Serikali yalikubali jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
Serikali imelikubali pendekezo la wadau mbalimbali zikiwemo Asasi za Kiraia na vyama vya upinzani waliotaka yafanyike marekebisho ya jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na iitwe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 30, 2024 wakati Bunge lilipokuwa likisoma kwa mara ya pili miswada mitatu ya sheria za uchaguzi ambayo imeanza kujadiliwa.
Florent Kyombo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ameliambia Bunge kuwa kabla Serikali ilikuwa na maoni ya kwamba kuongeza neno huru kwenye jina la sheria ni kubadili maudhui ya jina lililopo, ambalo linalotokana na ibara ya 74, kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Tanzania.
Hata hivyo kamati iliona kuwa matumizi ya neo huru hayakinzani na matakwa ya Katiba kwa kuwa Katiba haijaelekeza jina rasmi la kutumika na tume.
Katika taarifa yake iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama, Serikali imeonekana kukubaliana na maoni hayo ya kamati na wadau wengine.
Kamati ya Bunge yapendekeza isiwe lazima Wakurugenzi kusimamia uchaguzi
Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria imependekeza kuwa Serikali isiweke ulazima wa kuwafanya Wakurugenzi wa miji, majiji na halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Hayo yamebainishwa leo Januari 30, 2024 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Kizito Mhagama, wakati alipokuwa akiwalisha taarifa yao kwa Bunge wakati wa mjadala wa sheria za uchaguzi iliyosomwa kwa mara ya pili.
Mhagama amelieleza Bunge kuwa inatakiwa kuwepo na masharti ya mtumishi wa umma mwandamizi au mtu mwingine yeyote mwenye sifa kuteuliwa kuwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
Suala la Wakurugenzi kusimamia uchaguzi limekuwa likipingwa vikali na wadau mbalimbali nchini. Juni 13, 2023 Mahakama ya Afrika ya Haki na Haki za Binadamu (ACJHR) ilitoa maamuzi kwamba wakurugenzi hawapaswi kuendela kusimamia uchaguzi.
Hiyo ni katika kesi iliyofunguliwa na Bob Chacha Wangwe pamoja na LHRC.
Katika madai yao waliieleza mahakama kuwa vifungu vya 6(1), 7(1), 7(2) na 7(3) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, vinavyoruhusu wakurugenzi kusimami uchaguzi, vinakiuka vifungu mbalimbali vya mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Sekta ya uvuvi yadaiwa kutoa mchango mdogo kwenye pato la taifa
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwamba mchango wa asilimia 1.8 tu kwenye pato la taifa unaotolewa na sekta ya uvuvi ni mdogo sana ukilinganisha na rasilimali za uvuvi ambazo nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nazo.
Ameendelea kueleza kuwa ukuaji wa asilimia nne kwa mwaka wa sekta ya uvuvi pamoja na mauzo ya nje ya mwaka bado ni madogo sana hali ambayo inahitaji kuchukuliwa hatua ili Tanzania iweze kufanya vizuri zaidi ya hapo.
Rais Samia ameyaeleza hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mwanza kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Nyamagana. Na kabla ya hapo alishiriki zoezi la uzinduzi wa vizimba vya kufugia samaki pamoja na kugawa boti 160 kwa wavuvi waliokopeshwa.
Kwa muda mrefu sekta ya uvuvi imeweza kuajiri Watanzania wengi ambao wanamudu maisha yao ya kila siku kupitia shuguli zake. Tanzania ina wavuvi takribani 197, 763 na wakuzaji wa viumbe maji 34,05. Aidha, mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya uvuvi umeajiri karibu watu 6,000,000.