The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Haki ya Kupata Taarifa: Uzoefu wa Mwandishi wa Chombo cha Habari cha Mtandaoni

Wakati tatizo la upatikanaji wa taarifa ni kubwa sana nchini Tanzania, tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya mitandaoni ambao kutokana na kasumba inayozikumba baadhi ya taasisi hawaonekani kama ni waandishi wa habari.

subscribe to our newsletter!

Upo umuhimu mkubwa kwa wadau na taasisi zinazofanya kazi na vyombo vya habari kutambua kwamba vyombo vya habari vya mitandaoni kwa sasa vina umuhimu katika kuhabarisha, kufichua maovu katika jamii, kuelimisha na kuburudisha kama vyombo vingine vya habari ambavyo si vya mitandaoni yaani redio, televisheni na magazeti.

Kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya  wadau na taasisi, zikiwemo hata taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali hasa hasa zilizopo mikoa ya nje na Dar es Salaam, na kwangu nitailenga zaidi mikoa ya kusini, yaani Lindi na Mtwara, kutokuwa na ushirikiano kwa baadhi ya vyombo vya habari vya mtandoni pindi waandishi hao wanapotaka taarifa au kushiriki katika tukio fulani kwa kuona kuwa vyombo hivyo havina umuhimu kwa kuwa ni vya mtandaoni.

Mimi nikiwa kama mhanga kwa kuwa ni mwandishi wa habari wa chombo cha mtandaoni siyo mara moja  wala mbili nimeshawahi kupatwa na changamoto ya kukosa ushirikiano katika utendaji wangu wa kazi kwa baadhi ya taasisi za kiserikali.

Kuna siku nilikuwa nahitaji taarifa inayohusu takwimu za utoaji wa mikopo ya halmashauri katika ofisi ya Afisa Maendeleo ya Jamii inayopatikana kwenye wilaya moja wapo ya mkoa wa Lindi ambayo nisingependa niitaje kwa jina. Nilianza kwa kumpigia simu afisa huyo na kumueleza shida yangu akanielewa na akanipangia muda wa kwenda ofisini kwake ili aweze kunipatia taarifa hizo.

Nilifika katika ofisi yake kwa muda ambao aliniambia nifike hapo. Baada ya kufika tulisalimiana na nikaendelea kujitambulisha na baadae kumuambia anipe hizo taarifa nilizomuomba na hapo ndipo akaanza kuniuliza: “Kwani chombo chako ni cha mtandaoni au cha kawaida?” Nikamjibu cha mtandaoni ambacho tunatoa taarifa zetu kupitia wesite, YouTube, na kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii.

Siwezi kukupa hizo taarifa

Hapo ndipo afisa huyo alianza kunibadilikia na kuanza kuniwekea vikwazo vidogo vidogo na kunieleza: “Basi kama ndio hivyo mimi siwezi kukupa hizo taarifa bila kupata kibali cha Mkurugenzi wa Halmashauri. Kwa hiyo, nenda kapate kibali kwanza kisha nitakupa hizo taarifa.”

Kwa kuwa huo ni utaratibu wa kawaida nilienda kwa mkurugenzi na nikapatiwa kibali ila nilivyorudi tena kwa yule afisa maendeleo akaniambia kwa siku ile yeye hayupo tayari kunipa taarifa zile na akanambia nirudi tena siku inayofuta.

Siku iliyofuata nilienda ofisini kwake tena kwa wakati ambao yeye alisema niende bila kuchelewa lakini sikumkuta. Nilimpigia simu akanambia yeye ametoka hivyo atarudi baadae kama saa tisa na kunikamilishia zoezi langu.

Saa tisa ilifika na nilianza kumpigia simu ili nijue kama yupo tayari kwa zoezi hilo lakini alijibu kwa siku ile isingewezekana, hivyo nimpigie tena simu siku inayofuata ili anipangie muda mwingine wa kunipa hizo taarifa na hapo ndipo nilipogundua kuwa huyo afisa hakuwa tayari kunipa hizo taarifa.

Kama haitoshi kuna wakati huwa nazungumza na baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya mitandaoni waliopo karibu yangu ili kujua kama na wao pia wanapitia changamoto hizi na majibu yao yalikuwa ndio wanapitia.

Kuna siku nilienda kukusanya habari katika hospitali moja hapa Mtwara, nilikuwa nimefuatana na mwandishi mwenzangu anayefanya kazi kwenye chombo kisicho cha mtandaoni, yaani mainstream kama vinavyojulikana kwa kimombo. Katika safari hiyo yeye ndiye aliyefanya taratibu zote za kwenda kuchukua habari pale hospitalini kwa kuongea na wahusika na kueleza nini hasa tulikuwaa tunahitaji.

Ningewaambia tu tupo bize

Tulipofika pale katika mazungumzo ya hapa na pale nilimsikia mmoja wa wahusika wa pale hospitalini akimuambia yule mwandishi mwenzangu kuwa, “Hapa umepata ruhusa hii kwa kuwa wewe tu lakini wangekuwa wengine wa vyombo vya mtandaoni nisingeruhusu kuingia hapa. Ningewaambia tu tupo bize.”

Hapa sasa nikazidi kuona ukubwa wa hii changamoto kwa sisi waandishi wa habari za matandaoni katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.

Ni wakati sahihi sasa kwa wafanya kazi wa Serikali na taasisi binafsi kutambua umuhimu wa vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kuwa huko ndiko dunia na teknolojia inakoelekea tena kwa kasi.

Vyombo vya habari vya mitandaoni vina umuhimu katika kusambaza habari, kufichua maovu katika jamii, kuelimisha na mengine mengi kwa kuwa kupitia vyombo hivi taarifa husambaa kwa haraka na kuwafikia watu ulimwenguni kote tena taarifa hiyo hudumu kwa muda mrefu na kuweza kupatikana  wakati wowote ambao mtu atataka aipate.

Kwa kutambua hayo ndio maana Serikali inavitambua kwa kutoa leseni, sheria na taratibu za kuendesha vyombo hivyo hapa nchini.

Ipo haja pia kwa Serikali kutoa mafunzo kwa wadau au watumishi wa umma ambayo yatawakumbusha watumishi hao kutambua umuhimu wa vyombo vya habari vya mtandaoni na namna ya kufanya navyo kazi katika kuetekeleza majukumu ya kujenga taifa.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoa wa Mtwara. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia omarmikoma@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na siyo lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts