The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kufuta Kadi Nyekundu Haitoshi, Tuanzie Uchunguzi kwa Refa Japhert Smarti

Ni muhimu kwa mamlaka kuchukua hatua kuanzia hapo kwa Smarti na kwenda hadi matukio mengine mengi yanayolalamikiwa kila wiki tangu msimu huu wa Ligi Kuu uanze.

subscribe to our newsletter!

Imekuwa ni kawaida kwa mamlaka za soka kuchukua hatua za kubatilisha adhabu zilizotolewa na mwamuzi wakati wa mechi, au kumfungia refa aliyefanya uamuzi tata baada ya umma kupiga kelele dhidi ya matukio hayo.

Uamuzi wa kufuta kadi nyekundu umekuwa ni wa kawaida kutolewa na Kamati ya Usimamizi wa Ligi, maarufu kwa jina la Kamati ya Masaa 72, kila mara kunapokuwa na tukio linalolalamikiwa na timu, makocha, au hata wachambuzi. Na ni kawaida pia kusikia refa fulani amefungiwa kwa kushindwa kutafsiri sheria fulani.

Baada ya muda marefa haohao hurejeshwa katika ratiba na kuendelea kuchezesha mechi, huku baadhi wakirudia makosa yaleyale katika mechi ya kwanza kurudishwa kwenye ratiba. Na utoaji holela wa kadi nyekundu huendelea kana kwamba hakuna uamuzi kama huo uliowahi kufutwa na hivyo kusababisha waamuzi wawe makini zaidi.

Mambo yamekuwa “bora liende.” Kwamba mashabiki, viongozi na makocha watalalamika lakini baada ya uamuzi kama huo wa kuwatuliza, watakaa kimya na mechi zitaendelea kuchezwa kama kawaida.

Hakujawahi kuibuka hofu kwamba huenda makosa hayo ya kiuamuzi yana uhusiano na rushwa kwa waamuzi kushiriki kupanga matokeo kwa ajili ya kuzinufaisha timu. Kwa mamlaka, adhabu ndio njia pekee ya kukabiliana na kasoro hizo zilizopachikwa jina la “makosa ya kibinadamu.”

Pia, hakujawahi kutokea hofu kwa mamlaka kwamba kasoro hizo zinasababishwa na magenge ya michezo ya kubahatisha ambayo hutumia fedha nyingi kupanga matokeo kwa lengo la kutengeneza mabilioni ya fedha.

SOMA ZAIDI: Uwakilishi wa Wazanzibari Unahitajika Uongozi wa Michezo Kitaifa

Wiki chache zilizopita, redio moja iliibua mjadala wa wachezaji kushiriki michezo ya kubashiri matokeo, ikijenga hoja kuwa huenda matokeo ya mechi nyingi yanaathiriwa na tabia hiyo. 

Hata hivyo, mjadala huo haukutokana na ripoti kali ya uchunguzi iliyobaini vitendo hivyo, zaidi ya washiriki kusema wanawafahamu wachezaji wanaoshiriki michezo hiyo, kitu ambacho kwa vyombo vyetu vya uchunguzi hakiwezi kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.

Kwa wenzetu, mijadala kama hiyo hutanguliwa na ripoti makini inayoonyesha jinsi upangaji matokeo unavyoendeshwa na michezo ya kubahatisha na jinsi wahusika wanavyoshiriki, ripoti ambazo nyingi zimechukuliwa kwa uzito na vyombo vya uchunguzi na baadaye kuthibitisha ukweli uliosababisha baadhi ya washiriki kufungwa jela, wengine kufungiwa maisha kushiriki katika michezo.

Kutuliza mashabiki

Uamuzi wa Kamati ya Saa 72 uliotolewa wiki iliyopita ni miongoni mwa maamuzi ya mazoea ya kutuliza mashabiki ili waone hatua zimechukuliwa baada ya wengi, hadi mtangazaji wa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kushindwa kuona tukio lililosababisha mwamuzi kutoa adhabu hiyo kubwa uwanjani.

Mwamuzi Japhert Smarti alishindwa kuishi na jina lake la pili linalomaanisha ‘nadhifu’ kwa lugha ya Kiingereza, wakati alipomuonyesha beki wa Namungo, Derick Mukombozi, kadi nyekundu ya moja kwa moja katika ya 35 ya mchezo.

Refa alimaliza mechi hiyo akiwa ameamuru penati tatu dhidi ya Namungo iliyokuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu ya Bara.

SOMA ZAIDI: Jamii Haina Budi Kumlinda Ladack Chassambi

Kwa kawaida, maamuzi ya kutoa kadi nyekundu na penati ni kati ya maamuzi makubwa uwanjani yanayohitaji refa awe na uhakika wa angalau asilimia 80. Ni matukio ambayo hubadili mchezo kabisa, hata pale timu pungufu inapopata matokeo mazuri, hutokana na jitihada za ziada kukabiliana na upungufu huo na ari ya kutaka matokeo.

Mara nyingi hudhoofisha timu moja na kuondoa ladha ya mchezo, iwapo timu iliyo pungufu, au iliyoruhusu penati mapema haitakuwa imara kisaikolojia. Kwa wale wenye roho nyepesi, huamua kuondoka uwanjani hata kama matukio hayo yametokea mapema, hivyo yale mazingira ya ushabiki shindani hupotea uwanjani.

