The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kundi la Ramadhan Brothers kutoka Tanzania laibuka mshindi wa ‘America Got Talent’ 

Wasanii wa sarakasi kutoka Tanzania Ibrahim Ramadhan na Fadhili Ramadhan wanaounda kundi la The Ramadhan Brothers wameibuka washindi wa mashindano ya kusaka vipaji ya ‘America’s Got Talent Fantasy League’. Ushindi huo wameupata  usiku wa kuamkia leo huko nchini Marekani na kujinyakulia kitita cha dola za Kimarekani 250,000 pamoja na tuzo ya kwanza ya msimu huu wa mashindano hayo. 

Wakizungumza mara baada ya kutangazwa washindi ndugu hao wawili hawakusita kuelezea furaha yao na kumshukuru kila mmoja aliyefanikisha safari yao ya kufikia hapo. 

Naye Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na amewapongeza Watanzania hao akieleza kuwa safari yao inaendelea kudhihirisha kuwa juhudi, nidhamu, kujituma na kujiamini ni nguzo muhimu kufikia mafanikio. Na hatua waliyoifikia ni ya mfano kwani inazidi kulitangaza vyema taifa la Tanzania.  

Maonesho ya wanasarakasi hao hutumia balansi ya mikono na kichwa kuonyesha sanaa yao. Walishiriki katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 kwenye msimu wa 18 wa ‘America’s Got Talent’ wakashika nafasi ya tano. Wamewahi pia kushiriki kwenye mashindano kama hayo nchini Ujerumani, Slovakia, Ufaransa, pamoja na Australia.

Dawa za kulevya zenye uzito wa kilogramu zaidi ya milioni moja zilikamatwa 2023

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini  (DCEA) imetangaza kuwa kwa mwaka 2023 ilifanikiwa kukamata aina mbalimbali za dawa za kulevya kwenye maeneo tofauti tofauti zikiwa na uzito wa takribani kiligramu milioni 1.97.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 20, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama, ambapo amesema kuwa kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka huo mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini. Kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Mhagama ameendelea kueleza kuwa katika kipindi hicho watuhumiwa 10,522 wamekamatwa kwa kujihusisha na biashara hiyo haramu ambapo kati yao wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821 na  jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi zikiteketezwa.

Tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya limekuwa likiwaathiri vijana wengi hapa nchini. Takwimu kutoka kwenye vituo vya tiba saidizi kwa waraibu wa kutumia dawa za kulevya zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba hiyo kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915.

CHADEMA waendelea na maandamano Mbeya

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe leo ameongoza maandamano ya amani katika jiji la Mbeya. Mbowe aliambatana pamoja na viongozi mbalimbali wa chama hicho ukiwa ni mwendelezo wa maandamano yaliyopangwa kufanyika nchi nzima.

Lengo la maandamano hayo ni kupinga miswada ya uchaguzi iliyopitishwa bungeni hivi karibuni. Malengo mengine ni kuishinikiza Serikali irejeshe mchakato wa Katiba Mpya pamoja kushughulikia masuala mbalimbali yanayosababisha kuongezeka kwa gharama za maisha.

Maandamano hayo yanatarajiwa kuendelea kwenye jiji la Arusha tarehe Februari 27, 2024 mara baada ya kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza. 

Wakizungumza katika maandamano hayo, wananchi na wakazi mbalimbali wa Mbeya wamedai kupanda kwa kiasi kikubwa kwa gharama za maisha ndiyo sababu iliyowafanya leo wajitokeze kuandamana kwa lengo la kuishinikiza Serikali iwasikilize.