Mnamo Agosti 30, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri katika kile kinachoonekana kama nia yake ya kukipa chombo hicho nishati mpya. Kwenye mabadiliko hayo, Mkuu huyo wa Nchi pia alitambulisha Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu.
Kwenye mabadiliko hayo ambayo Samia aliyafanya akiwa nyumbani kwao Kizimkazi, Unguja, Rais huyo wa kwanza mwanamke wa Tanzania aliondoa na kuingiza watu wapya, huku akiwabadilisha ofisi wengine. Samia pia alibadili majina ya wizara na aliiboresha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kwa mfano, Rais Samia alimuweka kando Angeline Mabula kwenye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kisha kumteua Jerry Silaa kuongoza wizara hiyo. January Makamba katolewa Wizara ya Nishati kwenda Wizara ya Mambo ya Nje. Anthony Mavunde amepandishwa kutoka Naibu Waziri wa Kilimo kuwa Waziri wa Madini.
Rais Samia pia aliivunja Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kuunda wizara mbili tofauti: Wizara ya Ujenzi aliyokabidhiwa Innocent Bashungwa na Wizara ya Uchukuzi itakayokuwa chini ya Profesa Makame Mbarawa. Rais pia alihamisha, kutoa na kuingiza mawaziri wengine na manaibu waziri na makatibu wakuu.
Naibu Waziri Mkuu
Kwenye mabadiliko hayo, hata hivyo, Rais Samia alichukua uamuzi mmoja ambao baadhi wameutafsiri kama usiyo wa kawaida, na huo unahusu kuundwa kwa Cheo cha Naibu Waziri Mkuu.
Katika Marais sita waliopata fursa ya kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia anakuwa wa pili kuteua Naibu Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza, aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alimteua Dk Salim Ahmed Salim kuwa Naibu Waziri Mkuu.
Uteuzi wa Salim kuwa Naibu Waziri Mkuu unaweza kuutafuta kwenye makundi matatu: uteuzi wa kuoneana aibu, wa kiungwana, au kukosa namna. Inawezekana pia ukaangukia kwenye makundi yote hayo.
Rais Mwinyi, aliyeongoza kati ya 1985 na 1995, aliingia madarakani akimkuta Salim akiwa ni Waziri Mkuu. Wakati huo, nchi ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja. Rais akitoka Zanzibar, sharti lilikuwa Waziri Mkuu atoke Tanzania Bara ili awe Makamu wa Kwanza wa Rais. Mwinyi na Salim wote walikuwa Wazanzibari.
Joseph Warioba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Salim akawa Naibu Waziri Mkuu, akihudumu pia kama Waziri wa Ulinzi. Salim alikoma kuwa Naibu Waziri Mkuu Septemba 1989, alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), hivi sasa unaitwa Umoja wa Afrika (AU).
Augustino Mrema, Waziri wa Mambo ya Ndani mchapakazi, alimvutia Mwinyi. Januari 24, 1993, Mwinyi alimteua Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu, ili kumwongezea ari ya kufanya kazi.
Hata hivyo, katika kitabu chake cha Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu, ukurasa wa 269 hadi 273, Mwinyi anasimulia uhusika wa Mrema kwenye Baraza la Mawaziri aliloliongoza
Mwinyi, ambaye pia alihudumu kama Rais wa Zanzibar kati ya 1984 na 1985, anaandika kwenye kitabu hicho kwamba cheo cha Naibu Waziri Mkuu kilisababisha migongano kwenye Baraza la Mawaziri, hususan wakati wa Mrema, huku mawaziri wakilalamika kuingiliwa na Mrema kwenye majukumu yao.
Mnamo mwaka 1994, Rais Mwinyi alikifuta cheo hicho.
Rais Samia, aliyeingia madarakani Machi 19, 2021, amemteua Doto Biteko, Mbunge wa Bukombe (CCM), kuwa Naibu Waziri Mkuu. Hivyo, katika historia ya Tanzania, Biteko anakuwa kiongozi wa tatu kushika wadhifa huo, baada ya Salim na Mrema. Pamoja na unaibu Waziri Mkuu, Doto pia ni Waziri wa Nishati.
