Search
Close this search box.

Dodoma. Benki ya Dunia imeanza ziara ya kutembelea miradi mbalimbali hapa nchini, lengo likiwa ni kufanya tathimini ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na benki hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema miradi wanayoitembelea inatokana awamu ya pili ya mkopo wa gharama nafuu uliotolewa na benki hiyo. 

“Pamoja na mambo mengine ni  kwa ajili ya kujenga vituo jumuishi vya mahakama. Tunaposema vituo jumuishi maana yake inakuwa na mahakama ya mwanzo, mahakama ya wilaya , mahakama ya hakimu mkazi na pia mahakama kuu mpaka hata mahakama ya rufani,” amesema Prof. Elisante.

Benjamin Ndazi kutoka Benki ya Dunia amesema, wamekuwa na utaratibu wa kawaida kutembelea miradi ambayo wanaitekeleza kwa ushirikiano wa Serikali, lengo kubwa ni kupima utekelezaji wa malengo ya mradi. 

“Tutakuwa hapa kwa majadiliano ya takriban wiki nzima. Lakini pia kuangalia maeneo ambayo mradi unafanya vizuri. Na yale maeneo ambayo bado yanachangamoto basi kwa pamoja kuweza kujadiliana namna bora ya kutatua hizo changamoto . Kusudi tuweze kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.