The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hatimaye majaribio ya treni ya umeme yafanyika leo 

Shirika la Reli Tanzania (TRC) leo Februari 26, 2024 limefanya majaribio yake ya kwanza ya treni ya umeme ikiwa na abiria ndani kwa safari iliyoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro kisha Morogoro kurejea tena Dar es Salaam. 

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa, amesema kuwa treni hiyo itaanza rasmi kufanya safari zake mwisho wa mwezi wa saba huku akiwatoa hofu Watanzania juu ya changamoto za kukatika kwa umeme kuwa hazitaathiri ufanyaji kazi wake wa kazi.

Kuanza kufanya kazi kwa maradi huu kumekuwa kukikumbwa na danadana nyingi. Hali hii imekuwa ikiibua sintofahamu miongoni mwa Watanzania huku Serikali ikitoa sababu mbalimbali zinazokwamisha ikiwepo ya kuchelewa kwa vichwa vya treni na mabehewa.

Ujenzi wa reli hii ya kisasa kwa awamu ya kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro ulizinduliwa na Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Mgufuli mwaka 2017. Kipande hicho cha kwanza katika mradi huo kimeghrimu takribani dola za Kimarekani  bilioni 1.92.

Zanzibar yaondoa VAT kwenye Sukari kupunguza makali ya bei

Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi, leo Februari 26, 2024 ametangaza kuwa Serikali imeondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bidhaa ya sukari kwa ajili ya kupunguza makali ya bei ya bidhaa hiyo ambayo kwa sasa imekuwa ni adimu kupatikana. 

Rais Mwinyi ameeleza kuwa umamuzi huo umefikiwa kutokana na kupanda kwa bei ya sukari katika soko la nje hali ambayo inapelekea pia bei ya sukari katika soko la ndani kupanda kwa kiasi kikubwa hali ambayo inawaathiri Wazanzibar. 

Kwa hivi sasa bei ya sukari Zanzibar imepanda na kufikia kati ya shilingi 3,000 hadi 3,600 kutoka 2,000 mpaka 2,800 mwaka jana.

Mahitaji ya sukari Zanzibar kwa mwaka ni Tani 30,000 huku uzalishaji wa ndani ukiwa ni tani 10,000 kiasi kinachobaki huagizwa nje ya nchi. Kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni 15% inategemewa kupunguza makali ya bei ya sukari.

Serikali yasaini mkataba wa ujenzi wa matenki 15 ya mafuta bandari ya Dar es Salaam

Leo Februari 26, 2024 Serikali ya Tanzania na muungano wa kampuni mbili kutoka China zimesaini mkataba wa pamoja wa ujenzi na usanifu wa matenki na miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za mafuta katika bandari ya Dar es Salaam. 

Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi za Kitanzania bilioni 678.6 ukihusisha ujenzi wa matenki 15 ambayo yatatumika kwa ajili ya kuhifadhi mafuta ya petroli, diseli na mafuta ya ndege ambayo yatasambazwa sehemu tofauti tofauti nchini.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa, amaeeleza kuwa mradi huo utachukua muda wa miaka miwili hadi kukamilika na kuongeza kuwa Watanzania wajipange kunufaika na mradi huo kwani umelenga kutengeneza ajira na fursa za kutosha kwa ajili yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Plasduce Mbossa, ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza muda wa shughuli za ushushaji wa mafuta kwa bandari ya Dar es Salaam uliokuwa unachukua siku 11 kwa meli kubwa.