The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Headlines

Habari Kubwa Leo Aprili 24, 2024
Habari Kubwa Leo Aprili 23, 2024
Habari Kubwa Leo Aprili 22, 2024
Wawili Wahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa Kwa Kumuua Bodaboda Mtwara
Habari Kubwa Leo Aprili 15, 2024
Habari Kubwa Leo Arili 12, 2024
Habari Kubwa Leo Aprili 9, 2024
Habari Kubwa Leo Aprili 8, 2024

Live Reporting

Habari Kubwa Leo Aprili 24, 2024

Watanzania 17,850 wakabidhiwa nishani za miaka 60 ya muungano

Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano hapo Ijumaa ya Aprili 26, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan leo Aprili 24, 2024, amewatunuku nishani za miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Watanzania 17,850, zoezi ambalo limefanyika Ikulu, jijini Dodoma. 

Nishani alizowatunuku ni pamoja na nishani ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nishani ya mwenge wa uhuru daraja la pili, nishani ya utumishi uliotukuka, nishani ya utumishi mrefu na tabia njema, nishani ya utumishi mrefu pamoja na nishani ya kumbukumbu ya muungano. 

Baadhi ya watu waliokabidhiwa nishani hizo ni pamoja na Hayati Rais John Pombe Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Majeshi, Jacob Mkunda pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura. 

Sambamba na hilo, Rais Samia amezindua vitabu viwili vya muungano, kikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ofisi ambayo imekuwa ikishughulikia masuala ya muungano hapa nchini. 

Akizungumza mara baada ya kuzindua vitabu hivyo, Rais Samia amewataka Watanzania kudumisha amani na mshikamano wa taifa la Tanzania, kufanya kazi kwa bidii na kudumisha uzalendo kama sehemu ya kuwaenzi waasisi wa muungano huu. 

LHRC: Hali ya haki za binadamu mwaka 2023 ilidorora ikilinganishwa na mwaka 2022

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimebainisha kuwa hali ya haki za binadamu kwa mwaka 2023 ilidorora ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2022 kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za kiraia na kisiasa.  

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 24, 2024, wakati kituo hicho kilipokuwa kinazindua ripoti yake ya 22 ya haki za binadamu kwa mwaka 2023, zoezi ambalo limefanyika kwenye makao yake makuu yaliyopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam. 

Akizitaja haki kuu ambazo zilikiukwa sana kwa mwaka 2023, afisa utafiti kutoka LHRC, Fundikila Wazambi, amezitaja kuwa ni haki ya kuishi, uhuru dhidi ya ukatili, haki ya usawa mbele ya sheria, haki ya kuwa huru na salama pamoja na uhuru dhidi ya utesaji. 

Wazambi ameendelea kubainisha kuwa, kundi la watoto ndiyo limeonekana kuwa waathirika wakubwa wa ukiukwaji wa haki zao kwa asilimia 45 wakifuatiwa na wanawake ambao ni waathirika kwa asilimia 30, viwango ambavyo vimepungua ukilinganisha na mwaka jana. 

Kwa upande wa makundi ya wazee na wanaume, kiwango cha ukatili kimeonekana kuongezeka, ambapo wazee ni asilimia 12 kutoka asilimia 10 ya mwaka 2022 na wanaume pia ni asilimia 10 kutoka asilimia sita ya mwaka 2022. 

Ripoti hiyo kwa sasa inapatikana bure kupitia tovuti ya LHRC.  

Maombi ya leseni za madini 227 yafutwa 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kwamba Serikali, kupitia Tume ya Madini, imefuta jumla ya maombi ya leseni 227 ambayo yamekosa vigezo vya kuendelea kufanyiwa kazi.

Hayo ameyasema leo Aprili 24, 2024, jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari. 

Mavunde amesema kuwa maombi hayo yamefutwa kutokana na sababu ya kutolipiwa ada stahiki za maombi kwa mujibu wa sheria pamoja na kukosa nyaraka zinazotakiwa kuambatanishwa na maombi hayo. 

