The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Somalia rasmi mwanachama mpya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Leo Machi 04, 2024, taifa la Somalia limekuwa mwanachama rasmi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mara baada ya kukabidhi hati ya kuridhia kujiunga kwake katika makao makuu ya EAC yaliyopo jijini Arusha, Tanzania. 

Hatua hii inaifanya Somalia kuwa mwanachama wa nane wa jumuiya hiyo ambayo tayari ilikuwa na wanachama saba ambao ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC na Sudan ya Kusini.

Ombi la Somalia kujiunga na EAC liliwasilishwa na Rais wake Hassan Sheikh Mohamud, mnamo Julai 21, 2022 alipoalikwa kwenye mkutano wa viongozi wa jumuiya hiyo. 

Novemba 11, 2023, aliyekuwa Mwenyekiti wa EAC, ambaye pia ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alitangaza kuwa ombi la Somalia lilikuwa limekubaliwa. Kauli hiyo iliruhusu michakato mingine ya kupata uanachama rasmi kuendelea. 

Somalia ni nchi ambayo ina takribani raia milioni 18. Katika miongo ya hivi karibuni, taifa hilo limekuwa na hali duni ya kiusalama, hali ambayo EAC itakabiliwa na jukumu la kuitafutia suluhu. 

TPA yakanusha uwepo wa mgomo kwenye bandari ya Dar es Salaam

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa mgomo wa wafanyakazi kwenye bandari ya Dar es Salaam, hali iliyopelekea kudorora kwa utendaji kazi katika kuhudumia meli na shehena za mizigo. 

Taarifa hizo zilidai kuwa wafanyakazi waliamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu hawakubaliani na kitendo cha kufutiwa mikataba yao ya kazi kilichotokana kampuni ya DP World kutaka kufanya kazi na watu itakaowaleta. 

Taarifa iliyotolewa na TPA kwa vyombo vya habari leo Machi 4, 2024, imeeleza kuwa shuguli zote zinaendelea kama inavyotakiwa kwenye bandari hiyo na hakuna meli ama mzigo ambao umekwama.

Babu Duni ajitoa kinyang’anyiro cha Mwenyekiti wa ACT Wazalendo

Mwenyekiti wa Chama cha ACT  Wazalendo anayemaliza muda wake, Juma Duni Haji, maarufu kama Babu Duni, amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa chama hicho na kumuunga mkono Othman Masoud Othman ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Babu Duni amejiondoa kutetea nafasi hiyo aliyokuwa akihudumu kabla ya muda wake kuisha leo Jumatatu Machi 4, 2024, ikiwa imesalia siku moja kabla ya mkutano mkuu wa chama hicho kufanyika ili kuchagua viongozi wake wakuu. 

Awali, kulikuwepo na mchuano mkali baina ya wagombea hao, hali ambayo ilimuibua Babu Duni kulalamikia hujuma za watu waliokuwa wanamshinikiza ajiondoea kwenye kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.