Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kilichoketi visiwani Zanzibar leo kimemtangaza kada wake mkongwe, Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa chama hiko kufutia kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Daniel Chongolo Novemba 30, 2023.
Dk Nchimbi anakuwa Katibu Mkuu wa 12 wa chama hiko tangu kuasisiwa kwake mwaka 1977 baada ya vyama vya ukombozi vya TANU na ASP kuungana.
Kisiasa Dk Nchimbi ana uzoefu mkubwa na CCM kwani amekuwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kitaifa kuanzia Mwenyekiti wa UVCCM taifa akiwa na umri wa miaka 27 mwaka 1998, na Mjumbe wa NEC katika vipindi tofauti tofauti.
Nafasi nyingine ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bunda kuanzia mwaka 2003 mpaka 2005, Mbunge wa Songea Mjini kuanzia 2005 mpaka 2015, Naibu Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na Waziri wa mambo ya ndani mpaka mwaka 2013 alipotenguliwa katika nafasi hiyo na Rais Kikwete.
Kabla ya uteuzi huu wa sasa, Dk Nchimbi alikuwa Balozi katika nchi za Brazil tangu mwaka 2016 na baadaye Misri mwaka 2022 kabla Rais Samia kumuita nchini Agosti 2023.
Dk Nchimbi anakabiliwa na kazi kubwa ya kukiandaa chama chake katika chaguzi zijazo pamoja na vuguvugu la mageuzi linaloendelea ambapo hivi karibuni limepelekea joto la kisiasa kupanda baada ya baadhi ya wadau wakikosoa miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa Bungeni Novemba 10, 2023.