Siku ya Jumamosi, Julai 11, 2021, ilikua ni siku ya vilio na majonzi kwa wafanyabiashara wengi wa soko la Kariakoo, maarufu kama Shimoni, lililopo jijini Dar es Salaam. Moto ambao bado haujaelezwa chanzo chake ulizuka na kuteketeza mali nyingi na kuharibu jengo la soko. Moto huo ulifanikiwa kudhibitiwa baada ya masaa kadhaa ya kupambana nao, huku Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likilalamikia ukosefu wa miundombinu rafiki na kutokuwepo kwa maji karibu, kama moja ya changamoto zilizopelekea moto huo kutokuzimwa mapema.
Tayari wafanyabiashara kadhaa wamejitokeza wakilalama juu ya kupotea kwa mali zao na njia zao za kujiingizia kipato, huku wengi wakionesha majonzi zaidi juu ya mikopo wanayodaiwa. Kwa kawaida, mabenki mengi yanayokopesha wafanyabiashara, hasa wafanyabiashara wa kati, huwapa takwa la kuwa na bima ya biashara kama moja ya kigezo cha kupata mkopo. Lakini kundi kubwa la wafanyabiashara, hasa wadogo na wakati, pasipo kuwekewa shurti, bado huona bima ni kama jambo la starehe linalomaliza faida yao. Hii ni licha ya ukweli kwamba bima nyingi ni za gharama nafuu.
Kwa Tanzania, bima ambayo inaongoza kwa kununuliwa ni bima ya vyombo vya moto (yaani magari nakadhalika) ambayo inachukua asilimia 33 ya soko lote la bima. Bima hii ni lazima kisheria. Bima inayofuatia kununuliwa zaidi na Watanzania ni bima ya moto ambayo inachukua asilimia 22 ya soko la bima inayotolewa kwa makazi binafsi na biashara.
Watumiaji wa bima ya moto
Ukiangalia data hizi kwa harakaharaka, unaweza kudhani kwamba bima ya moto inachangamkiwa pia na Watanzania kama ilivyo kwa bima ya magari. Lakini hili si kweli. Wakati kuna magari zaidi ya laki tatu Tanzania, kuna mamilioni ya biashara Tanzania, achilia mbali makazi. Sehemu kubwa ya watu wanaonunua bima ya moto ni biashara kubwa na ni sehemu ndogo sana ya wafanyabiashara wa kawaida wanachukua bima hizi.
Kwa upande wa watoaji bima, wao wameweza kujipambanua vyema juu ya bima mbalimbali wanazoweza kutoa katika biashara kuilinda dhidi ya majanga ya moto. Kwanza, kuna bima ya moto (fire and allied perils) ambayo huaangalia uharibifu wowote unaoweza kufanywa na moto, radi, milipuko juu ya majengo na vitu vilivyomo ndani ya majengo kama samani, vifaa vya ofisi pamoja na bidhaa.
Pia kuna bima ya madhara ya moto (fire consequential loss/business interruption) ambayo inaenda mbali na kumgharamia mteja hasara zote atakazozipata moto unapotokea, ikiwemo kulipa mishahara, faida inayopotea, pamoja na kugharamia hasara mpaka pale biashara itakaposimama. Wastani wa gharama (premium) kutoka kwenye makampuni mengi ya bima ni chini ya asilimia 0.3 katika soko zima. Hii maana yake ni kwamba ukiwa na biashara ya milioni 100 utahitajika kulipia bima ya laki tatu au chini ya hapo kwa mwaka mzima. Gharama za bima hizi bado ni ndogo ukilinganisha na hasara inayoweza kujitokeza pale majanga yanapotokea.
Umuhimu wa kubadilisha tabia
Moja ya sababu kubwa inayopelekea watu wengi kutokua na bima tofauti na bima za magari ni tabia. Bado kampuni nyingi za bima, na hata Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), hawajafanikiwa kuilezea bima hii kwa namna ambavyo itaeleweka kwa jamii. Makampuni yamejikita zaidi kwenye kugombania keki ya ‘premium’ kutoka kwa makampuni makubwa, huku wakiacha kujijenga kimasoko kwa wateja wengi ambao ndio watakua mustakabali wa bima Tanzania na Afrika Mashariki.
Mbinu za masoko, ujumbe na ushawishi unaotumiwa kwa wateja wa kawaida ndiyo hizo hizo zinatumiwa kwa wateja wakubwa. Makampuni ya bima hayajapata lugha ya kuongea na wananchi wa kawaida. Na hii yote inatokana na uwekezaji mchache unaofanywa kwenye kujifunza namna kundi la wananchi wa kawaida linavyofikiri na namna ya kulibadilisha.
Moja ya suala linalofanya kampuni za bima kusita kujitanua zaidi kwenye masoko ya bima ya kawaida ni hatari za kibiashara (business risk). Kuna nadharia kwamba wafanyabiashara wadogo na wa kati ni rahisi sana kujikuta katika majanga au pia ni rahisi kufanya matendo ya ulaghai wa bima (insurance fraud). Zote hizi ni hofu zinazotokana na mtazamo tu na wala siyo utafiti.
Kama kukiwa na lengo thabiti la kutanua wigo wa bima kwa makundi ya wananchi wa kawaida kwanza lazima wataeleweshwa na kuelewa hatari inayotokana na kulaghai bima. Pili, wateja wengi wa kawaida hawana njia (sophistication) ya kufanya ulaghai wa bima hasa kwa bima kama za moto au biashara. Tatu, hatari za kibiashara zinazotokana na bima kwa biashara ndogo sio sawa na kwa biashara kubwa. Kwa mfano, ni ngumu kulinganisha madai yaliyotokana na hoteli kuungua miaka kadhaa iliyopita na madai yanayoweza kuletwa na mfanyabiashara wa sokoni au wa duka.
Naomba nimalizie kwa kusisitiza kwamba tukio la kuungua kwa soko la Kariakoo linatukumbusha tena juu ya ulazima wa kubadilisha uelewa wa jamii juu ya bima zaidi ya zile za magari. Ili hili lifanyike, kuna uhitaji mkubwa wa makampuni ya bima kuonesha utayari wa kibiashara lakini pia Serikali, kupitia TIRA, kuonesha njia, kwenda mbele na kutoa elimu itakayoleta mhamo wa ruwaza (paradigm shift) katika jamii yetu.
Tony Alfred ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.