The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ndege ndogo yapata ajali Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Ndege ndogo ikiwa ikiwa na abiria watatu na rubani mmoja imepata ajali wakati ikitua katika kiwanja cha ndege cha Kogatende kilichopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 28, 2024 na Afisa Uhifadhi Mkuu Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania Catherine Mbena ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 6:52 mchana ikihusisha ndege ya kampuni ya Flight Link 5H-FLI. 

Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa bado hakijajulikana lakini abiria wote na rubani wapo salama.

Mwili wa Mtanzania waopolewa mto Miami, Marekani

Mwili wa Mtanzania Abraham Mgowano aliyekuwa akiishi nchini Marekani na kufanya kazi katika kampuni ya Google kama mhandisi wa programu endeshi umepatikana ukielea katika Mto Miami, jijini Florida baada ya kuanguka toka kwenye boti siku ya Jumamosi ya Februari 24, 2024. 

Polisi nchini humo wamesema kuwa walipokea simu kutoka kwa mtu aliyekuwepo eneo la tukio akisema kuwa ameona mwili ukiwa unaelea. 

Kituo cha televisheni cha 7news kimeripoti kuwa Mgowano alipata ajali hiyo akiwa na wenzake 12 ambapo polisi walianza kumtafuta bila mafanikio hadi walipopata taarifa kutoka kwa mtu huyo. 

Mgowano alimaliza kidato cha nne mwaka 2006 katika shule ya sekondari Loyola, Dar es Salaam. Na amefanya kazi katika kampuni ya Google kwa miaka tisa baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Stanford. 

Hospitali binafsi zagomea kitita kipya cha NHIF 

Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini vimeeleza kuwa kuanzia Machi 1, 2024 vituo binafsi vya afya vitashindwa kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na kutokubaliana na kitita kipya cha NHIF cha bei za huduma za afya. 

Uamuzi huo ambao umetolewa siku ya jana Februari 27, 2024 umetokana na kukwama kwa mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya vyama hivyo na Wizara ya Afya kupitia kamati iliyoteuliwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, kujadili kuhusu kitita hicho kipya.

Wakati sekta ya afya nchini ikiwa katika hali hiyo ya sintofahamu, Mkurugenzi wa NHIF Bernard Konga, leo Februari 28, 2024 amewaambia waandishi wa habari kuwa kitita hicho kitaanza kutumika kama ilivyopangwa kwani wanaamini kuwa kitakwenda kuwa chachu ya kufikia azma ya Serikali ya kutoa huduma bora za afya kwa watu wote. 

Bei mpya za kitita cha matibabu za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya zilitarajiwa kuanza kutumika tangu Januari 1, 2024. Hata hivyo wadau mbalimbali kama vile vituo binafsi vya afya hawakukubaliana na suala hilo hali ambayo iliwafanya kwa mara ya kwanza watishie kutotoa huduma kwa wanachama wa NHIF. 

Hali hiyo ilimlazimu Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mnamo Januari 5, 2024 kuchukua uamuzi wa kusitisha matumizi ya kitita hicho na kuunda kamati ambayo ilitarajiwa kuwakutanisha wahusika wote ili kulitafutia muafaka suala hilo.