Kwa majina naitwa Rehema Masanja. Nimezaliwa Novemba 7, 2000, mkoani Shinyanga nikiwa mtoto wa sita kwenye familia ya watoto nane. Watoto saba tumezaliwa kwa mama mmoja isipokuwa mmoja amezaliwa na mama mwingine. Katika familia yetu, ni mimi peke yangu niliezaliwa na ulemavu wa ngozi, yaani albino.
Maisha yangu mpaka nakua nimekuwa nikilelewa na mama. Baada ya mama yangu kunizaa mimi nikiwa na hali hii ya ulemavu wa ngozi, baba yangu hakuweza kunikubali mimi kama mtoto wake. Na ilipofika wakati wa mimi kwenda shule, sikuweza, kwani baba yangu alikataa mimi kwenda shule. Alikuwa akisema kuwa mimi nikienda shule nitasumbua walimu na wanafunzi wenzangu kwa vile nina uoni hafifu hivyo sitaweza kusoma.
Baada ya hayo yote, baba yangu aliuza kila kitu na kuamua kuondoka nyumbani akatuacha bila ya kuwa na kitu chochote. Kabla ya yeye kuondoka, maisha yalikuwa ya kawaida sana, lakini baada ya kuondoka maisha yalikuwa magumu. Tulikuwa tuna hali ngumu lakini mama yangu alipambana kuhakikisha kwamba watoto wake tunapata chakula kama familia nyingine.
Nakumbuka wiki mbili kabla ya tukio la kukatwa mkono wangu wa kulia nikiwa mimi na wifi yangu, tulienda mashineni kusaga. Kuna mtu tulimuona alikuwa akiniangalia sana mimi. Nikajiuliza kwa nini mtu huyu ananiangalia kiasi hiki. Kwa sababu alikuwa akiniangalia kwa muda mrefu sana. Kiukweli, nilishituka sana nikaamua kumuuliza kwa nini unaniangalia hivyo? Wifi yangu yangu akaniambia muache tu labda kwa sababu hawajawahi kuwaona watu kama nyie, na mimi nikaachane naye.
Siku mbili kabla ya tukio, mtu mwingine tofauti na huyo alikuja nyumbani kuomba maji ya kunywa. Akapewa halafu akauliza kuna watu wengine humu ndani? Akajibiwa kuwa hawapo. Akaondoka zake.
Tukio la kukwata mkono
Ilipofika Aprili 26, 2010, majira ya saa tano usiku, watu watatu walituvamia nyumbani na ndipo waliponikata mkono wangu. Kati ya wale watu watatu, wawili nilikuwa nimewaona kabla ila mwingine sikuwahi kumuona kabisa. Cha kushangaza wale watu watatu baada ya kutenda unyama huo walichukua mafuta ya taa wakamkabidhi mama na wakamuambia animwagie kwenye kidonda ili nisife.
Na wakamuambia mama asiwalaumu wao, amlaumu Philipo aliyewaagiza kuja kufanya unyama huu. Huyu Philipo waliyekuwa wanamsemea ni mtu ambaye alikuwa na duka kubwa pale kijijini. Alikuwa ni mtu anayefahamika na watu wengi sana.
Watu ambao walinifanyia unyama huu waliweza kutiwa nguvuni na vyombo vya sheria. Niliweza kusikiliza kesi mahakamani kama mara mbili hivi lakini baada ya hapo sikusikia chochote kikiendelea. Kitendo cha mimi kukatwa mkono kilisababisha nikae mbali na familia yangu na jamii yangu iliyokuwa imenizunguka.
Baada ya tukio hili lililonikuta nilipelekwa kituo cha malezi cha Buhangija, Shinyanga ambacho huko tulikuwa tukiishi na walezi na tulikuwa wengi. Kwa haraka haraka maisha ya kituoni hayakuwa mazuri kwa sababu watu tulikuwa wengi nikiwa na maana ya kuwa mazingira hayakukwa rafiki.
Tukio la Kukatwa kwangu mkono nafikiri linatokana na imani potofu ambazo watu walikuwa nazo kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi. Watu wengi walikuwa wakiamini kwamba viungo vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi vinaweza vikamfanya mtu akapata madaraka, akawa tajiri au akawa na mafanikio makubwa. Nadhani hizi ndizo sababu ambazo zilifanya tuwe tunawindwa kila kona na kupoteza viungo kama ilivyonikuta mimi.
Safari ya kujipatia elimu
Nilipokuwa Buhangija mwaka 2011, ndipo nilianza kusoma elimu ya watu wazima kupitia Mpango kwa Elimu Maalum kwa Watoto waliokosa (MEMKWA). Nilisoma darasa la tatu na darasa la nne katika Shule ya Msingi Buhangija kwa sababu sikuwahi kwenda shule hapo awali.
Ilipofika mwaka 2012, nilifanikiwa kupata ufadhili nikahamishwa kutoka Shule ya Msingi Buhangija na kupelekwa Shule ya Msingi Mingasi iliyopo Kahama. Nikasoma darasa la tano, la sita. Darasa la saba nikasoma miezi michache nikapelekwa nchini Marekani kwa ajili ya matibu ya mkono, kisha nikarudi nikafanya mtihani na kuhitimu mwaka 2015.
