Tanzania hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupanda kwa bei ya vitu. Changamoto hii imechagizwa zaidi na kupanda kwa bei za mafuta. Mjadala kuhusu kupanda kwa bei za mafuta umeendelea bungeni, huku wabunge wakitoa hoja mbalimbali na mipango ya nini kifanyike.
Makala hii inajikita kuangalia hoja zipi ni mbivu, hoja zipi ni mbichi na hali ikoje kwa sasa na tutegeemee nini.
Hoja 1: Kuna harufu za rushwa kwa Wakala wa Ugaizaji Mafuta pamoja na utendaji usio wa uhakika
Tanzania inatumia mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja unaosimamiwa na taasisi ya Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA), ambapo baada ya zabuni kutoka, waagizaji mafuta wa nje na ndani ya nchi hushindana na mwenye bei ya chini katika kusafirisha pamoja na vigezo vingine hupewa zabuni.
Wabunge wameonyesha wasiwasi juu ya taasisi PBPA hasa kuhusiana na rushwa na utendaji wake. Wasiwasi huu unawezekana usiwe wa bure.
Muundo wa kamati inayoangalia na kupitisha tenda za mafuta nchini una mashaka makubwa. Kwa mujibu wa PBPA Manual (Kitabu cha mwongozo cha PBPA), ni watu sita ambao wanahusika na mfumo mzima wa manunuzi ya mafuta kupitia zabuni za PBPA. Watu hao ni mwenyekiti, wafanyakazi wawili wa PBPA, pamoja na wawakilishi watatu kutoka kwenye kampuni za mafuta nchini. Wawakilishi watatu kutoka kwenye makampuni na wawakilishi wa PBPA huteuliwa na Mtendaji Mkuu wa PBPA.
Ripoti ya Msimamizi na Mkaguzi Mkuu wa hesbau za Serikali (CAG) ya mwaka 2020 iliainisha mambo mengine kadhaa kuhusu Wakala.
Kwanza, kitabu cha mwongozo kinachotumika katika kufanya kazi yote ya PBPA, ikiwemo taratibu za manunuzi ya mafuta, hakikuwahi kuidhinishwa na mamlaka husika. PBPA walimueleza CAG kwamba walipeleka kitabu hicho kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa ajili ya kukipitia ili kupeleka kwenye uidhinishaji lakini hakikurudishwa.
Kitabu hiko kimekua kikitumika tangu mwaka 2017, ikimaanisha kwamba kitabu hicho hakina nguvu ya kisheria.
Pamoja na uchanga wa PBPA ambapo imeanza rasmi utendaji mwaka 2016, ripoti ya CAG ilibainisha pia kuwa PBPA haikuwahi kufanyiwa ukaguzi wa mahesabu tangu ilivyoanza. Pia, PBPA ilitumia Shilingi bilioni tatu kwa matumizi mbalimbali bila kufuata taratibu za manunuzi, huku watendaji wakijitetea kuwa walifanya hivyo kutokana na udogo wa taasisi ambapo hakuna watu wa kutosha na matumizi kuwa machache.
Mashaka zaidi kuhusu utendaji wa PBPA
Baadhi ya maamuzi ya manunuzi ya mafuta yanayofanywa na PBPA yanaacha maswali. Kwa mfano, mwezi Julai 2021, PBPA ilizuia zabuni za mafuta ya dizeli ya takribani tani 83,145 kwa ajili ya kugombaniwa na makampuni ya ndani pekee.
Kampuni ya Sahara Tanzania Limited ilishinda kwa gharama za usafirishaji za Dola za Kimarekani 47.63 kwa tani moja ya mafuta, hii ikimaanisha mzigo mzima uligharimu shilingi bilioni tisa. Lakini upande wa pili katika zabuni ambazo makampuni yote ya nje na ndani yaliruhusiwa kugombea gharama za kuleta mzigo wenye ujazo sawa sawa ilikua ni Shilingi bilioni 4.5.
Hii ikimaanisha kulikua na ongezeko la takribani Shilingi bilioni 4.5 katika gharama za usafiri zilizotokana na maamuzi ya BPA. Zabuni ya kuleta petroli iliyozuiliwa kwa makampuni ya ndani na kupewa GBP Tanzania ilikua na gharama za juu za takribani Shilingi bilioni 1.6 katika usafirishaji.
Kwa Agosti 2021, jumla ya tani 205,459 za dizeli zilizuiwa tena kwa ajili ya kushindaniwa na makampuni ya ndani. Makampuni ya ndani, ikiwemo Sahara Tanzania Limited, Orxy Oil, Hass Petroleum na GBP Tanzania yalishinda zabuni hizi, ambapo kwa ujumla wake bei ya usafiri ilizidi kwa takribani Shilingi bilioni 8.9 kulinganisha na zabuni zingine zilizowekwa katika ushindani wa jumla.
Tayari kuanzia Juni 2021 hali ya mfumuko ilianza kuongezeka. Ongezeko lolote katika gharama za kuagiza mafuta inamaanisha bei itapanda na mfumuko wa bei kuendelea kuongezeka. Katika hali kama hii ilitegemewa PBPA kuzingatia hilo na kuhakikisha mafuta yanaagizwa kwa bei shindani zaidi, hili halikuzingatiwa.
