Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza Serikali kugharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha na majeruhi kutokana na mafuriko na kutiririka kwa udongo kwenye makazi ya watu wilayani Hanang, mkoa wa Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu hadi sasa vifo vilivyoripotiwa ni 57 na majeruhi 85 wamefikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Maafa haya yameathiri mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na pia vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi.
Idadi ya kaya zilizoathirika ni takribani 1,150 zenye watu takribani 5,600 na mashamba yenye ukubwa wa ekari 750 yameharibiwa.
Rais Samia pia ameagiza Serikali kuhakikisha wananchi walioharibiwa makazi yao kuwa wanasitiriwa mahali pazuri katika kipindi hiki.
Bado mamlaka za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na shughuli za uokoaji.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia kurasa za The Chanzo