Ndani ya miezi miwili hii, Serikali itakuwa imefuta jumla ya maombi 2,875 kwa sababu Machi 22, 2024, Serikali ilitangaza kufuta maombi na leseni za utafiti 2,648 ambayo yalibainika kuwa na makosa mbalimbali. 

Nchini Tanzania, sekta ya madini ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023, migodi ilifanya manunuzi ya dola za Kimarekani bilioni 1.6, ambapo dola bilioni 1.4 zilihusisha kampuni za Kitanzania na hivyo kufanya zaidi ya asilimia 86 ya manunuzi yote ya migodi katika mwaka huo yawe yamefanywa na Watanzania.

Habari Kubwa Leo Aprili 23, 2024

Barabara ya Jangwani, Dar es Salaam yafungwa kutokana na mafuriko

Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) amesema kuanzia leo Aprili 23, 2024, amesitisha mabasi yake kupita katika barabara ya Jangwani jijini Dar es Salaam mara baada ya barabara hiyo kufungwa kutokana na mafurikio yaliyotokea jijini hapa.

Taarifa iliyotolewa na DART leo Aprili 23, 2024, imesema kuwa huduma ya usafiri wa mabasi yanayotoka Kimara hadi Kivukoni na Gerezani zitaishia katika kituo cha Magomeni Mapipa. 

Aidha, taarifa hiyo imesema huduma za mabasi zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa njia ya Morroco kwenda Kimara na eneo la katikati mwa jiji kwa njia ya Muhimbili na Gerezani. 

Eneo la Jangwani ni eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na changamoto ya mafuriko mara tu mvua kubwa zinaponyesha. 

Suluhu ya changamoto hiyo inatarajiwa kuwa ni mradi wa ujenzi wa Bonde la Msimbazi ulioanza mwezi huu kwa hatua za awali. Mradi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miaka mitano na utagharimu Shilingi bilioni 675. 

Ujenzi wake utahusisha miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, ujenzi wa karakana ya mwendokasi eneo la Ubungo Maziwa, ujenzi wa daraja la Jangwani, ujenzi wa busatani ya jiji na uendelezaji wa maeneo ya makazi na biashara.

Wabunge Zanzibar: Muungano unatupatia kila raha, Serikali itatue kero zinapojitokeza

Baadhi ya wabunge wanaotoka Zanzibar wameeleza kuwa muungano uliopo hivi sasa kati ya Tanganyika na Zanzibar una manufaa makubwa lakini wameitaka Serikali iendelee kutafuta suluhu za changamoto zinazojitokeza. 

Hayo yameelezwa leo Aprili 23, 2024, bungeni, jijini Dodoma, wakati wabunge hao walipokuwa wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. 

Akizungumzia moja ya suala ambalo amehitaji litafutiwe ufumbuzi, mbunge wa viti maalumu anayewakilisha Unguja Kaskazini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Sada Mansoor, amesema ni usumbufu mkubwa kwa wananchi wa pande hizo mbili wanapotoka upande mmoja na kuingia upande wa pili kupitia bandari ya Dar es Salaam na ile ya Zanzibar. 

Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar unatarajiwa kutimiza miaka 60 hapo Aprili 26, 2024. Muungano huo umekuwa ukikabiliwa na kero kadhaa ambazo wadau mbalimbali wamekuwa wakishinikiza zitafutiwe ufumbuzi. 

Machi 26, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, alisema kuwa kati ya kero 25 za Muungano zilizokuwepo mwaka 2010, Serikali imefanikiwa kutatua kero 22. 

Bandari zisizo rasmi 69 zabainika kuleta athari za kimazingira

Jumla ya bandari zisizo rasmi 69 zimekaguliwa kwa mwaka 2023/2024 na kubaininika kuleta athari za kimazingira ikiwemo kumwaga mafuta ya taa, taka ngumu na kutiririsha maji taka kwenda kwenye maziwa, bahari na uharibifu wa bayoanuai unaotokana na uondoaji wa uoto wa asii.

Haya yameelezwa leo Aprili 23, 2024, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, wakati akiwasilisha hotuba ya ofisi hiyo kuhusu mapitio ya utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka 2023/2024 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/2025.

