The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ilala imebaini kuwa miradi mitatu ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na ujenzi yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.35 ina mapungufu. 

Sehemu ya mapungufu yaliyobainika ni pamoja na ukiukwaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma, kutofanyika kwa vipimo vya ubora wa vifaa vya ujenzi, usimamizi duni uliosababisha matumizi ya vifaa visivyokidhi ubora na ucheleweshwaji wa miradi. 

Hayo yameelezwa leo Januari 31, 2024 na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ilala Sosthenes Kibwengo, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji wao katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2023. 

Kibwengo ameendelea kueleza kuwa miradi hiyo yenye mapungufu imebainika miongoni mwa miradi tisa iliyokaguliwa ambapo ni sawa na asilimia 33. Jambo ambalo lina unafuu ukilinganisha na ripoti ya miradi iliyokaguliwa kati ya Oktoba na Disemba mwaka 2022. Kwani kipindi hicho upungufu ulikuwa ni kwa asilimia 78. 

Wabunge wataka sheria itambue makosa ya ukatili wa kijinsia kwenye uchaguzi

Baadhi ya wabunge wamepaza sauti zao wakitaka suala la unyanyasaji wa kijinsia litambuliwe kama kosa katika kipindi cha uchaguzi. 

Wito huo umetolewa wakati wa mjadala wa Bunge kujadili miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 30, 2023 na kusomwa kwa mara ya pili jana Januari 30, 2024. 

Miswada hiyo imeonekana kutokugusia suala la makosa ya ukatili kijinsia hali ambayo imewafanya baadhi ya wabunge kutumia mifano yao dhahiri iliyowakuta ili kushinikiza suala hilo kifanyike. 

Mmoja wa wabunge hao ni Anne Kilango Malecela, mbunge wa Same Mashariki ambaye amelieleza Bunge kuwa yeye ni mwathirika wa unyanyasaji wa kijinsia tangu aliposhiriki uchaguzi wa kwanza mwaka 2005. 

Katika kuiongezea nguvu hoja hiyo Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria pia imependekeza kuwa sheria mpya ya uchaguzi iangazie pia makosa ya ukatili wa kijinsia. 

TMA yatoa tahadhari ya mvua kubwa kunyesha kwa siku tano

Mamlaka ya Hali ya Hewa imetoa tahadhari juu ya mvua kubwa kuendelea kunyesha kwa siku tano zijazo katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Mtwara, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma. 

Aidha, TMA imeeleza kuwa huenda kukawa na athari katika baadhi ya maeneo ya makazi kwa kuzungukwa na maji lakini pia kuathirika kwa shughuli za kiuchumi. 

Katika siku za hivi karibuni mvua hizi zimesababisha usumbufu mkubwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini. 

Itakumbukwa kuwa leo pia Shirika la Reli Tanzania kimetangaza kusitisha safari za treni kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Katavi, Kigoma na njia ya kuelekea mikoa ya Kaskazini kutokana na mvua kuharibu miondombini ya reli.