The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

ATCL yasema tukio la ndege yake kupata hitilafu ikiwa angani ni la kawaida 

Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema kuwa tukio la kupata hitilafu kwenye moja ya injini za ndege yake aina ya Airbus A220-300 lililotokea siku ya Jumamosi Februari 24, 2024 wakati ndege hiyo ikitokea Dar es Salaam kwenda jijini Mbeya ni la kawaida na halikusababisha madhara yoyote kwa abiria au ndege. 

Siku ya tukio ndege hiyo ilikuwa na abiria 122 ndani yake ililazimika kukatisha safari na kurejea kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada kuibuka kwa moshi uliodumu kwa muda wa dakika tano ndani ya ndege hiyo na kisha kutoweka. 

Akitoa ufafanuzi huo leo Februari 29, 2024 mbele ya waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi, amesema kuwa  moshi huo ulitokana na injini moja kupata joto sana ilipokuwa inafanya kazi. Hali hiyo ilipelekea mafuta ya eneo hilo yaanze kutoa moshi uliozua taharuki na hofu miongoni mwa abiria. 

Hata hivyo watumishi na marubani wa ndege hiyo waliwasihi abiria kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa walijuwa kilichokuwa kinaendelea. Na baada ya kurejea kutua kila kitu kilikuwa sawa na abiria 104 waliendelea na safari huku 18 wakibadilishiwa ndege.  

Rais Samia: Wanaotaka kuandamana tutawalinda 

Rais Samia Suluhu amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha misingi ya utawala wa sheria kwa kuwapa uhuru vyama vya siasa kufanya shughuli zao huku akisisitiza kwamba kwa wale wanaotaka kuandamana wanaruhusiwa na watalindwa. 

Kauli hiyo imepatikana kutoka kwenye hotuba iliyowekwa hadharani leo Februari 29, 2024, aliyoitoa wakati akiongea na Watanzania waishio nchini Italia wakati alipokwenda huko kwenye ziara ya kikazi iliyodumu kwa siku mbili kuanzia Februari 11 hadi 12, 2024. 

Kauli hiyo ni ya kwanza kutolewa hadharani kutoka kwa kiongozi huyo katika wakati ambao chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA kimekuwa kikiendela kufanya maandamano yake katika mikoa mbalimbali ili kuishinikiza Serikali kutekeleza baadhi ya mambo ambayo wanadhani hayaendi sawa. 

Tangu aingie madarakani Rais Samia amekuwa akiruhusu kufanyika kwa baadhi ya mambo ambayo vyama vya siasa pamoja na wanaharakati mbalimbali walikuwa wakiyadai katika uongozi wa awamu ya tano. 

Mfano Januari mwaka jana Rais Samia aliruhusu mikutano vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara mara baada ya kuzuiliwa kwa miaka saba mfululizo. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia awasili nchini kwa ziara ya kikazi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia Abiy Ahmed Ali amewasili nchini leo Februari 29, 2024 kuanza ziara yake ya  kitaifa ya siku tatu iliyotokana na mwaliko wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Ali, amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba na hapo kesho atapokelewa rasmi katika Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake huyo. 

Ziara ya Waziri Mkuu huyo inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Ethiopia katika maeneo ya kimkakati ikiwemo usafirishaji kwa njia ya anga, nishati, kilimo na mifugo, biashara na uwekezaji na ushirikiano katika sekta za elimu, uhamiaji, na ulinzi na usalama.