Jafo amesema kukabiliana na changamoto hizo, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilizishauri mamlaka zinazohusika na masuala ya bandari kufanya tathmini za mazingira, kutoa elimu kwa wadau, kusimamia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, kuhamasisha jamii kuhifadhi mazingira, kuimarisha miundombinu ya bandari na kubadili maeneo ya kuendeshea bandari hizo.

Kwa mujibu wa Jafo, mamlaka zilizoshauriwa kufanya tathmini hiyo ni Mamlaka ya Bandari Tanzania na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania.

Habari Kubwa Leo Aprili 22, 2024

CHADEMA yaanza wiki ya maandamano nchi nzima

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeanza wiki ya maandamano ya amani yatakayofanyika mikoa mbalimbali hapa nchini kuanzia leo Aprili 22,  hadi 30,2024 ikiwa ni utekelezaji wa azimio la Mtwara.

Maandamano hayo yameanzia Bukoba, mkoani Kagera leo tarehe 22 Aprili 2024, ambapo mwenyekiti wa Chama Taifa  Freeman Mbowe ameongoza maandamano hayo ikiwa ni awamu ya kwanza kati ya awamu mbili zitakazofanyika.

Kituo kinachofuata ni mkoa wa Shinyanga ambapo maandamano yatafanyika Wilaya ya Kahama kesho tarehe 23 Aprili 2024 huku ikielezwa kuwa Tundu Lissu yeye ataongoza maandamano mkoani Arusha tarehe 25 Aprili 2024. 

Lengo la CHADEMA kuandamana ni kupinga miswada ya uchaguzi iliyopitishwa bungeni hivi karibuni, kuishinikiza Serikali irejeshe mchakato wa Katiba Mpya pamoja kuitaka Serikali ishughulikie masuala mbalimbali yanayosababisha kuongezeka kwa gharama za maisha.

Makonda afika Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewasili kwenye ofisi za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa na Kamati ya Maadili.

Makonda ameitikia wito wa kufika mbele ya kamati hiyo kwa barua aliyoandikiwa Aprili 16, 2024 huku sababu za kuitwa kwake zikiwa hazijawekwa wazi.

Awali, Makonda alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Aprili 20, 2024 kabla ya kusogezwa mbele na kupangwa kufanyika leo Jumatatu, Aprili 22, 2024.

Lakini, wito huo huenda unahusishwa na kauli ya Makonda aliyoitoa wakati wa kumbukumbu ya miaka 40 ya kifo cha Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine ambapo Makonda alidai kuwa viongozi wakiwemo mawaziri wamekuwa wakilipa watu kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mitandao ya kijamii.

Makonda alitoa onyo kwa viongozi hao akisema kama wakiendelea atawataja hadharani na kwamba, hayuko tayari kuona Rais Samia akitukanwa.

Mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya Zanzibar kutaifishwa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCE), imetangaza kutaifisha mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh15.3 bilioni kuwa mali ya Serikali.

Akizungumza kuhusu kutaifishwa kwa mali hizo ofisini kwake leo Jumatatu  Aprili 22, 2024 , Kamishna Kanali Burhani Zuberi Nassoro amesema dawa hizo ziliingizwa nchini na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya.

Kamishna Nassoro amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Salehe Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir wote wakazi wa Chukwani, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Watuhumiwa hao wamebainika kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya Zanzibar, Tanzania Bara, Afrika, Asia, Ulaya na Marekani. Hata hivyo ameleeza kuwa iwapo kuna mtu hajaridhika na tamko hilo anaweza kwenda mahakamani ndani ya siku 30 kuanzia leo.

Wawili Wahukumiwa Kunyongwa Hadi Kufa Kwa Kumuua  Bodaboda Mtwara

Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara imewahukumu kunyongwa  hadi kufa, Badilu Mussa Hannogi [25] na Salum Ally Mauji [24]  wote wakazi wa Mtwara, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Mohamed Juma Mohamed ambaye alikuwa muendesha bodaboda hapa Mtwara.

Kesi hiyo namba 60/2022 imetolewa hukumu Aprili 15, 2024 na jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Matha Mpaze.