Tafsiri tofauti
Tunaweza kuutafsiri uteuzi wa Biteko kwa namna mbili kuu. Moja, Rais Samia anakoshwa na utendaji wa mbunge huyo na hivyo kumpandisha ngazi. Mbili, Mkuu wa Nchi ameona Ofisi ya Waziri Mkuu ina majukumu mengi na inahitaji msaidizi, akishawishika kwamba Biteko ni mtu sahihi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kama Naibu Waziri Mkuu, Biteko atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali. Ibara ya 52(1) ya Katiba ya 1977 inaeleza kwamba Waziri Mkuu ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali. Kwa maana hiyo, Biteko anapaswa kushughulikia uratibu wa shughuli za Serikali chini ya Waziri Mkuu.
SOMA ZAIDI: Tutathmini Utendaji Kazi wa Baraza la Mawaziri la Rais Samia
Eneo hili ndilo hasa linahitaji chemba ya watatu, yaani Rais Samia, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Biteko ili wazungumze namna bora Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu watakavyofanya kazi bila migongano.
Waziri Mkuu ni cheo cha Kikatiba, na wajibu wake wa kumsaidia Rais umewekwa bayana kwenye ibara ya 51. Naibu Waziri Mkuu ni cheo ndani ya mamlaka ya Rais, aliyopewa Kikatiba, kwenye ibara ya 36(1) na 36(2).
Rais Samia ndiye ameteua Naibu Waziri Mkuu chini ya Waziri Mkuu. Bila shaka kichwani anayo maono ya namna gani ofisi hizi mbili zinapaswa kumsaidia kazi. Maono hayo lazima ayatafsiri kwao.
Uhusiano na mipaka ya majukumu sharti viwe wazi kwa lengo la kurahisisha maisha mazuri ya kazi. Biteko hapaswi kuambiwa, “Utashughulikia uratibu wa Serikali.” Tayari mratibu mkuu wa Serikali ni Waziri Mkuu na cheo chake kimetafsiriwa kikatiba.
Migongano
Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa, katika kitabu chake cha My Life, My Purpose anasimulia mkasa wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Simon Mbilinyi, na naibu wake, Kilontsi Mporogomyi, uliohusisha kuvimbiana mpaka Mkapa akawaondoa wote.
Tunakumbuka pia sekeseke la Hamisi Kigwangalla, alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, hakuwa akiiva na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, mpaka kufikia hatua ya Rais John Magufuli kutoa onyo kali, akiwataka wawili hao wamalize tofauti zao ndani ya siku tano.
Hata Rais Samia, amepata kusimulia tabia za migongano kwa wasaidizi wake. Jumlisha na ukweli kwamba siasa zina visa vingi, ukweli unaopaswa kumsukuma Rais Samia kuketi na Majaliwa na Biteko kuwafanya wamsaidie ipasavyo.
SOMA ZAIDI: Je, Kuna Mantiki kwa Rais Samia Kuvunja Baraza la Mawaziri?
Isije kutokea Majaliwa anaona Biteko anaingilia majukumu yake. Haitafaa pia endapo Biteko atajisikia kubaniwa na Majaliwa kufanya kazi zake. Isitokee mambo hayafanyiki kwa sababu wawili hawa wanavutana, huku kila mmoja anamtegea mwenzake kwa kuona kitu fulani ni wajibu wake.
Muhimu zaidi ni kwamba iwe wazi kuwa Naibu Waziri Mkuu anafanya kazi chini ya Waziri Mkuu. Majaliwa awe anampa Biteko maagizo, miongozo, na maelekezo. Ikitokea Biteko na Majaliwa wote wanamtazama Rais katika uwajibikaji wao, pasipo wenyewe kuwa na nyenzo zinazowaunganisha na kuwapa njia za kupishana kikazi, kazi zitakuwa ngumu.
Ikitokea Rais Samia akambebesha majukumu mengi Biteko, ataua ‘shepu’ ya Waziri Mkuu. Vilevile, kuua dhana kuwa Doto anaandaliwa kuwa Waziri Mkuu ni kuwezesha wawili hawa kufanya kazi kwa maelewano kwa matokeo ya maono ya Rais na masilahi mapana ya Tanzania kama taifa.
Luqman Maloto ni mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thisluqman@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.