Mwezi huu, vyombo mbalimbalimbali vya habari vya Tanzania na nje vimeandika kuhusu suala zima la kusuasua kwa uuzwaji wa hisa za kampuni ya Tanga Cement kwa kampuni ya kimataifa ya Heidelberg ambayo inamiliki kampuni ya Twiga Cement hapa nchini.
Msingi wa taarifa hizo za kwenye vyombo vya habari ni hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Ushindani wa Haki (FCT) kwenye shauri lililofikishwa mahakamani hapo kupinga kitendo cha Tume ya Ushindani wa Haki (FCC) kukubali Twiga Cement inunue asilimia 68 ya hisa za Tanga Cement.
Hukumu ya FCT ilitolewa na majaji watatu wa Mahakama Kuu na kati yao wawili walitupilia mbali madai ya kampuni ya Chalinze Cement iliyofungua shauri hilo kwa maelezo kuwa haina msingi wa kisheria kufungua kesi.
Lakini jaji mmoja, Salma Maghimbi, alitoa msimamo tofauti, akiamua kuwa FCC haina nguvu kisheria kukubali Twiga Cement kuinunua Tanga Cement. Japokuwa shauri la Chalinze lilitupiliwa mbali, maelezo ya Jaji Maghimbi yanafuta uamuzi wa FCC ambayo ilikubali uuzwaji huo wa hisa Februari mwaka huu wa 2023.
Uamuzi huo ndiyo umesababisha baadhi ya vyombo vya kimataifa kuandika kuwa “suala la uuzwaji wa hisa za Tanga Cement umekwama” kwa vile inafahamika wamiliki wa Tanga Cement walikuwa wanatamani kuuza kampuni hiyo tangu mwaka 2017 lakini kwa sababu za kisheria, suala hilo limekwama hadi leo.
Utawala wa sheria
Mjadala au ripoti zinazoandikwa kuhusu suala hili la Tanga Cement, hata hivyo, hazisemi kitu kimoja kikubwa kinachoendelea nchini Tanzania hivi sasa: mabadiliko makubwa ya kuheshimu utawala wa sheria yanayoendelea chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ni rahisi kwa jambo hili kuwapita watu kwa sababu si tabia ya Rais mwenyewe kujipiga kifua na kueleza mabadiliko yanayoendelea kwenye Serikali yake.
Hakuna namna nzuri zaidi ya kueleza dhamira hii ya Rais Samia kama kuchukua maelezo ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, aliyezungumza bungeni mwezi Mei mwaka huu na kufafanua kuwa Serikali ya Tanzania inataka suala hili liishe haraka na Twiga iruhusiwe kununua Tanga Cement haraka iwezekanavyo.
SOMA ZAIDI: A-Z Sakata la Twiga Kuchukua Umiliki wa Tanga Cement na Ukinzani Unaombatana na Hatua Hiyo
Tafsiri ya maneno ya Mwigulu ilikuwa kwamba kama isingekuwa kuheshimu utawala wa sheria, uuzwaji wa hisa za Tanga Cement ungekuwa umemalizika.
Kwa Watanzania na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania walau kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, watafahamu kwamba huko tulikotoka, haingekuwa jambo rahisi kwa Mahakama au vyombo vyenye nguvu za kimahakama kama FCT kuweka “mguu chini” katika jambo ambalo inaonekana Serikali ina maslahi nalo na ingependa litekelezwe.
Itakumbukwa kwamba mtangulizi wa Rais Samia, hayati Rais John Magufuli, alipata kuzungumza hadharani kwamba yeye hatarajii Mahakama kuamua vinginevyo kuhusu jambo lenye maslahi kwa Serikali kwa vile yeye (Rais) ndiye ambaye huidhinisha mishahara, posho na marupurupu ya watumishi wa Mahakama – wakiwemo Majaji.
Huu ndiyo muktadha ambao inabidi Serikali ya sasa iangaliwe katika sakata hili la Tanga Cement. Kama Rais Samia angeamua kutumia mabavu na cheo chake, huenda sasa hivi tungekuwa tunazungumza mengine. Na kama Samia angeamua kufuata njia hiyo, asingekuwa Rais pekee wa Afrika kufuata njia hiyo.
Uchumi na uwekezaji
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi za Africa Legal na LexisNexis ilibainika kwamba katika bara zima la Afrika, ni nchi tatu tu zilikuwa na sifa ya kuingia kwenye kundi la nchi 50 bora kwa kufuata utawala wa kisheria – ikiwemo kutekeleza maamuzi ya Mahakama. Nchi hizo ni Rwanda, Botswana na Mauritius.
