Ningeomba nitumie safu hii kutoa ufafanuzi mdogo kuhusiana na kile ambacho kimekuwa kikiripotiwa hivi karibuni kuhusiana na mgogoro unaoendelea huko wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha. Ni muhimu kuelewa kwamba hapa kuna migogoro miwili ambayo watu wamekuwa wakiizungumzia kama vile ni mgogoro mmoja, kitu ambacho nadhani siyo sahihi kwani migogoro hii inahitaji aina tofauti za utatuzi.
Tunahitaji kufanya utenganisho kati ya Ngorongoro na Loliondo. Ngorongoro ni wilaya, kwamba kuna wilaya inaitwa wilaya ya Ngorongoro. Ndani ya wilaya ya Ngorongoro, kuna eneo la uhifadhi linaloitwa Eneo la Uhifadhi la Ngorongoro, au Ngorongoro Conservation Area (NCA) kwa kimombo. NCA inachukua takribani asilimia 59 ya wilaya nzima ya Ngorongoro.
Eneo linalobaki limegawanyika kimsingi katika maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza ni pori tengefu la Loliondo na eneo la pili ni pori tengefu la Lake Natron. Sasa tuna mgogoro wa Ngorongoro, kwa upande mmoja, na huu uliojitokeza juzi ni mgogoro mwengine, ule wa Loliondo.
Migogoro yote hii miwili ipo kwa muda mrefu. Mgogoro wa Loliondo ni mgogoro unaotokana na sababu za kimatumizi za ardhi ambayo kuna mseto wa kazi zinazofanyika katika eneo la Loliondo.
Na mgogoro mkubwa huko ulianza miaka ya 1992, 1993 na 1994 ambapo kampuni ya uwindaji ya Otterlo Business Corporation (OBC), ambayo inamilikiwa na mwana wa mfalme wa UAE, iliingia mkataba na Serikali ya Tanzania kupata leseni ya uwindaji ya miaka 20.
Sasa eneo la pori tengefu la Loliondo, kisheria, ni eneo ambalo linaruhusu matumizi mseto ya ardhi, kwa maana ya kwamba shughuli za uwindaji zinaruhusiwa na shughuli za binadamu, ikiwemo ufugaji, zinaruhusiwa.
Na katika eneo hilo Serikali ilianzisha vijiji na vijiji hivi vinamiliki ardhi kihalali ndani ya eneo la pori tengefu la Loliondo. Moja wapo ya vijiji hivyo ni hivyo vijiji 14 ambavyo kwa sasa vipo kwenye mgogoro na Serikali.
Sasa kwa muda mrefu wanakijiji hawa wamekuwa wakipata madhila kutokana na shughuli za uwindaji zinazofanywa na kampuni ya OBC ingawa kuna wahusika wengine waliondani wanaofanya shughuli pia za utalii ndani ya vijiji hivyo au maeneo hayo.
Umiliki halali wa ardhi
Wanakijiji hawa ni wamiliki halali wa ardhi za vijiji vyao kwa sababu ni vijiji vilivyo anzishwa kihalali na vina vyeti vya ardhi ya kijiji vilivyotolewa na Wizara ya Ardhi vikionyesha umiliki wa mkutano mkuu wa kijiji kama mdhamini wa ardhi ya vijiji hivyo kwa niaba ya wanakijiji wote. Lakini kwa upande mwengine pia, eneo hilo limebaki kuwa pori tengefu.
Sasa huyu muwindaji anaingia kuwinda katika maeneo ya vijiji na ndipo hapo mgogoro unapotokea, ndio mgogoro uliokuwa kwa miaka yote.
Mnamo mwaka 2009 wakati sheria ya wanyama pori inaundwa, mjadala huu ulijitokeza na wadau mbalimbali tuliokuwa tunachangia juu ya mabadiliko ya sheria hiyo na katika sheria hiyo tulitanabaisha si Loliondo tu au pori tengefu la Lake Natron bali maeneo yote yenye mapori tengefu hayafai kuendelea kuwa na hadhi hiyo kwani yanashughuli kubwa za wananchi kuliko kuwa mapori ya wanyama na kuwa vitalu vya uwindaji.
Sheria ikaweka bayana kwamba waziri husika pindi sheria hiyo itakapoanza kutumika miezi 12 akakague mapori tengefu yote yaliyopo nchini Tanzania, ambapo ni mapori kama 41, na baada ya hapo apendekeze zipi zinafaa kuendelea kuwa na hadhi ya mapori tengefu.
