Wingu la hasira, chuki na manung’uniko limetanda wilayani Kilosa, mkoani Morogoro. Dalili zote za mvua ya visasi, mapigano na damu zimetawala. Rasharasha, manyunyu ya hasira kwa kiasi chake imeshaanza kuhisiwa katika baadhi ya maeneo.
Haihitaji kuwa mtabiri, mbashiri, msoma nyota au nabii mwenye maono kuweza kuliona hili. Haihitaji uwe mdadisi sana, mtaalam, afisa mpelelezi au kachero au mwanausalama, kuweza kulibaini hili.
Inakuhitaji utenge tu muda wako na upige kambi wilayani humo, hata kwa nusu saa tu, nawe utaweza kuliona hili katika nyuso zao. Inakuhitaji uzungumze na wana Kilosa, hata pasipo kufika huko, nawe utalisikia hili katika sauti zao.
Inakuhitaji uweze kupita kando tu ya barabara zao, na pasipo shaka utaweza kuinusa harufu ya fukuto la chuki na hasira. Inakuhitaji uwe mtu, ambaye hisia zako hazijapigwa ganzi, kuweza kuwaelewa na kuelewa misingi ya makasiriko yao.
Janga kuu la ardhi
Wilaya hii imegubikwa na changamoto na kadhia nyingi. Kubwa kuliko, hata hivyo, wakazi wa wilaya hiyo wanakabiliwa na janga la ardhi. Janga hili siyo la leo wala jana. Janga hili ni la muda mrefu. Hili ni, unaweza kusema, ni Janga Kuu!
Wanakijiji wilayani humo wanakabiliwa na uhaba wa ardhi ya kutumia. Uhaba huo wa ardhi ya kutumia unawapunguzia uwezo wa kufanya shughuli zao, hususani shughuli za kilimo na ufugaji. Jambo hili linawanyima fursa ya kuweza kujipatia mahitaji yao ya msingi na kipato, ambavyo vyote, kwa pamoja, vitawawezesha kujikimu.
Ni muhimu, hata hivyo, kuelewa kuwa wana Kilosa wanaouhaba wa ardhi ya kutumia na siyo kweli kwamba kuna uhaba wa ardhi wilyani humo. Tatizo, kwa hiyo, siyo ardhi bali kuporwa kwa maeneo yao ya asili.
Yapo maeneo yaliyokuwa yanatumiwa na wazee wao, na hata baadhi ya wazee wapo hadi hii leo, maeneo haya siyo sehemu ya maeneo ambayo yanaelezwa kugaiwa kwa wawekezaji.
Maeneo yao ya asili hivi sasa yanaelezwa kuchukuliwa na mamlaka za Serikali kwa hoja ya kwamba yalikuwa ni maeneo ya wawekezaji, ili hali hayako ndani ya mipaka ya maeneo ya wawekezaji. Hali hii inaelezwa kuwepo katika vijiji chungu nzima wilayani humo, iwe ni katika kijiji cha Kimamba, Mbwade au Madoto.
Maeneo mengine, kwa mfano katika kijiji cha Mambegwa wilayani humo, yanaelezwa kuchukuliwa na mamlaka nyinginezo kama Jeshi la Magereza, ili hali maeneo hayo hayako ndani ya mipaka ya ardhi ya magereza.
Maeneo mengine yanachukuliwa na watu binafsi, wengi wakiwa ni watu wenye uwezo wa kifedha na wenye nafasi katika mamlaka au wenye ushawishi kwa watu wenye mamlaka.
Watu hao hutumia mamlaka hiyo hiyo katika kuwapora na kuwadhibiti wanakijiji dhidi ya haki yao ya msingi na ya asili katika ardhi yao. Kutokana na hali yao ya unyonge unaosababishwa hususani na kipato chao duni, wanakijiji hao, kwa idadi yao kubwa, wameishia kuporwa maeneo yao hayo ya asili.
Wananchi na maeneo ya uwekezaji
Kutokana na kukua kwa idadi ya watu na mifugo na haswa kuongezeka kwa wingu la uporaji wa maeneo ya asili ya wananchi ambayo hayakuwa ni makubwa hata hivyo, wananchi hao hao wamejikuta wakiwa na uhaba wa maeneo ya kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walilazimika kuanza kutumia maeneo ambayo awali yanaelezwa kutengwa kwa ajili ya uwekezaji lakini yakaishia kutelekezwa.
Aghalabu inaelezwa kuwa wananchi hawa walivamia kiholela maeneo hayo yaliyotelekezwa, ili hali sio kweli. Jambo la kustaajabu sana ni kwamba wananchi wa Kilosa ni watiifu mno kwa taratibu na sheria, licha ya kwamba taratibu na sheria hizo hizo haziko upande wao.
Baada ya kubaini kuwa wana uhaba wa maeneo ya kufanya shughuli zao, wananchi hawa waliwasilisha maombi na mapendekezo katika mamlaka mbalimbali na kutokana na jitihada zao za awali walipatiwa maeneo kwa ajili ya matumizi yao.
Utaratibu uliwekwa juu ya matumizi ya hayo maeneo waliyopatiwa na kisha wao kama wananchi watautii utaratibu huo.
Hivi sasa, wananchi wanalalamika kwamba utaratibu wao waliojiwekea na uliopata baraka za mamlaka husika umetupiliwa mbali. Mamlaka ya wilaya pamoja na Wizara ya Ardhi zimewageuka na zimekacha kutambua na kuzingatia utaratibu na makubaliano ya awali, ambayo yalikuwa mahususi kwa eneo kwa eneo.
