The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Matokeo Kidato Cha Nne 2023: Somo La Kiswahili Laendelea Kuongoza Kwa Ufaulu

Kwa ujumla ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.87 ambapo watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 wamepata madaraja I, II, III na IV ukilinganisha na mwaka 2022.

subscribe to our newsletter!

Baraza la Mitihani la Taifa limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) uliofanyinyika Novemba mwaka jana ambapo somo la Kiswahili limeongoza kwa ufaulu kwa kuwa na watahiniwa asilimia 96.8 waliopata daraja A mpaka D ukilinganisha na masomo mengine. 

Hili ni ongezeko la asilimia 1.38 ukilinganisha na mwaka 2022 ambapo somo la Kiswahili pia liliongoza  kwa kuwa na asilimia 95.59 ya watahiniwa waliopata dara ja A mpaka D.

Kwa upande wa ubora wa ufaulu wa daraja A mpaka C, ukilinganisha kati ya masomo saba yanayosomwa na wanafunzi wengi yaani Kiswahili, Biolojia, Uraia, Historia, Jiografia, Kiingereza na Hisabati, somo la Kiswahili limeongoza kwa kuwa na asilimia 74.39 ya ubora wa ufaulu.

Masomo mengine yaliyofuatia kwa ufaulu wa daraja A mpaka C, ni Biolojia asilimia 35.36, Uraia asilimia 30.91,  Historia asilimia 30.48, Jiografia asilimia 30.33, Kiingereza asilimia 27.49 na Hisabati asilimia 12.75.

Jumla ya watahiniwa  543,332 walifanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne kati ya watahiniwa 572,359 waliosajiliwa na Baraza la Taifa la Mitihani mwaka wa 2023.

Akitangaza matokeo haya mbele ya vyombo vya habari Dk Said Mohammed ambaye ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani amesema kuwa somo la Kiswahili ndilo limeongoza kwa kuwa na wanafunzi waliopata daraja la juu zaidi.

“ Somo la Kiswahili  limeongoza kwa kuwa na ufaulu wa daraja A, 22,427, pamoja na kuwa na watahiniwa wengi zaidi kwenye ubora wa ufaulu” alisema Dk Mohammed.

Kutokana na hali hiyo ya ufaulu katika masomo saba ambayo husomwa na wanafunzi wengi, baadhi ya wadau wameibua hoja kuhusiana na suala la lugha ya kufundishia kwa wanafunzi kwenye mfumo wa elimu.

“Kiswahili wanafaulu kwa asimilia 74.39 na masomo mengine wanachezea kichapo cha kati ya 12.75 – 35.36%. Hapa unaanzaje kupuuza suala la lugha ya kujifunzia na kufundishia?” Christian Bwaya ambaye ni Mwanataaluma wa Saikolojia na Mshunuzi  alihoji kupitia mtandao wa X.

Bwaya ni mmoja wa wadau ambao wamekuwa wakipigania mabadiliko mbalimbali kwenye mfumo wa elimu ikiwemo suala la lugha ya kujifunzia ili kuwawezesha wanafunzi wengi kuweza kufanya vizuri kitaaluma.

Kwa upande wa masomo mengine ya Sayansi ufaulu kwa ujumla umeonekana kuimarika huku somo la Kemia likiongoza kwa ufaulu uliofikia asilimia 96.14 na  Fizikia ufaulu ukiwa ni 71.86 kwa wanafunzi waliopata daraja A mpaka D.

Dk Mohammed amesema kwa ujumla ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.87 ambapo watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 wamepata madaraja I, II, III na IV ukilinganisha na watahiniwa 476,450 sawa na asilimia 86.78 mwaka 2022.

Kati ya watahiniwa hao waliofaulu, 257,892 sawa na asilimia 86.17 ni wasichana na Wavulana waliofaulu ni 226,931 sawa na asilimia 89.40.

Kwa upande wa ubora wa ufaulu, watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja I, II na III ni 197,426 sawa na asilimia 37.42. Kati yao, wavulana 108,368  sawa na 44.47% ukilinganisha na wasichana 89,058  sawa na 31.37%.

Wanafunzi 56,149 sawa na asilimia 10,64 wamefeli ambapo kati yao wasichana 33,764 na wavulana ni 22,385. Kiwango cha waliofeli kimepungua ukilinganisha na mwaka 2022 ambapo jumla ya watahiniwa 63,583 walifeli.

Katika taarifa yake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani pia alisema kuwa watahiniwa 13, 736 hawakuweza kufanya mtihani kwa sababu mbalimbali na Baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 376 kutokana na watahiniwa hao kupata matatizo ya kiafya, hivyo kushindwa kufanya mitihani yao. Hata hivyo Baraza limewapatia fursa kwa mujibu wa kanuni kuweza kufanya mitihani yao mwaka 2023.

Lakini pia matokeo ya watahiniwa 102 yamefutwa na Baraza kwa kufanya udanganyifu na watahiniwa wengine watano kwa kuandika matusi kwenye karatasi ya kujibia mtihani.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts