The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Serikali kukopa fedha NMB kwa ajili ya kununua mabasi 100 ya mwendokasi 

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema kuwa Serikali imepanga kufanya mazungumzo na benki ya NMB kwa ajili ya kuona ni kwa namna gani wanaweza kupata fedha zitakazotumika kununua mabasi ya mwendokasi takribani 100 ili kukabiliana na upungufu mkubwa uliopo sasa. 

Mchechu ameyasema hayo leo Julai 15, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akizungumza na wahariri, ambapo ameeleza kuwa mabasi hayo ambayo wanategemea kuyapata ndani ya kipindi cha miezi sita toka watakapo toa oda hadi kuwasili, yatakuwa yakifanya kazi kwenye njia kuu peke yake. 

Akizungumzia kuhusu kampuni za usafirishaji kwenye mradi huo, Mchechu amesema kwamba ipo haja ya Serikali kuongeza idadi ya kampuni hizo ili zifanye kazi kwa ushindani na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.  

Mradi wa mwendokasi ulianza kufanya kazi mwaka 2016. Katika siku za hivi karibuni mradi huo umekuwa ukidaiwa kushindwa kuwahudumia ipasavyo wakazi wa jiji lenye watu wengi zaidi la Dar es Salaam, hali ambayo imekuwa ikipelekea usumbufu mkubwa. 

Mpaka mwezi Oktoba mwaka jana mradi huo ulikuwa una mabasi 210, lakini kati ya hayo, mabasi 140 pekee ndiyo yanayotoa huduma.

Wanaharakati waiburuza Serikali mahakamani kuzimwa kwa mtandao uchaguzi 2020

Mwanaharakati Kumbusho Dawson Kagine ameishtaki Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu kwa kitendo chao cha kuzima mtandao wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. 

Akizungumza na waandishi wa habari wakili anayesimamia kesi hiyo, Tito Mgoti, amesema kuwa kesi hiyo ni ya kikatiba na imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kwa lengo la kuiomba mahakama iliangalie suala hilo kwa namna ambavyo Serikali ilikiuka haki za watu.

Magoti ameeleza kwamba mteja wake anadai tukio lile lilikiuka baadhi ya haki zake ambazo zimetajwa katiba, ikiwemo haki ya kupata, kutoa na kusambaza taarifa. Lakini vilevile, haki ya kujumuika na wengine, haki ya kushiriki katika masuala ya umma na vilevile Serikali imevunja wajibu wake kwa mujibu wa ibara ya 26 ambao ni wajibu wa kulinda na kutii na kuheshimu sheria za nchi.

Magoti ameongeza kuwa mteja wake anaitaka mahakama itamke kwamba tukio hilo halikuwa lakufaa, lilikuwa ni kinyume cha misingi ya utawala bora na lilivunja haki zake. Lakini pia, anaitaka Serikali ikiri kwamba haitarudia tena kufanya hivyo. 

Mashirika ya umma kuanza kuweka wazi taarifa zao za fedha 

Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, leo Julai 15, 2024, ametangaza kuwa mashirika yote ya umma nchini yataanza kuchapisha wazi taarifa zao za kifedha ili kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji kwenye mashirika hayo katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kufanya mageuzi kwenye mashirika hayo.

Mchechu ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, kwenye kikao kilichofanyika hapa jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa kwa sasa taasisi za kifedha na kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa pekee ndizo zinazotakiwa kuchapisha taarifa za kifedha. 

Hivyo, kwa sasa agizo hilo jipya litakwenda kwenye mashirika yote ambayo yanaendeshwa na Serikali. 

Mchechu akasisitiza kwamba umma lazima uarifiwe kuhusu utendaji wa kifedha wa taasisi zote za umma, ambapo uwazi huo utaweka wazi ni taasisi zipi zitalipa gawio kwa Serikali na zipi hazitafanya hivyo.

×