Tangu mwaka huo mpaka leo hii waziri mwenye dhamana na maliasili hajafanya hilo na matokeo yake kumeendelea kuwa na migogoro katika mapori tengefu haya kwa sababu shughuli za wawindaji zinaingiliana na shughuli za wananchi ambazo kwa kiasi kikubwa ndizo zinazofanyika sasa kwenye maeneo hayo kwani uwepo wa wanyama umepungua na ni haki yao hawa wananchi kutumia hayo maeneo.
Na sheria ilitamka bayana kwamba endapo waziri mwenye dhamana wakati anaangalia hayo maeneo akikuta ardhi inayotumika na wananchi haruhisiwi kuiingiza ardhi hiyo katika hadhi ya pori la akiba.
Kwa hiyo, unaanza kuona kwamba mvunjifu wa kwanza wa haki za watu ni Serikali ambayo ameshindwa kutekeleza sheria iliyoitunga yeye mwenyewe na hivyo inapelekea mgogoro.
Kwa sababu kama waziri angekagua hayo maeneo angelikagua pia pori tengefu la Loliondo na kuhitimisha kwamba eneo hilo kwa sasa, kwa vijiji vilivyopo na shughuli wanazofanya, haistahili kuendelea kuwa pori tengefu wala halipaswi kuwa pori la akiba na hivyo wananchi wangeachiwa.
Wamaasai kama wahifadhi wa asili
Suala la pili ni suala linaloendana na uhifadhi na hasa kinachotokea huko Loliondo – nitazungumzia zaidi Loliondo kwa sababu nadhani Ngorongoro tunahitaji kuwa na mda wake – wote tunafahamu kwamba wafugaji jamii ya Wamaasai ni wahifadhi wa asili na wahifadhi wa kwanza.
Sasa kinachotokea katika vijiji hivyo, kwa sababu nimepita na nimefanya kazi katika hivyo vijiji, kutokana na shughuli za utalii zinazoendelea Serengeti na shughuli za uwindaji zinazoendelea katika pori tengefu la Loliondo, wanyama wemeondoka katika hayo maeneo na kuingia katika maeneo ya ardhi za vijiji ambazo zinatumika kwa ufugaji na mambo mengine ya asili.
Kuna maboma ya jando wanawekwa huko na vitu vingine ili kupata hifadhi kutokana na uwindaji na shughuli za vurugu zinazoendelea Serengeti. Mwindaji OBC, pamoja na kampuni nyingine zinazofanya kazi ya uwindaji, zinakwenda kuwinda hao wanyama kwenye maeneo ambayo ni maeneo ya vijiji ambako kuna wanyama.
Na sasa hivi huo ukanda unaotambaa kutoka mpaka wa Kenya na kushuka mpaka kijiji cha Arash ambayo Serikali inataka kuuchukua ina aina nyingine ya uhifadhi. Kwa mfano, kijiji cha Ololosokwan ni mfano bora kabisa wa vijiji ambavyo vinaweza kufanya uwekezaji kwa kujitegemea wenyewe na linaweza kuwa ni mfano Tanzania na pengine hata mfano Afrika.
Uzoefu wa Ololosokwan
Kijiji hiki, kwa mfano, kina ekari 20 ambazo zipo mpakani mwa Serengeti na Loliondo na eneo hilo ni shamba ambalo lina wanyama.
Miaka ya 1990, shamba hilo lilikuwa linamilikiwa na kampuni inaitwa CC Africa baadae wanakijiji wakaja kugundua kwamba ardhi waliyopewa hati hiyo kampuni ni ardhi ya kijiji chao na wao kipindi kile walikuwa na hati miliki kabla hawajapewa cheti cha ardhi cha kijiji.
Wanakijiji wakaenda wakapata cheti cha ardhi cha kijiji kikionesha shamba hilo liko ndani. Wakaenda Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kuishtaki hiyo kampuni.
Hiyo kampuni kipindi hicho ilikuwa umiliki wake unabadilika kutoka CC Africa kwenda AndBeyond. AndBeyond hawakutaka huo mgogoro. Kwa hiyo, wakaenda mahakamani wakakubaliana wamalize hiyo kesi nje ya Mahakama.
Sharti la wanakijiji cha Ololosokwan kwa AndBeyond ilikuwa ni kampuni hiyo iende kwa Kamishna wa Ardhi ili afute ile hati waliyokuwa nayo ili ardhi ibaki kwa wanakijiji halafu kampuni iende kuongea na wanakijiji upya.