Mwaka 2016 nilifanikiwa kujiunga na na elimu ya sekondari katika shule ya Montessori Maria iliyopo mkoani Mwanza na kuhitimu 2019. Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, nilifanikiwa kufaulu vizuri na kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Lake mkoani Mwanza ambap sasa nipo kidato cha tano, ninachukua mchepuko wa Historia, Kiswahili na Kiingereza (HKL).
Changamoto moja kubwa ambayo tunakutana nayo hasa sisi wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ni walimu kushindwa kutuelewa. Unaweza ukamueleza mwalimu shida yako, yaani yeye anaona ni jambo la kawaida sana. Kwa hiyo, kwangu mimi ni changamoto kubwa sana. Mfano nina mkono mmoja kila kitu kinautegemea huu mkono, sina ule uwezo wa kusema nitaandika zile notes zote kwa muda ule ule. Kwa hiyo, unakutana na mwalimu ambaye hakuelewi na hawezi kukusikiliza.
Changamoto nyingine labda kwenye mitihani. Kuna wakati unatamani umalize maswali lakini muda unakuwa umeisha. Ukikutana na mwalimu hajali, hawezi akakusikiliza au akakuongezea dakika. Kwa hiyo, hii nayo ni changamoto ambayo kwa kipindi cha nyuma nilipitia.
Rehema mpambanaji
Namna ambavyo jamii inanitazama ni kwamba Rehema anaenda shule, anasoma na anahakikisha amefaulu. Rehema anarudi kwenye jamii anafanya kazi mfano za ulimaji, wengine wanavutiwa wanatamani kufika sehemu niliyofika lakini hawana uwezo na wengine si kwamba hawana uwezo ni uoga tu.
Lakini Rehema anakaa, anashona kitu ambacho pamoja na mtu kuwa na mikono miwili hawezi akakifanya. Naona kama jamii yangu inanitazama kwa mtazamo wa kwamba watu wengine wanaweza wakahamasika kwa kupitia mimi na kuweza kunyanyuka na bila kukata tama.
Kiukweli iliwahi kutokea nikakata tamaa kutokana na hali niliyokuwa nayo. Nakumbuka ilikuwa ni kidato cha pili. Ilifika muda nipo kama kwenye makundi mawili. Kundi moja linataka kunisaidia na kundi la pili linataka kunikwamisha. Hii ilisababisha mimi kupoteza muelekeo. Nikasema sasa nimsikilize nani nimuache nani.
Mama yangu aliwahi kuniambia kipindi cha nyuma kwamba ulemavu katika maisha sio mkosi. Kwa babu kama ingekuwa mkosi nisingekuwa najitokeza kwenye jamii ya aina yeyote. Kwa hiyo, jamii kama jamii inapaswa kutambua kwamba ulemavu wowote ule sio mkosi katika jamii ni mipango ya muumbaji.
Na mtu kuwa na ulemavu haimanishi kuwa hawezi kufanya chochote. Mtu mwenye ulemavu ni mtu kama watu wengine na anaweza akafanya mambo makubwa na wengine wakaiga kwake.
Ndoto kufanyakazi na UNICEF
Mimi ndoto yangu kubwa ni kuwa mwanasheria na natamani kufanya kazi na shirika la watoto duniani, UNICEF. Kitu kilichonivutia mimi kusomea masomo hayo [ya HKL] ni kwa sababu nilipita manyanyaso toka nikiwa mtoto mdogo. Kwa hiyo, natamani katika maisha yangu kuwasaidia watoto ambao wanapitia haya niliyopitia mimi katika sehemu mbalimbali za dunia.
Wito kwa Serikali ni kwamba inapaswa kufahamu wanafunzi wenye ulemavu tunapitia nini tukiwa shuleni. Kwa sababu, kuna wakati mwingine walimu huamua kuchukua maamuzi bila kuzingatia sheria za watu wenye ulemavu. Kwa hiyo, Serikali kwa upande mwingine ifike sehemu itembelee shule kujua sisi wanafunzi tunaendeleaje kuliko kuweka sheria na kuamini kuwa zinatekelezwa kumbe hazitekelezeki.
Kinachopaswa kufanyika ni walimu hawa tulionao wakaeleweshwa namna ya kuishi na watu kama sisi. Kwa sababu, mimi ninachokiona, kwa mfano, walimu wengi utakuta wanasema ah wewe si unafanana tu na wengine hali uliyokuwa nayo ni ya kawaida. Kwa hiyo, ifike muda Serikali iwaelimishe walimu ili wawe na moyo wa kutusaidia.
Rehema Masanja amesimulia kisa hiki kwa mwandishi wa The Chanzo mkoani Dodoma Jackline Kuwanda. Unaweza kumfikia Jackline kupitia jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na simulizi hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
One Response
Asante kwa makala nzuri yenye kuhamasisha. Kuwa mlemavu wa viungo ama ngozihaukuzuii kuizhi maisha ya kawaida kama wanafamilia wanakupa uhimili. Mara nyingi unatengwa lakini kama wewe nipambanaji, unakuja kuthamaniwa huko mbele. Japokuwa mimi nimeona kuwa maisha ya mlemavu kwa sehemu kubwa ni yenye upweke. Inabidi ajitahidi sana kukidhi mahitaji yake na kwa hiyo inampasa kujitambulisha vitu vingi na kutokuwa na kiburi.