Na ndio maana matukio ya penati na kadi nyekundu ya moja kwa moja ni kati ya yanayochunguzwa kwa kamera tofauti za Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) na refa kutakiwa aangalie vizuri kwenye runinga inayosimikwa pembeni ya uwanja ili atoe uamuzi akiwa na taarifa kamili ya tukio.

Lakini Smarti hakuwa na msaada wa kamera hizo tatu na tukio lilitokea eneo ambalo mwamuzi msaidizi namba mbili yuko upande wa mbali na hivyo asingeweza kumsaidia, huku refa wa kati mwenyewe akiwa anatakiwa kufuatilia mwenendo wa mpira baada ya kutoka eneo ambalo Mukombozi alikuwa akimdhibiti Leonel Ateba wa Simba.

Pamoja na kamera za televisheni kurudia matukio kwa kona tofauti, bado haikuweza kungamua eneo ambalo tukio la Mukombozi na Ateba lilitokea. Hivyo, Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, ikaamua kufuta kadi hiyo ya Mukombozi, ikisema kuwa ripoti ya Smarti inatofautiana na picha za marudio ilizoangalia. Au, kwa maneno mengine, kamati ingesema kuwa hakuna tukio ambalo lilisababisha Smarti atoe kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti; umethibitisha kwamba mwamuzi alitaka kuiua Namungo mapema na wengine wakiona kwamba kufuta adhabu pekee si kutatua tatizo kubwa la uamuzi linaloendelea kusumbua kila wiki.

SOMA ZAIDI: Ifike Wakati Maofisa Habari wa Klabu Waache Kupumbaza Mashabiki wa Soka

Kutofautiana na uamuzi wa refa kunatakiwa kuwe hatua ya kwanza kukabili janga hilo linaloweza kuondoa heshima ya mchezo wa mpira wa miguu. Hatua inayofuata iwe na uchunguzi kama kuna ushawishi ulisababisha achukue uamuzi ambao umetafsiriwa kuwa ulilenga kuidhoofisha Namungo.

Kamari, rushwa

Lakini hatua nyingine iwe ni kufuatilia kwa ukubwa zaidi kasoro hizi zinazochafua mchezo huu, hasa nyakati hizi ambazo michezo ya kubashiri inakua kwa haraka kadri teknolojia inavyokua, na magenge ya wachezaji kamari yakizidi kutumia fedha kupanga matokeo.

Lakini si kamari pekee, uchunguzi pia uangalie kama tuhuma zinazotolewa kila wiki kuwa kuna mpango wa kuibeba timu moja, zina mizizi yoyote ili wahusika wachukuliwe hatua. Kesi za rushwa katika soka letu hazijawahi kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na kusababisha ligi zetu zionekane kama ni safi.

Lakini kwa tuliowahi kuwa kwenye utendaji tunajua kuwa ziko nyingi,  lakini wahusika hawataki zishughulikiwe na vyombo husika. Kuna wakati kulipatikana ushahidi mzito wa miamala ilivyotembea kwa wachezaji wa klabu moja baada ya kufungwa, lakini familia ya wamiliki wa hiyo klabu wakasema suala hilo liishie hapo na hawako tayari kuwasilisha vielelezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kuna wakati mchezaji alikiri kuwa alipewa fedha ili asifunge bao timu moja na akaandika barua, lakini mamlaka hazikushughulikia kesi hiyo kwa uzito. Kuna wakati mchezaji alikamatwa na fedha baada ya polisi kufuatilia mawasiliano yake na kipa wa timu moja, lakini suala hilo likaishia kituo cha polisi. Hivi sasa kuna taarifa kuwa kuna vijana ambao wamejitoa muhanga kufuatilia marefa na kuwapa fedha kutoka timu zetu za Ligi Kuu ili wazipendelee.

Viongozi hawawezi kujihusisha moja kwa moja kuwafuata waamuzi kutokana na kuogopa kufungiwa, hivyo wanawatumia vijana ambao si rahisi kuwahisi na hata wakibainika, adhabu za mpira haziwaathiri.

Hatua

Haya yote hayawezi kupita hivihivi kwa kudhani yataisha tu. Badala ya kuisha yanakomaa na yakikomaa yataushusha hadhi mchezo huo na kupoteza umaarufu wake kirahisi.

SOMA ZAIDI: Uraia kwa Viungo Watatu wa Singida Big Stars Haukidhi Maslahi Yoyote ya Kisoka au Kitaifa. Ubatilishwe

Ni muhimu kwa mamlaka kuchukua hatua kuanzia hapo kwa Smarti na kwenda hadi matukio mengine mengi yanayolalamikiwa kila wiki tangu msimu huu wa Ligi Kuu uanze.

Kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu ndicho ambacho hujaa matukio ya upangaji matokeo wakati timu zikisaka ubingwa, nafasi za kushiriki mashindano ya kimataifa, kukwepa kushuka daraja moja kwa moja na kukwepa kwenda michezo ya mtoano kwa ajili ya kubakia Ligi Kuu.

Tuanzie hapo kwa Smarti, na kipindi hiki cha mwisho wa msimu. Tungependa kusikia mamlaka zikitoa tamko la matokeo ya uchunguzi kabla ya kumalizika kwa msimu.   

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×