Rais Samia akemea tabia ya kuvunja mikataba hovyo
Rais Samia Suhulu Hassan amewataka wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuzingatia sheria pale wanapotaka kusaini au kuvunja mikataba na taasisi mbalimbali ili kuiepusha Serikali kufikishwa mahakamani kwa madai ya kukiuka matakwa ya kimikataba.
Wito huo ameutoa leo Jumatano Machi 13, 2024, wakati alipokuwa akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua katika siku za hivi karibuni, zoezi ambalo limefanyika katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais Samia ameeleza kuwa maamuzi ya kusaini na kuvunjwa kwa mikataba yanayofanywa na viongozi hao yamekuwa yakifanyika kiholela, hali hiyo imekuwa ikipelekea Serikali kufikishwa mbele ya mahakama za ndani na za kimataifa na kisha kuamuriwa kulipa gharama nyingi.
Masuala yanayohusu mikataba nchini yanasimamiwa na Sheria ya Mikataba Sura ya 345 iliyorekebishwa mwaka 2019. Katika kesi za hivi karibuni ambazo Serikali imeshtakiwa zipo ilizoshinda na ilizoshindwa, ambapo iliamuriwa kulipa mabilioni ya fedha.
Serikali ya Zanzibar yawataka wananchi waache kula kasa
Wizara ya Afya ya Zanzibar imewataka wananchi waache kula nyama ya kasa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kifo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 13, 2024, na Naibu Waziri wa wizara hiyo Hassan Khamis Hafidh, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mnazimmoja.
Kutolewa kwa taarifa hii kumetokana na tukio la hivi karibuni la vifo vya watu tisa lililotokea katika mkoa wa Kusini Pemba, ambapo watu wengine 18 wakilazwa katika hospitali ya Abdulla Mzee mara baada ya kula nyama ya kasa.
Akitoa taarifa yake, Mkemia Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Faridi Mzee Mpatani, ameeleza kuwa kwa kushirikiana na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Tanzania, wamefanya uchunguzi wa kitaalamu na kubaini uwepo wa sumu katika nyama hiyo, sumu ambayo inahimili joto kiasi kwamba hata ikipikwa haiwezi kutoka.
Watu 23 wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, (DCEA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga watu 23 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Washtakiwa hao wamefikishwa mbele ya mahakama kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya aina ya bangi, heroini na mirungi, kitendo ambacho ni kinyume na sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Akisoma shauri hilo leo Machi 13, 2024, mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Christina Chovenye, wakili wa Serikali John Hamenya, amesema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti tofauti katika mwezi Februari na Machi 2023.
Tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya limekuwa likiwaathiri vijana wengi hapa nchini. Takwimu kutoka kwenye vituo vya tiba saidizi kwa waraibu wa kutumia dawa za kulevya zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba hiyo kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915.