The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dk Mpango aguswa na malalamiko ya wananchi juu ya mfumo wa kodi 

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amekiri kuwa mfumo wa kodi nchini umekuwa ni kikwazo kwa wawekezaji kutokana na uwepo wa malalamiko mengi dhidi yake kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. 

Dk Mpango ameyasema haya leo Februari 27, 2024 wakati alipokuwa akifungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC). Jukwaa hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya uwekezaji na biashara kwa lengo la kujadiliana mazingira ya sekta hizo hapa nchini. 

Baadhi ya malamiko hayo aliyoyataja ni pamoja na utitiri wa kodi tozo na ada, sera za kodi zisizotabirika, viwango vya juu vya kodi lakini pia rushwa na mkadirio ya kodi yasiyoakisi uhalisia. 

Malalamiko mengine ni kutosomana kwa mifumo ya kielektroniki hasa katika taasisi za utoaji wa vibali, leseni na huduma nyingine. Lakini pia uwepo wa sheria na kanuni zinazokinzana na kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ya kitaasisi. 

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, yeye akaeleza kuwa kwa sasa Tanzania bado ina changamoto ya kukusanya mapato ya ndani kutokana na ulipaji wa kodi kwa hiari hasa matumizi ya mashine za kielektroniki na utoaji risiti kuwa bado ni mdogo huku ukikumbana na visingizio vingi.

CHADEMA yafanya maandamano ya mwisho ya awamu ya pili

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe leo Februari 27, 2024 ameongoza maandamano ya amani katika jiji la Arusha. Maandamano hayo yanakuwa ni ya mwisho kwa awamu hii ya pili mara baada ya kufanyika katika jiji la Dar es Salaam, Mwanza pamoja na Mbeya. 

Katika maandamano hayo Mbowe aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama hicho pamoja na wananchi ambao licha mvua kubwa kunyesha hawakuondoka barabarani ili kufanikisha adhma ya kufikisha ujumbe wao kwa Serikali.

Lengo la CHADEMA kuandamana ni kupinga miswada ya uchaguzi iliyopitishwa bungeni hivi karibuni, kuishinikiza Serikali irejeshe mchakato wa Katiba Mpya pamoja kuitaka Serikali ishughulikie masuala mbalimbali yanayosababisha kuongezeka kwa gharama za maisha.

Wakizungumza katika maandamano hayo, wananchi na wakazi wa jiji la Arusha wamedai kupanda kwa kiasi kikubwa kwa gharama za maisha ndiyo sababu iliyowafanya leo wajitokeze kuandamana kwa lengo la kuishinikiza Serikali iwasikilize.

Polisi Lindi washutumiwa kuificha kashfa ya ukatili wa kijinsia kwa mtoto inayomhusisha afisa wake

Jeshi la Polisi mkoani Lindi linakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kumkamata afisa wao anayedaiwa kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 13, baada ya kubainika kuwa chombo hicho chenye wajibu wa kusimamia ulinzi wa raia na mali zao kinajaribu kuificha kashfa hiyo ili kumlinda asichukuliwe hatua za kisheria. 

Afisa huyo ambaye anafahamika kama Madushi Mhogota Ng’wala, alikuwa akifanya kazi kwenye dawati la kijinsia la Kituo cha Polisi cha Liwale, anadaiwa kumbaka msichana wa darasa la sita kutoka shule moja ya umma ya Liwale. 

Inaelezwa kwamba Ng’wala alimvamia msichana huyo usiku wa Februari 18, 2024, wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwao kwenda kwa jirani kulala, akampeleka kichakani na kumbaka. 

Tukio ambalo limeleta hofu na hasira miongoni mwa wazazi na wanajamii wengine, ambao sasa wanaitaka polisi imkamate afisa huyo na kumchukulia hatua. 

Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, John Makuri, hakupatikana pale alipotafutwa na The Chanzo kwa njia ya simu kwa ajili ya kupata taarifa zaidi. Na alipotumiwa ujumbe wa maandishi hadi tunachapisha habari hii tulikuwa hatujapokea majibu kutoka kwake.