AndBeyond wakafuta hati yao halafu wakarudi wakakaa na wanakijiji wakaingia mkataba wa matumizi ya pamoja ya ardhi ya kijiji, kwa maana AndBeyond inajenga kambi, itakuwa inatembeza watalii kwa kupiga picha na wanakijiji wakati wanahitaji malisho watakuwa wanafanya malisho.
Wakaunda kamati ya pamoja wakawa wanatumia pamoja lile eneo na wanatumia mpaka sasa.
Waliingia mkataba mara ya mwisho mwaka 2015. Kijiji kilikuwa kinalipwa dola laki moja na kumi na tano kwa mwaka mbali na mahitaji mengine ambayo yanatolewa kijijini, hasa katika shule na kila kitu na hawa wanakijiji wamekuwa wakitumia hizo fedha kwa ajili ya kusomesha watoto wao. Hiki ni kijiji ambacho ukienda leo nusu ya vijana wao wana shahada, nyingi zao zikiwa ni za sheria.
Mwaka 2015 wakati wanahangaika kusaini huo mkataba na Serikali inachelewesha, akiwemo Waziri wa Ardhi aliyepita William Lukuvi pamoja na Kamishna wa Ardhi wa Kanda ya Kaskazini, viongozi wa kijiji walisema kuna vijana 56 ambao wapo kwenye vyuo vya ufundi wanatakiwa kulipa ada tusiposaini huu mkataba hawataenda kwa sababu sera ya kijiji inatumia hizo hela kwa elimu, mtoto akimaliza darasa la kwanza anasomeshwa mpaka Chuo Kikuu na kijiji.
Serikali inazitaka hizo fedha
Kinachotokea hivi sasa ni nini? Kinachotokea ni kwamba Serikali ya Halmashauri ya Ngorongoro inazitaka hizo fedha na kumekuwa na shinikizo miaka yote wachukue hizo fedha.
Fedha kutoka NCAA za wanavijiji ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ambazo zilikuwa wanapewa wananchi walishinikizwa watoe kwa Halmashauri! Na sasa hivi pesa ambazo zilitakiwa wapewe wananchi wa vijiji vilivyo ndani ya hifadhi zinapelekwa Halmashauri ya Ngorongoro! Madiwani na Wazee wa Baraza la Wafugaji walikubali hili jambo kwa shinikizo
Kwa hiyo, tatizo hapa ni ulafi wa Serikali wa kutaka kuwanyang’anya wananchi ardhi zao ili waingize mapato kwenye Serikali Kuu na si kwa ajili ya kufurahisha wananchi.
Na ndipo hapo tunarudi kwenye hoja kwamba eneo hili linataka kutengwa pengine hawa watu wamepewa za mfukoni kwa sababu kama Serikali ingetaka kufanya uhifadhi wa kweli ingejiridhisha kwanza na haya maeneo kama sheria inavyoagiza. Haijafanya hivyo na inamuda huo na ilikuwa na muda huo na ilitakiwa ifanye Tanzania Bara nzima.
Kwa nini wanataka huo ukanda wa kilomita za mraba 1,500 kwa kutumia nguvu? Ni kwa sababu kama Serikali ingefanya uhakiki ingegundua hawawezi kukipata, hawawezi kumpatia mwekezaji. Ni muhimu basi kwa Serikali kusitisha zoezi hili kwani zoezi hilo linalenga kuwanyang’anya wananchi ardhi yao.
Jambo ambalo ningependa kutahadharisha ni kwamba tukiwa tunachangia kuhusiana na suala hili tusihusishe dini au sehemu anayotoka Rais Samia Suluhu Hassan na mpango wa Serikali huko Ngorongoro. Katika suala la uhifadhi nchini Tanzania, tangu hifadhi hizi kubwa zinaanzishwa mwaka 1951, hakuna rais aliyewahi kutenda haki kwenye eneo la ardhi.
Tatizo hili ni la kimfumo na kuendelea kuhusisha Uislamu, au Uzanzibari, nahofia kwamba tunaweza kuyatenga makundi haya kwenye harakati zetu za kupinga dhuluma inayoendelea kufanywa dhidi ya wenyeji wa Ngorongoro.
Emmanuel Mvula ni Msemaji wa Fedha na Uchumi wa chama cha ACT-Wazalendo ambaye amekuwa akitafiti mgogoro wa Loliondo kwa takriban miaka 15. Anapatikana kupitia emmanuel.mvula@yahoo.com au Twitter kama @Immamvula. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
3 responses
Asante Emmanuel Mvula umeeleza vizuri sana kuhusu migogoro inayoendelea Wialaya Ngorongoro
Asante sana kwa ufafanuzi wa kina ndugu Mvula.
Kaka Mvula. Asante sana kwa andiko hili.