The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali yasema sanamu ya Nyerere ya AU imefanana naye kwa asilimia 92

Serikali ya Tanzania imesema kuwa sanamu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyozinduliwa Februari 18, 2024 kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyopo  Addis Ababa, Ethiopia imefanana naye kwa asilimia 92.

Ufafanuzi huu umetolewa leo Februari 22, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaibu Mussa, kufuatia ukosoaji mkubwa ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii ukieleza kuwa sanamu hiyo haifanani na kiongozi huyo halisi. 

Balozi Shaibu amesema sanamu hiyo imetengenezwa kwa kumzingatia Mwalimu Nyerere wa Miaka 60 hadi 80 wakati alipokuwa na nguvu za kupambana kusaidia kupatikana kwa uhuru na maendeleo katika nchi za kusini mwa Afrika. 

Lakini pia mmoja wa watoto wake Mwalimu Nyerere ambaye ni Madaraka Nyerere amethibitisha kuwa sanamu hiyo inafanana na muonekano halisi wa baba yake. 

Ujenzi wa sanamu hiyo umefanyika nchini Ubeligiji ukifadhiliwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Serikali ya Tanzania iliunda kamati maalumu ya wataalamu iliyohusisha ndugu kutoka kwenye familia ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.

Bashe kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria kunusuru upungufu wa sukari

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema mwezi wa sita mwaka huu atapeleka muswada mabadiliko ya Sheria ya Sekta ya Sukari bungeni kwa ajili ya kuondoa urasimu kwenye biashara ya sukari ili wazalishaji wa ndani waweze kushindana na makampuni na wazalishaji wengine kutoka nje ya nchi.

Akiongea na waandishi wa habari leo Februari 22, 2024 Ikulu Dar es Salaam Bashe amefafanua kuwa atachukua umamuzi huo kutokana na kitendo cha Serikali kuwalinda wazalishaji wa ndani wa sukari kwa zaidi ya miaka 20 hivyo anadhani kwamba kwa sasa muda umekwisha na tayari watakuwa wameshakua kibiashara. 

Wakati mpango huo ukiendelea kwa sasa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa sukari hali ambayo imewafanya watumiaji wake kuipata kwa bei ya juu. Kwa takribani miezi mitatu iliyopita bei ya sukari imepanda kutoka Shilingi 2,800 kwa kilogramu moja hadi shilingi 4,000 mpaka 5,000 katika maeneo tofauti ya nchi. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka 2022/2023 yalipanda kutoka tani 490,048 hadi tani 555,000 mwaka 2023/2024.Wakati huo huo Tanzania ilizalisha tani 460,048 mwaka 2022/2023 huku matarajio yakiwa kuzalisha tani 560,000 mwaka 2023/2024.

Tofauti na matarajio ya kuzalisha ziada, Serikali imeeleza kuwa kuna upungufu wa uzalishaji wa sukari nchini hali ambayo imedaiwa kutokana na athari za mvua za el nino zilizonyesha na kuathiri uvunaji wa miwa. 

Simalenga adai haoni sababu ya kuomba msamaha kwa waandishi wa habari

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga, ametetea uamuzi wake wa kuwatimua waandishi wa habari katika kikao muhimu cha mashauriano cha wilaya kilichofanyika Februari 19, 2024 na kusema kuwa haoni sababu ya kuomba msamaha kwa sababu hakufanya kosa lolote bali alikuwa anafuata miongozo.

Katika mahojiano na kituo cha redio cha Nyanza FM Simalenga alisema kumekuwa na upotoshaji wa kile kilichotokea katika mkutano huo. Na si kweli kwamba aliwafukuza waandishi hao lakini kwa uungwana aliwataka waondoke kwani miongozo ya mikutano hairuhusu uwepo wao.

Kujitetea kwa Simalenga kunatokana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa waandishi wa habari, vyama vyao na watetezi wa uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania, ambao wamelaani tabia yake, ambayo wanafikiri inahatarisha usalama na uhuru wa waandishi wa habari.

Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Simiyu ilitoa tamko kali mnamo Februari 20, 2024, siku moja baada ya tukio hilo kutokea ikitangaza kwamba wanachama wake hawataandika chochote kuhusu mkuu huyo wa wilaya hata kulitaja jina lake kwenye vyombo vya habari hadi mamlaka za juu ziwahakikishie uhuru wa kazi zao.