The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tanzania, Ethiopia zasainiana hati tatu za makubaliano

Tanzania na Ethiopia zimetiliana saini hati tatu za makubaliano kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya utamaduni na sanaa, kilimo pamoja na biashara. 

Zoezi hilo limefanyika leo Machi 1, 2024, jijini Dar es Salaam mbele ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali ambaye yupo nchini tangu jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu. 

Mbali na kushuhudia utiaji saini wa hati hizo viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo ambayo yamelenga kujadili masuala mbalimbali yanayoyahusu mataifa hayo. 

Tanzania na Ethiopia ni nchi ambazo zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia kwa muda mrefu ukiasisiwa na Hayati Julius Nyerere na Mtawala wa Ethiopia Hayati Haile Salassie. Viongozi hao walishirikiana kupigania uhuru wa bara la Afrika na walikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Umoja wa Afrika mwaka 1963.

Hayati Ali Hassan Mwinyi aagwa Dar 

Maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam leo Machi 1, 2024, wamejitokeza katika barabara mbalimbali na kwenye uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi. 

Taarifa za kifo cha Rais huyo, aliyepewa jina la utani la ‘Mzee Rukhsa,’ zilitangazwa jana na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliuambia umma kuwa Mwinyi amefariki katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu. 

Kiongozi huyo ambaye aliingia madarakani mwaka 1985 akipokea kijiti kutoka kwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kung’atuka mwaka 1995 anatarajiwa kuzikwa huko visiwani Zanzibar hapo kesho Machi 2, 2024. 

Baadhi ya waombolezaji wamemuelezea Mwinyi kama kiongozi wa mfano wa kuigwa na viongozi wa sasa, hiyo ni kwa jinsi alivyosimamia sera ya mageuzi ya kiuchumi na kuruhusu mfumo wa soko huria. 

Serikali yazitaka hospitali binafsi ziheshimu mikataba majadiliano yakiendelea

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, leo Machi 1, 2024, amezitaka hospitali binafsi ziheshimu mikataba yao ya utoaji huduma katika wakati ambao majadiliano yao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya juu ya kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 yakiendelea. 

Kauli ya Mwalimu inakuja kufuatia baadhi ya hospitali kuanza kutekeleza mpango wa kutotoa huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo kwa sababu hawakubaliani na kitita hicho. 

Kitita cha mafao cha mwaka 2023, kilitangazwa kuwa kitaanza kutumika leo Machi 1, 2024. Taarifa hiyo iliwafanya wamiliki hospitali binafsi kutangaza mapema kuwa watasusia utekelezaji huo kwa sababu mazungumzo ya kwanza yaliyokuwa yanafanyika kujadili mustakabali wa kuanzia kutumika kwake yalikwama. 

Mara ya mwisho NHIF kufanya maboresho ya kitita cha mafao ilikuwa ni mwaka 2016. Hali hii inayoendelea hivi sasa inawaweka mashakani wanufaika wa NHIF takribani milioni 4.9 ambao wamesajiliwa kwa ajili ya kupata huduma za afya katika vituo vya matibabu zaidi ya 9,000 vilivypo nchini.