Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara imeagiza vielelezo vya mabaki ya mwili wa Mussa Hamis anayedaiwa kuuliwa na Polisi saba kuendelea kutunzwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Uamuzi huo umekuja kufuatia ombi la wakili wa upande wa mashitaka Maternus Marandu aliyeomba Mahakama kutoa maagizo maalum juu ya namna ya kutunza vielelezo namba sita, saba na nane vya kesi hiyo ambavyo ni mabaki ya mwili yanayodhaniwa kuwa ya Mussa Hamis.
Mabaki hayo ni mifupa nane ya mbavu, mifupa miwili inayodaiwa kuwa ni ya mguu wa kulia pamoja na suruali iliyookotwa kwenye eneo walilokuta mabaki.
Wakili Marandu ameiambia Mahakama kuwa mabaki hayo bado yanaweza kuendelea kutumika katika ushahidi wa kesi hiyo licha ya Hawa Bakari ambaye ni mama mzazi wa marehemu Mussa Hamis kuiomba Mahakama mabaki hayo kwa ajili ya mazishi kama yamethibitishwa kuwa ni ya mwanaye.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa vinasaba kutoka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyosalishwa Mahakamani hapo na shahidi namba tisa inaonyesha kuwa uwezekano wa vinasaba hivyo kuwa na uhusiano na sampuli ya mate iliyochukuliwa kwa Hawa Bakari ni asilimia 99.9.
Kufuatia uamuzi huu, kesi hii ambayo imesikilizwa mfululizo kwa siku 14 kuanzia Novemba 13, 2023 hadi Disemba 1, 2023, imehairishwa mpaka itakapopangiwa kikao kingine.
Hadi sasa tayari mashahidi 10 kati ya 72 upande wa mashitaka wameshawasilisha ushahidi wao mbele ya Jaji Ediwini Kakolaki.