The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Madereva wa Malori Tanzania Waeleza Chanzo cha Migomo ya Mara kwa Mara

Madereva hao wanalalamikia hatua ya Serikali kuingilia kati ili masilahi yao yaimarishwe.

subscribe to our newsletter!

Songwe. Madereva wa malori nchini Tanzania wametaja masilahi duni kama sababu ya msingi ya wao kugoma mara kwa mara, wakisema wanafanya hivyo kuikumbusha Serikali madhila wanayokumbana nayo kwenye kazi yao hiyo muhimu ya usafirishaji wa bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi nyengine.

Baadhi ya madereva hao wanaopatikana katika mji mdogo wa Tunduma mkoani hapa, ambapo ni mpakani na nchi jirani ya Zambia, walielezea uzoefu wao wa kufanya kazi kama madereva wa malori pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa mahojiano na The Chanzo mnamo Aprili 18, 2022.

Hatua hiyo ilikuja kufuatia hali ya kujirudia rudia kwa migomo ya madereva hao mpakani hapo huku The Chanzo ikitaka kufahamu ni nini haswa kinaweza kuwa ni chanzo cha hali hiyo isiyoridhisha kwa ustawi wa taifa na ni nini kinaweza kufanyika ili kuepusha hali hiyo isijurudie.

Kutokana na mazungumzo hayo, mbali na masilahi duni, madereva pia wametaja sababu nyengine zinazochochea migomo: usumbufu wa askari wa usalama barabarani; kuwekwa ndani kwa zaidi ya masaa 24 baada ya kukamatwa; kutozwa ushuru na kodi katika kila halmashauri wanayopita; na kutakiwa kulipa fedha za maegesho kiasi cha Kwacha 50,000 wanapokuwa nchini Zambia.

“Maslahi ndiyo tatizo kubwa sana, ndiyo maana migomo inakuwa [ya] mara kwa mara, hususani mikataba siyo mizuri,” anasema Shaaban Omari Mponda, anayeendesha lori kutoka Tanzania kwenda Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). “Mishahara ya dereva iko chini, dereva analipwa Sh150,000. Sasa mshahara wa Sh150,000 utamsaidia nini, si ni sawa sawa na mshahara wa mfanyakazi wa ndani tu?”

Mponda anadai kwamba baadhi ya makampuni hayalipi kabisa mishahara kwa madereva wao lakini bado watu wanafanya kazi kwani mtaani hakuna kazi na wanatafuta namna yoyote itakayowawezesha kuishi.

“Serikali inatakiwa iingilie kati hili suala,” Mponda, baba wa mtoto mmoja, ameieleza The Chanzo. “Binafsi huwa nasafiri na mtungi wa gesi, unga na mchele ili nikifika sehemu nipike chakula kupunguza gharama za maisha.”

Mwinyi Ibrahim ni dereva mwengine wa lori ambaye maoni yake yanafanana na yale ya Mponda, akienda mbali zaidi kwa kusema kwamba madereva wa malori nchini Tanzania wamegeuzwa wafungwa huku mamlaka husika zikiwa hazijali kile wanachofanyiwa.

“Tunakuwa kama wafungwa,” anasema Ibrahim, baba wa watoto watano kwenye mahojiano maalum na The Chanzo. “Yaani dereva wa Kitanzania anakuwa kama mfungwa. Mimi nakwambia ukweli. Matajiri wamepewa nguvu kubwa kuliko madereva. Inakuwa ngumu zaidi kwa Serikali kuweza kuwanyang’anya ile nguvu [na kufanyia kazi madai ya madereva].”

Kwa mujibu wa madereva hawa, kichowasukuma kushuka kwenye malori yao na kugoma ni kushindwa kwa mamlaka husika kufanyia kazi malalamiko yanayoibuliwa na madereva kila wanapopata fursa ya kukutana na mamlaka husika.

“Kwa hiyo, tunahisi labda njia sahihi ya kuwakumbusha ni kuendesha mgomo,” anasema Musa Hamad, dereva wa lori kati ya Tanzani na Zambia. “Malalamiko yetu kadhaa hayajafanyiwa kazi: mishahara duni; kuungwa kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF); na ukosefu wa fedha za matibabu. Malalamiko yote haya yamefika serikalini na bungeni. Lakini ambacho tumekuwa tukiambulia ni ahadi hewa.”

The Chanzo ilimtafuta Katibu wa Madereva Malori Taifa Gerson Bwimile ili kufahamu endapo wao kama chama wana mikakati yoyote ya kuweza kusaidia wanachama wao kuondokana na changamoto hizi.

Hata hivyo, Bwimile alisema kwamba hawezi kuongelea masuala hayo kwenye simu na alipoombwa miadi ya kukutana kwa ajili ya mahojiano ya ana kwa ana alishindwa kutoa ushirikiano.

Omary Mgumba ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe ambaye ameieleza The Chanzo kwamba Serikali inafahamu malalamiko ya madereva hao na imekuwa ikichukua juhudi za kuongea na waajiri kuangalia namna wanavyoweza kuboresha masilahi ya madereva wao.

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts