The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tanzania Yadaiwa Kuwa Hatarini Kukabiliwa na Matukio ya Ugaidi 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Tanzania inakabiliwa na matishio ya kigaidi kutokana na mitandao ya ugaidi kuwachukua vijana wa Kitanzania wenye umri wa miaka kati ya 15 na 35 kisha kuwasafirisha ili wakajiunge na vikundi vya ugaidi vilivyopo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji pamoja na Somalia. 

Kutokana na hali hiyo amelitaka Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kuhakikisha linachukua tahadhari za mapema dhidi ya matukio ya kigaidi kwa kuwajua wahusika, kuvichambua vikundi vya ugaidi na kuangalia ni matukio gani ya kigaidi yanaweza kuikabili Tanzania hapo baadaye. 

Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa 7 wa mwaka wa Mkuu wa Majeshi na Makamanda wa JWTZ unaofanyika hapa jijini Dar es Salaam. 

Mwaka 2022 The Chanzo ilichapisha habari ya uchunguzi huko Zanzibar iliyoelezea namna vijana walivyokuwa wanasahiliwa kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi katika nchi za Somalia na Msumbiji. 

The Chanzo ilibaini kuwa uandikishaji wa  vijana hao ambao waliondoka na kuzitelekeza familia zao ulikuwa ukifanyika kwa mgongo wa mafundisho ya kidini. 

Jeshi la Polisi Labariki Maandamano ya CHADEMA

Kikao kilichofanyika baina ya chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro, kimefikia makubaliano ya kuwa maandamano yaliyopangwa kufanywa na chama hicho siku ya Jumatano, Januari 24, 2024 yaendelee kama yalivyopangwa. 

Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, kupitia ukurasa wake binafsi uliopo kwenye mtandao wa X zamani Twitter.

Mbowe amelipongeza Jeshi la Polisi kwa busara hiyo na kuwakaribisha Watanzania wote kuandamana kwa amani. 

CHADEMA ilitangaza uamuzi wa kufanyika kwa maandano hayo mnamo Januari 13, mwaka huu. 

Lengo la kufanyika kwa maandano hayo ni kuitaka Serikali iondoe miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 20 mwaka jana, kupunguzwa kwa gharama za maisha pamoja na kuanzishwa kwa mchakato wa maboresho ya Katiba ya mwaka 1977. 

Naibu Waziri Mkuu wa China Awasili Tanzania kwa Ziara ya Kikazi 

Naibu Waziri Mkuu wa China Liu Gouzhong, amewasili nchini Tanzania leo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu na kupokelewa na Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania Dk Doto Biteko. 

Ndani ya siku tatu hizo zinazoanza leo Januari 22 hadi 24, 2024, Waziri Gouzhong anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali. 

Tanzania na China ni nchi ambazo zimekuwa na ushirikiano kwa takribani miaka 60. Kwa sasa China imewekeza nchini zaidi ya miradi 1,100 ambayo imetoa ajira takribani 134,000.