Utekelezaji finyu mapendekezo ya CAG yawaumiza vichwa wadau, watoa mapendekezo haya
Wadau mbalimbali wamemtaka Mdhibiti Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aone umuhimu wa kuikutanisha ofisi yake, maafisa masuhuli, kamati za Bunge za usimamizi, kamati ya hesabu za Serikali Kuu, kamati ya Serikali za mtaa na kamati ya uwekezaji ili watafute suluhu ya utekelezaji finyu wa mapendekezo ya ripoti za CAG.
Wito huo umetolewa leo Julai 16, 2024, jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa ripoti nne za uwajibikaji za taasisi ya Wajibu kwa mwaka 2022/2023, ripoti ambazo zimetokana na ripoti za CAG za mwaka 2022/2023.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa taasisi ya Wajibu, Ludovick Utouh, amesema kuwa wito huo umetolewa kwa sababu kwa miaka mingi utekelezaji wa mapendekezo ya CAG haujawa wa kuridhisha. Mara nyingi hutekelezwa kwa asilimia 40, kwa hiyo asilimia 60 na zaidi yanabaki hajatekelezwa.
Taasisi ya Wajibu imekuwa ikitoa ripoti za uwajibikaji kila mwaka. Lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mambo muhimu yaliyoibuliwa kwenye ripoti za CAG.
Wajibu huzisambaza ripoti hizo kwa wananchi lakini pia zinapatikana mtandaoni kwenye tovuti yao ya www.wajibu.or.tz
Tanzania na Oman zasaini maboresho ya mkataba wa usafiri wa anga
Tanzania na Oman zimesaini maboresho ya Mkataba wa Usafiri wa Anga (BASA) ili kuyawezesha mashirika ya ndege kutoka mataifa hayo kusafiri baina ya pande hizo bila kujali idadi ya safari au ukubwa wa ndege husika.
Kusianiwa kwa mkataba huo kutayawazesha mashirika ya ndege yasiyokuwa na ndege pia kuungana na yale yanayomiliki ndege ili kuendesha biashara kwa pamoja.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika leo Julai 15, 2024, na kushudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, aliyeiwakilisha Tanzania na kwa upande wa Oman waliwakilishwa na Rais wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga wa nchi hiyo, Ali Nabri.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mbarawa amesema kuwa mkataba wa awali ulisainiwa mwaka 1982, hivyo maboresho yalikuwa ni muhimu.
Mbarawa ameongeza kuwa mkataba huu wa sasa utafungua fursa mpya za usafiri baina ya nchi mbili hizi, kuleta ongezeko la abiria pamoja na kukuza biashara na uchumi.
Kwa upande wa Nabri amesema kuwa mkataba huo ni sehemu muhimu sana katika kuongeza ushirikiano kati ya Tanzania na Oman, lakini pia ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa nchi zote mbili.
Tanzania, Marekani kushirikiana kupambana na ugonjwa wa saratani
Taasisi ya Biden Cancer Moonshot ya Marekani imeahidi kutoa ongezeko la kiasi cha dola za Kimarekani milioni 10 ambazo ni sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 300 kwa ajili ya kusaidia mapambano ya ugonjwa wa Saratani hususani katika nchi za Afrika.
Hayo yamebainishwa leo Julai 16, 2024, huko Washington DC, Marekani, wakati wa kikao kilichofanyika baina ya taasisi hiyo na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu, aliyembatana Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassoro Mazrui.
Fedha hizo zinatarajiwa kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na uhaba wa wataalamu, ukosefu wa miundombinu wezeshi, vifaa tiba hususani vya kutoa huduma za mionzi, takwimu, tafiti pamoja na ubunifu ili kuwezesha wananchi wake kupata huduma bora za saratani bila kikwazo.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mwalimu amesema kuwa ugonjwa wa Saratani umekuwa ni changamoto kubwa nchini Tanzania ambapo inakadiriwa kuwa kuna ongezeko la wagonjwa wapya wa Saratani takribani 45,000 kila Mwaka.
Kwa upande wake mratibu wa taasisi hiyo, Catherine Young, wakati akifungua kikao hicho amesema kikao hicho muhimu kilikuwa ni kwa ajili ya kuwaleta pamoja wadau wakubwa wanaojishughulisha na ugonjwa wa Saratani ili kuwezesha nchi Afrika kupambana vyema na huo.