Migodi ya madini yafanya manunuzi ya zaidi ya Trilioni 3 kutoka kwenye makampuni ya Tanzania
Imeelezwa kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2022/2023, migodi ya madini nchini ilifanya manunuzi ya dola bilioni 1.6, ambapo dola bilioni 1.4 sawa na takribani Trilioni 3 za kitanzania zilihusisha kampuni za Kitanzania na hivyo kufanya zaidi ya asilimia 86 ya manunuzi yote ya migodi mikubwa katika mwaka huo yawe yamefanywa na Watanzania.
Hayo yamebainishwa leo Machi 21, 2024, na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati wa hafla ya kukabidhi leseni kubwa kwa kampuni za uchimbaji na usafishaji madini za Nyati Heavy Mineral Sands na Tembo Nickel Refining Company Limited.
Mavunde ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya Madini, mabadiliko ambayo yaliweka sharti la lazima la ushiriki wa Watanzania kwenye sekta hiyo, hali ambayo imepelekea makampuni ya Kitanzania kupata fursa ya kutoa huduma na kusambaza bidhaa migodini.
Kwa upande wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, Mavunde amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la kasi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kwani idadi ya watu wanaopata ajira moja kwa moja katika sekta hiyo imeongezeka kutoka 17,000 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hadi kufikia 19,000 mwaka huu.
Watalii milioni moja na nusu watembelea hifadhi
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limesema kuwa kwa mwaka 2023/2024 idadi ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa imeongezeka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia watalii 1,514,726 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.
Kati ya watalii hao, watalii wa ndani ni 721,543 na wa nje ni 793,183, ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 5, ikiwa ni zaidi ya lengo lililowekwa la kupokea watalii 1,387,987 katika kipindi hicho.
Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Nassoro Juma Kuji, ameeleza kuwa kwa mwaka huu matarajio ya idadi ya watalii watakaotembelea Tanzania ni 1,830,081, ambapo watalii wa ndani ni 866,667 na wa kimataifa ni 963,413.
Kuji ameeleza kuwa mafanikio hayo yanathibitisha juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya utalii, huku akiitaja filamu ya Tanzania: The Royal Tour kuhusika kuchangia ongezeko hilo.
Mawakili, wanasheria waonywa kufanya kazi kwa mrengo wa kisiasa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa mawakili na wanasheria kuepuka kufanya kazi kwa mrengo wa kisiasa na kuwasisitiza kuzingatia kanuni za kitaaluma kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Majaliwa ameyasema hayo leo Machi 21, 2024, jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali wa Tanzania, mkutano ambao ni jukwaa la kitaluma la wanasheria katika utumishi wa umma ambalo hufanyika mara moja kila mwaka.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, amewaasa mawakili kutumia sheria kuleta maendeleo kwa Watanzania na kuiwezesha nchi kushindana kimataifa.
Profesa Juma ameeeleza kuwa uwepo wa sheria nzuri pekee hautoshi kufikia malengo ya maendeleo, kwani tabia na tamaduni zinaweza kuzuia utekelezaji wake.