Kwa mujibu wa mahakama ni kwamba mnamo tarehe Januari 15, 2021 majira ya jioni washtakiwa hao walimkodi marehemu  Mohamed Juma Mohamed awapeleke nyumbani kwao wakitokea maeneo ya Cocobeach Manispaa ya Mtwara Mikindani, wakiwa njiani walianza kumshambulia hadi kumuua na mwili kuutupa porini kisha kuchukua pikipiki yake.

Baada muda, Jeshi la Polisi lilichunguza tukio hilo na kuwakamata Badilu na Salum wakituhumiwa kufanya tukio hilo ambapo Februari 2022, walifikishwa makamani kwa mara ya kwanza.

Habari Kubwa Leo Aprili 15, 2024

Ripoti 21 za CAG zatua bungeni leo

Ripoti 21 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazohusu ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa Mwaka 2022/2023 zimewasilishwa bungeni leo Aprili 15, 2024, na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.

Miongoni mwa ripoti hizo zilizowasilishwa ni ripoti ya ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali Kuu, taarifa za fedha za mamlaka za Serikali za mitaa na taarifa za fedha za miradi ya maendeleo. 

Nyingine ni taarifa za fedha za mashirika ya umma, ufanisi na ukaguzi maalumu, mifumo ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), upatikanaji wa huduma za afya ya akili na udhibiti wa vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya vya umma.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, aliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 28, 2024, ambapo alisema katika mwaka huo ametoa jumla ya hati 1,209 za ukaguzi. Kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni hati 1197, sawa na asilimia 99. Hati zenye shaka ni tisa, sawa na asilimia 0.7. Hati mbaya ni moja, sawa na asilimia 0.1, pamoja na hati nyingine mbili ambazo CAG alishindwa kutoa maoni.

Kichere pia aliyataja mashirika ya umma kadhaa yaliyotengeneza hasara, akitaka hatua zichukulie ili hali hiyo isijirudie. Mashirika hayo ni kama vile Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Mawasiliano (TTCL), Shirika la Reli (TRC), Kampuni Tanzu ya Mafuta (TanOil ) na Shirika la Posta.

Makonda kuwataja mawaziri wanaoendesha mpango wa kumtukana Rais Samia? 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, leo Aprili 15, 2024, alitarajiwa kuwataja baadhi ya mawaziri aliodai kuwa wanawalipa watu kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan, lakini mpaka dakika hii alikuwa bado hajafanya hivyo. 

Makonda alisema hivyo Aprili 12, 2024, wakati wa hafla ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, iliyofanyika Monduli Juu, mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wakuu mbalimbali, akiwemo Rais Samia mwenyewe. 

Makonda, anayejitambulisha kama mtoto wa pekee wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, alisema kuwa anawafahamu mawaziri hao na endapo wataendelea kufanya hivyo angeyaweka majina yao hadharani leo hii.  

Hii isingekuwa mara ya kwanza kwa Makonda kuwaweka hadharani watu anaodai wanafanya makosa fulani. Mwaka 2017, wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, aliyaweka hadharani majina ya watu aliodai kuwa wanajihusisha na biashara ya madawa ya kulevya. 

Hata hivyo, wakati huu imekuwa tofauti kwani tuhuma zake alizelekeza kwenye Baraza la Mawaziri ambalo kwa mujibu wa katiba ndilo ambalo linaunda Serikali. 

TBS yawataka wananchi wafuate maelekezo ya matumizi ya ‘Energy Drink’

Shirika la viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa kwenye vinywaji ili kuepuka madhara ya kiafya ambayo yanatokana na kutofuata maelekezo  wakati wa matumizi ya vinywaji hivyo.  

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2024, jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka TBS, Lazaro Msasalaga, amesema kuwa shirika hilo limekuwa likidhibiti viwango vya viambata vinavyotakiwa kuwekwa kwenye vinywaji kama ‘Energy Drink’ na pombe kali, lakini watumiaji wake ndiyo hunywa vibaya.  

Akitolea mfano kuwa, maelekezo yaliyotolewa na wazalishaji ni kuwa mtu anywe chupa moja ya ‘Energy Drink’ kwa siku, agizo ambalo anadai halifuatwi na wengine wanatumia kinywaji hicho pasipo kula, hali ambayo hupelekea athari za kiafya kama vile mgonjwa ya moyo na figo.

