapo kipindi cha nyuma katika nchi za Asia kama chakula, hali iliyoleta hofu ya kutoweka kwao kwani kuzaliana kwao ni tofauti na wanyama wengine.
“Kwa hiyo, historia ya nyuma kuwindwa sana walikuwa katika hatari ya kutoweka lakini kutokana na tafiti ambazo tunafanya sasa hivi ambazo tunaendelea kuzifanya zinaonyesha kwamba wanyama hawa sasa hivi wanaongezeka na nadhani leo mmeshuhudia tulivyoingia majini mmeangalia makundi mbalimbali na wengi katika hifadhi yetu,” alieleza Maige.
Sambamba na uzindizu wa kampeni ya msimu wa nyangumi kwenye hifadhi ya hiyo, Dk Ngowo aliongeza kuwa kwa sasa unaandaliwa muongozo maalumu ambao utaweza kuwaongoza watalii na shughuli za utalii ili kuhakikisha wanyama hao wanalindwa na kuwafanya waendelee kubaki kwenye hifadhi hiyo.
“Na namna ya kuhakikisha tunahifadhi basi sasa hivi tunaandaa miongozo kwa ajili ya watu wanaotaka kwenda kuwaangalia wafanye nini na nini wasifanye nini,” alisema Dk Ngowo. “Hata madereva wa boti ili kuhakikisha kwamba hatuwatishi, hatuwaumizi na hatutupi taka ambazo zitawadhuru.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.Â