Badala yake, mamlaka hizo zimekuja na utaratibu mpya, ambao kwa kiasi kikubwa unawakandamiza wanakijiji wengi wa wilaya hiyo, kwani utaratibu huo mpya umeweka msisitizo zaidi kwenye mfumo wa ukodishaji wa ardhi kwa wananchi kwa fedha kuu kuu na hivyo kuwatenga wananchi wa hali ya chini walio wengi.
Ulinzi dhidi ya uvamizi
Kilio kikuu cha wananchi kuhusiana na ardhi wilayani humo ni waweze kupata ulinzi dhidi ya kuvamiwa na kuporwa maeneo yao ya asili. Pia, wanataka kuwekwa utaratibu wa haki na utakaozingatia haki, usawa na utu wao katika maeneo yanayoelezwa kuwa ya wawekezaji.
Ni dhahiri hatua hizi hazitaweza kulimaliza tatizo lote, lakini walau litatoa na kuhakikisha hali ya utulivu katika jamii, katika kipindi cha kuweza kutafuta, kuunda na kujenga suluhu ya kudumu, kuhusiana na ardhi wilayani humo na kote nchini.
Hata hivyo, wana Kilosa wenyewe wanaamini, pasipo shaka, janga hili litaendelea kudumu kwa sababu ya mapuuza ya watawala. Wanaeleza kuwa ni kupuuzwa kwao ndiko kunafanya janga hili kuwa sugu.
Baadhi yao wanaamini, pengine mapuuza hayo ya watawala yanasababishwa na uhalisia wa kwamba siyo wao (watawala), wala ndugu zao wa karibu na wa damu, watakao athirika moja kwa moja pale ambapo janga hilo litazua majanga.
Manung’uniko na malalamiko makubwa mengine ya wana Kilosa yanahusu hali ya watawala wilayani humo, na hata katika Serikali Kuu, kutozingatia na kushughulika na wananchi wa wilaya hiyo.
Wengi wanaeleza kudharauliwa na kudhihakiwa na watawala, hususani pale wanapokuwa wanawasilisha malalamiko, madai na mapendekezo yao mbali mbali. Kauli za kebehi na maudhi zimekuwa ni ada, jambo ambalo wanaeleza kuwa wamelazimika kulizoea, ili hali hawafurahishwi nalo.
Ikiwa malalamiko yao yanapokelewa na dhihaka na kejeli; utu wao unadharauliwa; madai yao yanapuuzwa; na iwapo watawala wamekuwa ni watu mahiri wa kutoa kauli za hadaa kwa wananchi wa wilaya hiyo; hivyo watu hawa hawana budi kujiuliza wafanye nini, wanapaswa kufanya nini?
Ikiwa watu wawategemeao kushughulika na masuala yanayowahusu na yanayohusu ustawi wao, watu hao hao ndiyo mwiba na ndiyo tatizo, kama siyo sehemu ya tatizo, hivyo kilio chao wakipeleke wapi? Je, wanapaswa kuyangoja majaliwa au mpango wa Mungu (kudra) au suluhu ya kutoka mataifa ya mbali?
Chuki, hasira katika ardhi
Hali ya uvumilivu inaelekea kuwatoka watu wa Kilosa. Wamechoka kudharauliwa, kupuuzwa na kudhihakiwa. Isivyo bahati, kwa kuwa wingu la hasira na chuki limewazonga, wananchi wa wilaya hiyo wanaanza kunyoosheana vidole wakishtumiana kuwa miongoni mwao ndiyo maadui.
Wanaanza kupakana na kushtumiana kwa mifumo yao ya maisha, huyu mkulima na huyu mfugaji; wanaanza kufukua makaburi ya ukabila, huyu Msukuma, Mchaga, Mmasai, Mkinga, Mbena; wanaanza kudhihakana kwa asili zao, huyu wakuja na huyu mzawa.
Hali hii inajengeka na fukuto linazidi kukua. Linaanza kushirikishwa na kuzungumzwa kwenye kaya zao; watoto wanaanza kufundishwa na kupandikizwa vimelea vya ubaguzi na chuki. Hali inazidi kujengeka.
Punde si punde, nazo siku zaja, mbingu zitafunguka, nazo zitakuwa ni mbingu za mapigano kati ya wanajamii ambao kimsingi wote ni wahanga. Wakati huo adui atakuwa yuko pembeni ametulia tu.
Je, ndipo hapo tunataka kufika ili mamlaka iamke na ishtuke kisha itume jeshi lake la kutuliza ghasia wakati ghasia hizi zingeweza kudhibitiwa na kuepukika tangu mwanzo?
Msanii nguli wa muziki wa Reggae Bob Marley katika wimbo wa Them Belly Full (Matumbo Yao Yamejaa), anaimba na kueleza kuwa kuna kundi la watu wachache walioshiba na kusaza na upande wa pili kuna kundi la watu wengi waliogubikwa na janga la njaa.
Msanii huyo mwanamapinduzi, anaendelea, katika wimbo huo huo, kutahadharisha kuwa kundi la watu wenye njaa ni kundi la watu wenye hasira.
Wimbo huu hauzungumzi mahususi kuhusu njaa ya mlo. La hasha! Wimbo huu unazungumza kuhusu njaa ya haki, ustawi, maendeleo na uhuru.
Nao watu wa Kilosa wanakabiliwa na njaa kali. Njaa yao ni ya ardhi, hususani haki yao katika ardhi. Haki yao na madai yao yazingatiwe!
Jasper “Kido” Sabuni ni mchambuzi wa masuala ya kijamii. Anuwani yake ya barua pepe ni kidojasper@gmail.com. Anapatikana pia Twitter kama JasperKido. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.