Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango ameweza kuonekana hadharani leo Disemba 10,2023, na kuzima uvumi uliokuwa ukiendelea nchini juu ya hali ya afya yake.
Mpango ameeleza kuwa amefika nchini Disemba 09,2023 na kuanza shughuli mbalimbali leo.
“Mheshimiwa Rais nilirejea jana nchini saa nane na leo asubuhi nimefika hapa saa moja nikakimbilia kwanza kwenda kuomba msaada wa Mungu na kumshukuru kwa kurejea salama,” ameeleza Dr.Mpango wakati akishiriki katika shughuli ya kupokea michango mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa maporomoko ya Hanang
“Kwa hiyo mheshimiwa Rais najua yamesemwa mengi kweli kweli lakini kikubwa niko salama nina siha njema kama ambavyo mnaniona,” aliendelea kufafanua.
Akizungumza mapema leo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma, Dr.Mpango ameeleza kuwa alikwenda nje ya nchi kufanya shughuli maalum kwa takribani mwezi mmoja.
Akiongelea kuhusu uzushi uliokuwa ukiendelea, Rais Samia ameeleza ni tabia ya watu wanaopenda kuleta taharuki nchini.
“Karibu nyumbani na nikuambie tu ukiwa kiongozi wewe ni mtu mashuhuri. Sasa kuna wale watakaojiuliza kwa kweli yuko wapi mbona hatumuoni lakini kuna wazushi tu wanaoamua kuzusha tu na kuleta taharuki kwenye nchi,” alielezea Rais Samia.