Ripoti hiyo ilikwenda mbali kwa kueleza kwamba kutokuaminika kwa utawala wa sheria ni miongoni mwa masuala yanayoathiri sana ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hakuna mfano mzuri wa kueleza hali hii kama mahojiano yaliyofanywa baina ya watafiti wa ripoti hiyo na wawekezaji wa Nigeria walioeleza kwamba hofu yao kubwa kuhusu uwekezaji ilihusu utii kwa utawala wa sheria nchini kwao na kwenye nchi nyingine za Afrika walikowekeza.
TAZAMA: Mtetezi wa Walaji Abainisha Madhara ya Twiga Cement Kuchukua Umiliki wa Tanga Cement.
Ni jambo zuri kwamba ingawa Rais Samia hajasema chochote hadharani kuhusu suala la Tanga Cement, amewahi kuzungumza hadharani kuhusu umuhimu wa watendaji wa Serikali na wataalamu kuzungumza vizuri na kutoingia kwenye migogoro na wawekezaji kiasi cha kufikia kupelekana mahakamani na Tanzania kulipishwa mabilioni ya shilingi kwa mambo ambayo kama sheria na taratibu za kawaida zingefuatwa, hali isingefika huko.
Kufuatwa kwa utawala wa sheria ni dalili mojawapo ya nchi inayotaka kuvutia wawekezaji zaidi – ndani na nje ya nchi, na kuongeza kujiamini kwa wawekezaji ambao tayari wana mitaji ndani ya nchi.
Ripoti tofauti za taasisi zinazoheshimika kama Benki ya Dunia, zimeonyesha kwamba mahali ambapo utawala wa sheria unaheshimika, ni mahali ambapo rushwa haiwezi kukua. Rushwa ni miongoni mwa maadui wakuu wa ukuaji wa uwekezaji na uchumi kwa ujumla.
Kusuasua uuzwaji Tanga Cement
Ingawa wamiliki wa Tanga Cement, kampuni ya AfriSam iliyosajiliwa nchini Mauritius lakini yenye asili ya Afrika Kusini, wameonyesha dalili ya kutaka kuuza kampuni hiyo maarufu nchini Tanzania, baadhi ya kampuni za uzalishaji wa saruji zimepinga uuzwaji huo kwa vile unakiuka Sheria ya Ushindani wa Haki inayozuia kampuni moja kuwa na umiliki mkubwa wa soko na hivyo kuwa kwenye hatari ya kuwa na bei zisizo shidani na zinazoumiza walaji.
Ingawa sheria inataka kampuni moja isiwe na udhibiti wa soko wa zaidi ya asilimia 35, wadai katika kesi iliyopelekwa FCT walionyesha kwamba endapo Twiga Cement itanunua Tanga Cement, itakuwa na udhibiti wa soko unaozidi kiwango kilichowekwa kisheria – wakidai kiwango kinaweza kufikia asilimia 47.26 ya soko zima.
TAZAMA: Aliyeishitaki Tume ya Ushindani Sakata la Twiga, Tanga Cement Afunguka
Bila shaka Serikali tayari imeweka makisio yake ya kodi, ajira na mapato mengine yanayoweza kupatikana endapo uuzaji huo utafanyika. Lakini, kinachoonekana hapa ni kwamba Serikali ya Rais Samia imeamua kwamba inaweza kujizuia na matamanio yake kwa kufuata utaratibu wote wa kisheria ili suala hilo lisije kuleta mgogoro baadaye.
Bahati nzuri ni kwamba katika uamuzi wake wa kupinga uamuzi wa FCC kuruhusu kuuzwa kwa hisa hizo, Jaji Maghimbi aliweka bayana kwamba kinachotakiwa kwa AfriSam na FCC ni kuhakikisha kwamba Mahakama ndiyo inatoa uamuzi huo kwa vile jambo lenyewe ni la kisheria na yenyewe ndiye yenye locus standi (nguvu ya kisheria) ya kufanya uamuzi wa mwisho wa jambo hilo.
Uzuri wa kufuata utawala wa kisheria ni kwamba endapo Mahakama itaeleza kwamba suala la asilimia 35 haliwezi kukiukwa, ina maana AfriSam wanaweza kuamua kuanza upya mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine aliye tayari kuinunua Tanga Cement pasipo kuvunja masharti hayo ya kisheria ya kutokuwa na udhibiti uliopitiliza wa soko.
Na kwa kufanya hivyo, wawekezaji wengine watakuwa na imani kwamba Tanzania ni nchi salama kwao na kwa vitega uchumi vyao. Pengine hili ndilo lililo kichwani mwa Rais Samia Suluhu Hassan hivi sasa.
Pius Mgheni amejitambulisha kama mchumi aliyebobea zaidi katika masuala ya uchumi wa viwanda. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mghenipius@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.