Gharama za usafirishaji kuongezeka
Wakati bado tukitafakari hali ya ongezeko la mafuta, inawezekana ikawa bado machungu yakawa yanakuja mbeleni. Katika hali ya kushangaza gharama za usafirishaji kwa mafuta yanayotakiwa kuingia nchini mwezi Mei 2022 zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 300.
Hii ni kwa mujibu wa matangazo ya kushinda kwa zabuni yaliyotangazwa na PBPA ambapo inaonekana jumla ya tani 567,527 za mafuta zimeagizwa, huku bei ya usafirishaji wa mafuta hayo ikiwa ni kati ya dola za Kimarekani 88 na dola za Kimarekani 145.6 kwa kila tani moja ya mafuta. Hii ni bei kubwa zaidi y ausafirishaji kutokea, kwa mwaka uliopita bei kubwa ya usafirishaji iliyowahi kurekodiwa ilikua ni Dola za Kimarekani 53 kwa tani moja ya mafuta.
Hii ikimaanisha kusafirisha mafuta yote kipindi cha Mei 2022 itagharimu takribani Shilingi bilioni 153 kama gharama za usafiri, ongezeko la takribani Shilingi bilioni 112 kama tukitumia bei ya wastani ya usafirishaji kulingana na bei zilizotumika kati ya Januari 2018 mpaka Aprili 2022.
Ikimaanisha zaidi ya Shilingi bilioni 112 itaenda kutoboa mifuko ya watu kama ongezeko la bei. Kupanda huku kwa gharama za usafirishaji, ukijumlisha na kuendelea kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia, inamaanisha hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Pamoja na vita vya Ukraine, hili ongezeko la bei ya kusafirisha mafuta ni la kihistoria, pengine maswali ya ziada yanahitajika kwa PBPA kuelewa nini kimetokea kabla ya hatua zingine zozote kuendelea.
Hoja 2: Pamoja na vita, kupanda kwa bei ya mafuta kumesababishwa na mfumo wa uagizaji mafuta unaozuia fursa ya kununua mfuta ya bei rahisi kwa njia za panya
Hoja hii imewasilishwa na Mbunge wa Gairo Ahmed Shabiby pamoja na Mbunge wa Geita Joseph Kasheku (Msukuma), wote kutoka chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hoja ya Mbunge Shabiby na Msukuma kwamba kuna fursa ya mafuta ya bei rahisi katika deep sea au njia za panya, ni hoja yenye ukakasi mkubwa. Mafuta yanayozungumziwa hapa ni mafuta ya soko haramu, au black market. Mafuta haya huuzwa na nchi zilizowekewa vikwazo (kupitia mawakala), maharamia, wachuuzi wa mafuta ya magendo, wababe wa vita (war lords) nakadhalika.
Hii si njia sahihi kwa nchi kutegemea, na hata ikitokea kampuni ikagundulika inanunua mafuta kwa njia hii, nchi ina jukumu la kuacha kufanya naye kazi. Sehemu kubwa ya mapato ya namna hii pia hutumika kufadhili uhalifu kama ugaidi na uasi. Hivyo, kuweka nchi katika hatari ya kujikuta katika vikwazo.
Kwa hiyo, siyo sahihi kuutazama mfumo wa ununuaji kwa pamoja kama ndio umesababisha ongezeko la bei. Mfumo huu umekuwa ukiendana sawa na ongezeko la bei katika soko la dunia. Mafuta yanapopanda na nchini hupanda na yanaposhuka hushuka. Kwa mfano, mnamo Aprili 2020, mafuta yalivyoshuka kwa rekodi ya kipekee hata nchini mafuta yalishuka kwa rekodi.
Mfumo huu umeweza kuhakikisha usalama wa mafuta nchini. Bei inaweza kupanda kutokana na bei ya dunia lakini kusiwe na uhaba. Pia, ubora wa mafuta umeongezeka kutoka 2012 ambapo mfumo ulianza, changamoto kubwa kwa sasa iko kwenye taasisi inayosimamia huu mfumo.
Hoja 3: Serikali iingilie kati kupanda kwa bei ya mafuta
Kwa kuangalia hali ya mfumuko unavyoendela, na kwa kuwa kuna uwezekano wa bei kuendelea kupaa, wazo la Serikali kufanya kitu lina uzito mkubwa. Hata hivyo, umakini unahitajika katika kufanya maamuzi kwa kuangalia uhitaji wa sasa na wa baadae.
Kuna uamuzi wa kuweka ruzuku kama walivyofanya Kenya, au kuamua kusitisha ukusanyaji wa sehemu ya kodi kwa muda fulani.
Hata hivyo ni muhimu sana kwa hoja mbalimbali za Wabunge hasa kuhusu uwazi na utendaji mzima wa PBPA zikaangaliwa kwa ukaribu, ili kuhakikisha hakuna matundu ambayo fedha za umma zitakuwa zikivuja.
Tony Alfred K can be reached through tony@thechanzo.com or on Twitter through @tonyalfredk