Habari Kubwa Leo Arili 12, 2024

Watu 39 wapoteza maisha kutokana na mafuriko Pwani, Morogoro na Arusha

Watu 39 wamepoteza maisha katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Arusha kutokana na mvua kubwa zilizonyesha. Mvua hizo pia zimewaacha maelfu ya watu bila makazi katika maeneo hayo pamoja na kuharibu mashamba ya chakula na miundombinu.  

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa ya Aprili 12, 2024, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, katika mkoa wa Morogoro idadi ya watu waliopoteza maisha ni 28 na wengine watano ni kutoka mkoani Pwani. 

Nako mkoani Arusha, mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, ameeleza kuwa mpaka sasa watu sita wamepoteza maisha kutokana na athari za mvua zilizonyesha kuanzia Aprili 8 hadi Aprili 12, 2024. 

Kutokana na matukio hayo, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa wote waliokumbwa na mafuriko alipokuwa akishiriki misa maalumu ya miaka 40 ya kumbukumbu ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, leo Aprili 12, 2024, akisema kuwa Serikali itakuchukua hatua zote kurejesha utulivu katika mikoa iliyoathirika.

Rais Samia: Hayati Sokoine atakumbukwa kwa uwajibikaji kupitia matendo yake 

Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine, hautasaulika hapa nchini kwa sababu alikuwa ni kiongozi aliyesisitiza uwajibikaji kupitia mienendo na matendo yake kwenye uongozi.

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 12, 2024, aliposhiriki misa maalumu ya miaka 40 ya kumbukumbu ya kifo cha kiongozi huyo, tukio ambalo limefanyika Monduli Juu, mkoani Arusha, eneo ambalo lilikuwa ndiyo nyumbani kwake enzi za uhai wake. 

Rais Samia ameeleza kuwa funzo hilo kuu kutoka kwa Sokoine linatokana na umahiri wake katika kazi tatu alizozisimamia kipindi cha uongozi wake ambazo ni kazi ya kusimamia ukombozi kusini mwa Afrika, vita ya Tanzania na Uganda na suala la operesheni uhujumu uchumi. 

Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika vipindi viwili  Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na Februari 24, 1983 hadi Aprili 12, 1984. Aliwahi pia kuwa Waziri wa Ulinzi (1972-1977) na Waziri Mdogo wa Mawasiliano, Uchukuzi na Kazi (1967-1972). 

Sokoine anakumbukwa sana katika mapambano yake dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi miaka 1980 na alifariki dunia Aprili 12, 1984, kwa ajali ya gari eneo la Wami Dakawa mkoani Morogoro akitokea Dodoma kwenye kikao.

Mradi wa ujenzi wa Bonde la Msimbazi kuanza Aprili 15, 2024

Serikali imesema kuwa mradi wa ujenzi wa Bonde la Msimbazi unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) utaanza Aprili 15, 2024, kwa hatua ya awali ya ubomoaji wa nyumba zilizopo katika eneo la Jangwani, kandokando mwa mto Msimbazi. 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12, 2024, jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema kuwa TARURA itaanza zoezi la ubomoaji kwa kuzingatia makubaliano yake na wakazi wa eneo hilo, kwamba nyumba zao zilifanyiwa tathimini, wakalipwa fidia, ndipo nyumba husika zitavunjwa. 

Kwa mujibu wa Matinyi hadi kufikia Februari 29, 2024, TARURA ilikuwa imeshaingiza malipo ya fidia ya kiasi cha Shilingi bilioni 52.61 kwenye akaunti za wamiliki wa nyumba 2,155 kati ya wamiliki 2,329 walioandikishwa kwenye daftari la kwanza. 

Mradi wa Bonde la Msimbazi unatarajiwa kuchukua miaka mitano kutoka sasa na utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 675. Ujenzi huo utahusisha miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, ujenzi wa karakana ya mwendokasi eneo la Ubungo Maziwa, ujenzi wa daraja la Jangwani, ujenzi wa busatani ya jiji na uendelezaji wa maeneo ya makazi na biashara.