Lindi. Makumi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka kijiji cha Njinjo, tarafa ya Njinjo, kata ya Njinjo, wilayani Kilwa mkoani hapa wanadaiwa kurejesha kadi za chama hicho tawala baada ya Serikali ya wilaya kudaiwa kuhamisha mradi wa ujenzi wa kituo cha afya uliopaswa kujengwa kijijini hapo na kuupeleka kijiji kingine cha Kipindimbi.
Uamuzi wa wanachama hao wanaodaiwa kuwa ni kati ya 200 na 800 ulikuja baada ya hatua ya Mkurungezi wa Halmashauri ya Kilwa Wiston Ngulangwao kuwaomba wanakijiji wa Njinjo kutenga eneo lenye ukubwa wa hekari 25 na kulifanyia kazi kwa kujitolea kwa ajili ya kuliandaa kwa ujenzi wa mradi wa kituo hicho cha afya uliotarajiwa kugharimu Shilingi milioni 250.
Taarifa zinadai kwamba baada ya wanakijiji hao kufanya hivyo, Serikali ya wilaya, kwa kushirikiana kwa ukaribu na ofisi ya CCM wilaya, walichukua uamuzi wa kuuhamishia mradi huo katika kijiji cha Kipindimbi ambacho kinapatikana takriban kilomita tano kutoka kilipo kijiji cha Njinjo.
Wakiongea na The Chanzo mwishoni mwa juma lililopita, wanakijiji wengi wa Njinjo ambao walikiri kurejesha kadi zao za CCM walisema kwamba walilazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kuona chama chao walichokitumikia kwa siku nyingi kinashiriki katika zoezi la kuwakandamiza na kuwanyima stahili yao ya kujengewa kituo cha afya.
Shamsa Ally Nyila ni mkazi wa Njinjo, ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) kijijini hapo. Amesema mpaka wakati wa kuongea na The Chanzo jumla ya wanachama 98 wa CCM kutoka kwenye tawi lake pekee walikuwa wamekabidhi kadi zao kwake.
“[Serikali na CCM] wametutengenezea mazingira magumu kiasi ya kwamba watu [wa vijiji vya Njinjo na Kipindimbi] hatuzikani, hatuangaliani na hatusaidiani,” anasema Shamsa ambaye anadai amekuwa mwanachama wa CCM tangu mwaka 1998. “Tatizo lote hili limeletwa na Serikali, pia nailaumu CCM ambao wote wameshindwa kuja kutotuona. Hawatujali, hawatuthamini na hata kututembelea hawaji.”
The Chanzo haikuweza kufahamu mara moja kwa nini Serikali ya wilaya ya Kilwa ilichukua uamuzi wa kuuhamishia mradi huo kutoka kijiji cha Njinjo kwenda Kipindimbi na kusababisha taharuki kubwa ambayo mpaka wakati wa kuandika habari hii ilikuwa bado haijatulia.
Tulimtafuta Mkurungezi wa Halmashauri ya Kilwa Wiston Ngulangwao ili atueleze uamuzi huo unaweza kuwa ulisababishwa na nini ila baada tu ya kujitambulisha kama anayeongea naye ni mwandishi wa habari alikata simu na juhudi za kuendelea kumtafuta hazikuzaa matunda.
Lakini kwa mujibu wa maelezo ya wanakijiji wa Njinjo, maafisa wa Serikali na CCM wamekuwa wakidokeza kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya kugundulika kwamba katika kijiji hicho hakuna wanachama wa CCM.
Sababu nyengine inayotajwa ni kwamba kijiji hicho hakijawahi kuwa na mafuriko, hali inayokifanya kisikidhi sifa ya kunufaika na mradi huo. Hata hivyo, wanakijiji wa Njinjo wanakana mambo yote haya mawili.
“Njinjo mafuriko yalitokea na kituo cha afya ni haki yetu wana Njinjo [na] kipo kisheria isipokuwa wenzetu wanataka tu kutunyang’anya ili kikajengwe Kipindimbi kwa maslahi yao,” anasema Selemani Mohamedi Mayele, mkazi wa Njinjo na mwanachama wa CCM. “Baada ya kuona hivyo wana Njinjo tukaamua bora tuachane na CCM kutokana na mambo ambayo wanayotufanyia sio mazuri na sio ya kistaarabu.”
Fatuma Abdala Ngoko, mkazi mwengine wa kijiji cha Njinjo na mmoja kati ya wana CCM waliorudisha kadi zao anasema aliamua kuchukua hatua hiyo baada ya maafisa wa chama hicho tawala kudai kwamba Njinjo hakuna wanachama wa CCM.
“Wanasema eti tukijenga kituo cha afya Njinjo CCM tutaipoteza wakati hapa Njinjo ndo kwenye wanachama wengi wa CCM kuliko huko Kipindimbi, Njinjo ndiyo tumeligomboa jimbo kutoka kwa upinzani,” anasema Fatuma, na kuongeza:
“Tumetawaliwa na upinzani kwa miaka 15 tukasema haiwezekani tukambana mpaka CCM tumeipa heshima. Lakini cha kushangaza viongozi wa chama hao ndio waliokaa wakasema kituo cha afya tunaenda kujenga Kipindimbi. Binafsi nikaona hakuna sababu ya kubaki na CCM, nakawarudishia kadi yao.”
The Chanzo ilimtafuta Katibu wa CCM mkoa wa Lindi Barnabas Esau ili kufahamu tuhuma hizi zina ukweli gani na endapo kama anafahamu kwamba baadhi ya wanachama wa chama chake wamekihama chama hicho lakini bila mafanikio yoyote.
Hata hivyo, akijibu swali hilo kwa kituo cha redio mkoani hapa Mashujaa FM, Esau alikanusha taarifa za uwepo wa wana CCM waliorudisha kadi zao, akisema kwamba kilichofanyika ni “mchezo ambao umefanywa na watu wachache kwenye matawi yao wenye lengo la kukichafua Chama cha Mapinduzi.”
Omar Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mtwara anayepatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.