The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tanzania yathibitisha askari wake watatu kupoteza maisha DRC

Tanzania imethibitisha kupoteza askari watatu na wengine watatu kujeruhiwa katika misheni ya kuimarisha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Taarifa hiyo imetolewa leo Aprili 9, 2024, siku moja tangu Sekretarieti ya SADC ilipotoa taarifa yake ikieleza kuwa vifo hivyo vilitokana na bomu ambalo liliangukia karibu na kambi waliyokuwa wakiishi askari hao. 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax, ameviambia vyombo vya habari kuwa, askari waliofariki ambao majina yao hakuyaweka wazi watapumzishwa kwa heshima kwa kuzingatia taratibu za kijeshi.

Mwaka 2023, SADC iliazimia kupeleka Misheni ya Ulinzi wa Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kushughulikia masuala muhimu yanayoathiri amani na utulivu nchini humo kufuatia mapigano ya muda mrefu dhidi ya makundi ya waasi yenye silaha.

PPRA yaokoa fedha za umma kiasi cha Shilingi Bilioni 16.27

Katika mwaka wa fedha 2021/22 na 2022/23, Mamlaka ya Udhibiti  wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imefanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 16.27, hii ni baada ya kufanya uchunguzi kwa zabuni zilizotekelezwa.

Akiongea na waandishi wa habari leo Aprili 9, 2024,  jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri  na Kujenga Uwezo kutoka PPRA, Mhandisi Amini Mcharo, amesema kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi bilioni 13.83 zilitokana na kuingilia kati kwa mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato.

Aidha, kiasi cha Shilingi bilioni 2.44  kilirudishwa na wasambazaji wa bidhaa na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na taasisi nunuzi.

PPRA ilianzishwa kutokana na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004. Mamlaka hii ina dhamana ya kuhakikisha taasisi za umma zinasimamia haki, ushindani na uwazi kwenye suala la manunuzi ya umma. 

Serikali yatangaza kufunguliwa dirisha la usajili wa MAKISATU

Serikali leo Aprili 9, 2024, imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la usajili wa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU).

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema mashindano hayo yatahusisha wabunifu kutoka vyuo vya elimu ya juu, taasisi za utafiti na maendeleo, vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, shule za msingi, shule za sekondari na wabunifu kutoka mfumo usio rasmi. 

Mkenda ameongeza kuwa washindi 10 kwa kila kundi watashiriki katika maadhimisho ya ngazi ya kitaifa, huku washindi wa jumla wakiingia katika mpango wa Serikali wa uendelezaji na ubiasharishaji wa bunifu zao.

Dirisha la usajili wa washiriki wa mashindano hayo limefunguliwa rasmi leo tarehe Aprili 9, 2024 na litafungwa tarehe Mei 8, 2024.