Nimefanikiwa kuusoma unaoitwa Waraka wa Mabadiliko 2013 uliotayarishwa na Samson Mwigamba, aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha, na kuhaririwa na Kitila Mkumbo, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, uliolenga kumuuza Zitto Kabwe, wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa chama, kwa nafasi ya mwenyekiti taifa wa CHADEMA.
Waraka huo ulieleza mabadiliko ambayo wafuasi wa Zitto Kabwe walitamani kuyaona ndani ya chama na njia za kuyafanikisha. Kwa bahati mbaya, Waraka huo ulitafsiriwa kama “uhaini” ndani ya CHADEMA, na Zitto, pamoja na Kitila, walifukuzwa kutoka chama hicho kwa madai ya “kupanga mapinduzi.”
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya wawili hao kudaiwa kuvunja kanuni za chama kwa kupeleka malalamiko yao mahakamani. Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA wakati huo, Tundu Lissu, alitangaza uamuzi huo kwa kunukuu kifungu 8(a)X cha kanuni za chama.
Mjadala kuhusu tukio hilo umeibuka tena wakati wa mchakato wa uchaguzi unaoendelea ndani ya CHADEMA. Lissu, ambaye sasa anawania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho cha upinzani, alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu mlingano kati ya kile anachokifanya sasa na matendo ya Zitto Kabwe takriban miaka 12 iliyopita, aliendelea kuueleza Waraka huo kama “mpango wa mapinduzi.”
“Zitto Kabwe alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama,” Lissu alisema kwenye moja ya mahojiano yake na wanahabari. “Waliandaa mpango wa kufanya mapinduzi ndani ya chama. Tuliwafukuza kwa sababu waliandaa mpango wa kufanya mapinduzi ya uongozi.”
Naye Ezekiel Wenje, anayegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, katika kikao chake na waandishi wa habari Januari 16, 2024, alijibu tuhuma mbalimbali kutoka kwa Godbless Lema na akatoa maelezo kuhusu tukio hilo.
“Zitto Kabwe, akiwa mwana-CHADEMA, rafiki yangu Godbless Lema ndiye aliyekamata laptop ya [Samson] Mwigamba huko Arusha. Ndani ya laptop hiyo walikuta maandishi yaliyohisiwa kuwa mpango wa Zitto na wenzake kufanya mapinduzi ndani ya chama.”
Zitto alikuwa sahihi
Mjadala huu unaonyesha kuwa kuna mtazamo miongoni mwa wanachama kuwa Zitto Kabwe na Kitila Mkumbo walikuwa sahihi, kwani mambo waliyolalamikia wakati huo yanaonekana kuwa tatizo hata sasa.
Waraka huo ulianza kwa kuwapongeza viongozi wa CHADEMA waliotangulia, yaani Edwin Mtei, Bob Makani, na Freeman Mbowe. Aidha, ulieleza kuwa chanzo cha jitihada za Mwigamba, Kitila na wenzao kutafuta mabadiliko kilikuwa ni kuheshimu ukomo wa madaraka uliowekwa na kuheshimiwa na Mtei na Makani na kupinga jinsi ukomo huo ulivyoondolewa kinyemela mwaka 2006 Freeman Mbowe akiwa Mwenyekiti.
Ajenda ya ukomo wa madaraka, ambayo ni moja ya hoja kuu za Tundu Lissu leo, ni sawa kabisa na ile ya Zitto Kabwe mwaka 2013. Ni dhahiri kuwa ukomo wa madaraka uliondolewa ili kumruhusu Mwenyekiti aliyepo kuendelea kuongoza bila kikomo, jambo lililokiuka utamaduni uliowekwa na waasisi wa chama.
Chanzo cha mgogoro kati ya Zitto na CHADEMA kilihusiana na uenyekiti wa chama, kama ilivyo sasa kwa Tundu Lissu.
Kwa mantiki hiyo, si sahihi kuita kitendo cha Zitto Kabwe “uhaini” kwani leo tunakubaliana kuwa ukomo wa madaraka ni muhimu. Zitto Kabwe amekuwa muumini wa dhana hii hata akiwa kiongozi wa ACT-Wazalendo, alipoanzisha ukomo wa madaraka mwaka 2019.
Pili, Waraka wa Mabadiliko 2013 ulizungumzia matumizi mabaya ya fedha za chama. Hadi sasa, kuna ukimya kuhusu fedha za kampeni ya Join The Chain, licha ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kujitokeza hadharani na kutoa maelezo mafupi kuhusiana na kiasi cha fedha kilichokusanywa au jinsi zilivyotumika.
Waraka wa Mabadiliko 2013 ulifichua kuwa baada ya uchaguzi wa 2010, vikao vya chama vilielekeza fedha fulani kuhifadhiwa kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini kufikia wakati wa kuandikwa kwa Waraka, fedha hizo hazikuwepo tena.
Aidha, ilielezwa kuwa watu watatu pekee walikuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi kuhusu fedha za chama. Hali hiyo imepelekea baadhi ya wanachama kuamini kuwa chama hakiwezi kujiendesha bila mtu mmoja kufadhili. Hili limefanya baadhi ya wanachama waandamizi kumuita Mwenyekiti was “alpha na omega” wa chama.
SOMA ZAIDI: Zama za Samia, Zitto na Mbowe
Waraka wa Mabadiliko 2013 pia ulieleza changamoto za uongozi ambazo zinafanana na zile zinazotajwa na Tundu Lissu na timu yake ya kampeni leo hii, zikiwemo za matumizi mabaya ya madaraka na mfumo mbovu wa uteuzi wa maofisa wa makao makuu. Haya yote yalikuwa msingi wa Zitto Kabwe kutaka uenyekiti wa chama.
Waraka wa Mabadiliko 2013 ulikuwa mpango wa kuelezea roadmap ya kufanikisha azma hiyo. Kuonyesha kuwa waliouandaa Waraka husika walikuwa na nia ya kumweka mtu sahihi kama Mwenyekiti, na si njama tu za kumuondoa aliyekuwa madarakani, waliandaa tathmini ya kina kuhusu uimara na udhaifu wa mgombea wao kupitia uchambuzi wa SWOT – Strengths, Weaknesses, Opportunities, and Threats.
Uchambuzi huo ulilenga kumtathmini Zitto Kabwe kwa undani. Kwa kuwa tathmini hiyo ilijumuisha vipengele vingi vya kina, nawashauri wasomaji waende moja kwa moja kwenye Waraka husika kujisomea na kuelewa kwa undani jinsi SWOT analysis hiyo ilivyoandaliwa na hoja zilizowekwa mezani.
Kampeni za kisiasa zinahitaji maandalizi, na tofauti kati ya Zitto na wenzake ni kwamba mpango wao uligunduliwa mapema. Hata hivyo, si sahihi kuwaita wasaliti au wahaini. Kama ilivyokuwa kwa Zitto Kabwe, Tundu Lissu pia anasukumwa na nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ndani ya chama na kwa taifa kwa ujumla.
Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au X kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.